chukua tahadhari, shetani yupo kazini

Maswali ya Biblia No Comments

 

Shalom mtu wa Mungu.Jina la Bwana libarikiwe.
Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Ayabu 1:6 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao.

7 BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, NATOKA KATIKA KUZUNGUKA-ZUNGUKA DUNIANI, NA KATIKA KUTEMBEA HUKU NA HUKU HUMO.

Bila shaka kama wewe ni msomaji mzuri wa biblia… Naamini umeshasoma hichi kitabu cha Ayubu na kuna mengi Roho Mtakatifu amekufundisha. Sasa leo kwa Neema za Mungu tutajifunza jambo lingine ambalo yamkini bado hujalifahamu.

Mwanzoni kabisa mwa kitabu hiki kabla Ayubu hajaenda kupitia katika majaribu yale… tunasoma BWANA alikutana na Shetani na akamwuliza swali kwamba umetoka wapi? Na Ndipo Shetani akamjibu Bwana na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huko..

Sasa tutafakari hilo jibu la Shetani vizuri, maana somo letu limeegemea hapo,

Sio kwamba Bwana hakujua kwamba Shetani alitoka wapi mpaka amuulize, Bwana alikuwa anajua kwani hakuna jambo asilolijua maana yeye ni Mungu. Ila alimwuliza kwa ajili ya faida yetu sisi…tupate kujifunza na kuelewa kazi za Shetani hapa duniani, na Shetani anatudhihirishia kuwa yupo hapa duniani na hana makao rasmi bali anazunguka-zunguka tu na kutembea huku na huko ni mzururaji,

Sasa jiulize kwanini anazunguka-zunguka hapa duniani?

Kwanini asiende kukaa na kutulia huko kuzimu asubirie hukumu yake, huku duniani anatafuta nini?

Biblia imeweka wazi kwamba anazunguka-zunguka akitafuta mtu ammeze na hilo tunalithibitisha hapa..

1Petro 5:8 Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.

Umeona hapo!. Shetani yupo kazini, anazunguka-zunguka kila siku amtafute mtu ammeze, na sio kila mtu bali ni wana wa Mungu, watu waliozaliwa mara ya pili kwa mapenzi ya Mungu. Ndio hao shetani anawawinda usiku na mchana kama vile mtumishi wa Mungu Ayubu,

Usidhani kuwa Shetani alikuwa mbali na Ayubu, alikuwa anamtafuta kwa kila namna ili aweze kummeza, pamoja na kuwa Ayubu alikuwa ni mtu aliyekuwa mkamilifu, mtu aliyemcha Mungu na kuepukana na uovu, ila hicho haikumfanya Shetani amkatie tamaa, ila alikuwa anamtafuta kwa kila kona yaani kwenye mali zake, familia yake, kazi zake, afya yake n.k, ndio maana alipoona kuwa ameshindwa kummeza Ayubu, alimwambia Bwana kuwa ni kwasababu umemzingira pande zote.

Ayabu 1:8 Kisha BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.

9 Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu Yuamcha BWANA bure?

10 Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.

Hata leo bado Shetani hajabadilika, ni yule yule aliyemdanya Hawa pale Hedeni na ndio yule yule aliyetaka kummeza Ayubu, ndio yule yule aliyetaka kumwangusha Bwana Yesu kwa majaribu yake, Shetani yupo kazini, anazunguka-zunguka kila siku akitafuta kukumeza wewe mtu uliyeokoka,

anatutafuta sisi sote, usidhani kuwa Shetani anafurahia wokovu wako, usidhani kuwa anafurahia mafanikio yako uliyopewa na Mungu, chochote ulichonacho iwe ni kazi, elimu, watoto, n.k, shetani anataka akuharibie, anataka ameze afya yako, kazi yako, huduma yako, na mwisho akutenge kabisa na Mungu, Ukilijua hilo utakaa kwa tahadhari katika hii dunia ukijua kuwa shetani yupo kazini, anazunguka-zunguka kila mahali, hata hapo ulipo yupo, hapo kazini, shuleni shetani yupo na anakutafuta wewe maadamu we ni uzao wa Mungu…

Hapa namaanisha Mkristo halisi aliyejazwa Roho Mtakatifu na anatembea katika njia ya Bwana na kufanya mapenzi yake, fahamu kuwa shetani anakuwinda, unachopaswa kufanya ni kuwa kama Ayubu.

Sasa Ayabu alikuwaje? Maandiko yanasema

Alikuwa ni mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.

Ayubu 1:1

[1]Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu.

Unapokuwa mtakatifu wa mwilini na rohoni, na kutii Neno la Mungu hapo shetani hawezi kukupata kwa njia yoyote, tena kadiri utakavyozidi kumtafuta Mungu na kutafuta kufanya mapenzi yake na kumtii kwa kila neno, Ndipo utakavyozidi kumweka shetani mbali.

Yakobo 4: 7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.

Pia unapokuwa mjinga kwa kutozifanya na kuzifuatilia mambo ya kidunia, kama mipira, movies, magemu, kamari, fashion, na anasa zote za kidunia hapo unakuwa unamweka shetani mbali.

Warumi 16:19 Maana utii wenu umewafikilia watu wote; basi nafurahi kwa ajili yenu, lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima mambo mabaya.

20 Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi.

Umeona hapo, unapokuwa mjinga kwa kutozifanya mambo maovu unampa Mungu nafasi ya kumseta shetani chini ya miguu yako, yaani kwenye Kazi yako, elimu yako, huduma yako, familia yako n.k shetani anakosa nguvu, ila ukiwa unashikamana na mambo ya kishetani na bado unataka shetani akuache, ukweli ni kwamba Shetani hatakuacha na ataendelea kukumeza, na kuharibu maisha yako,

Mungu hatakulinda ikiwa una mali za shetani, una vitu vya shetani, mfano we ni mwanamke na umevaa mahereni, mawigi, umepaka rangi usoni, kwenye kucha, na unategemea ulinzi kwa Mungu! hilo jambo sahau kabisa, Mungu atawezaje kukulinda na huku una vitu vya kishetani? na unafahamu shetani kama jina lake lilivyo ni mshitaki, ni lazima tu akushitaki kwa vitu vyake na Mungu ni wa haki hana upendeleo, hawezi kukulinda na huku shetani anadai vitu vyake ulivyoviweka kwenye mwili wako,

kwahiyo unapoona mambo yako hayaendi, uchumi wako unayumba, usikimbilie tu kumlalamikia Mungu au kuhangaika huku na huku kutafuta maombezi, angalia kwanza je! Kwenye mwili wako umevaa nini? hivyo Kabla hujaenda kuomba msaada kwa Mungu kubali kuondoa mapambo yote kwenye mwili wako na ubaki kama Mungu alivyokuumba na asili yako  hata kama utaonekana mjinga,

kumbuka hili neno

Warumi 16:19 “…. lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya.

20 Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi.”

Kwa kuhitimisha ishi kulingana na Neno la Mungu ndivyo utakavyozidi kumpinga shetani na kumfanya akae mbali na wewe, neno linaposema vaa mavazi ya kujisitiri, litii Neno la Mungu, Bwana anapokuambia acha pombe,acha uzinzi,acha kujichua,acha mambo yote mabaya unaacha haraka, tena unaikimbia dhambi kama alivyofanya yusufu mbele ya mke wa potifa, lakini ukienda kinyume shetani atakumeza tu,

Kumbuka shetani hana habari na wewe kama upo nje ya wokovu, ikiwa ujaokoka fahamu kabisa shetani kashakumeza, lakini habari njema ni kuwa unayo nafasi kutoka kwenye mikono yake adui, ni kwa kumaanisha kabisa kumpokea Bwana Yesu moyoni mwako kwa kutubu na kubatizwa ubatizo sahihi ili upokee Roho ambaye atakulinda na mitego yote ya adui,

Na ikiwa umeshaokoka zidisha bidii yako Katika kumtumikia Mungu, kujitenga na dhambi,na mambo yote mabaya, kuwa mtu wa kusoma biblia takatifu,kuwa mtu wa maombi na kuwashuhudia wengine habari njema ndivyo utakavyomuweka shetani chini..

Shalom,Maran atha

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312  au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *