Je! Umepatanishwa na adui zako?
Mithali 16:7 “Njia za mtu zikimpendeza BWANA, Hata adui zake huwapatanisha naye.
Kama tunavyofahamu kuwa adui wetu mkubwa tunayepambananae ni ibilisi pamoja na mapepo yake, adui wa pili ambaye anatuharibia mahusiano yetu na Mungu ni dhambi. Sasa tukilijua hilo..hatutapoteza muda kupambana na wanadamu wenzetu kwa kuwachukulia kama ni maadui. Ni kweli kwa jicho la nje wanaonekana ni maadui kwasababu ya chuki na visa wanavyotutendea.. lakini tunapaswa tuende mbali zaidi, tuelewe kuwa ni ile roho ya ibilisi na dhambi iliyo ndani yao ndiyo inawafanya wawe hivyo.
Hakika tukijua hivyo, tutakuwa watu wa kiroho sana waliokomaa, hata siku moja hatutarushiana maneno wala kusosana nao, kinyume chake tutawapenda na kuwaombea daima wafunguliwe. Na hapo tufanyavyo hivyo ndivyo tunapompendeza Baba na hakika yeye atatimiza hili Neno alilolisema..
“Njia za mtu zikimpendeza BWANA, Hata adui zake huwapatanisha naye”.
Kwa sababu yeye analitazama Neno lake ili alitimize ndivyo anavyosema, Na maadui ambao Bwana atatupandanisha nao sio shetani na mapepo yake bali ni watu ambao shetani huwatumia kutuletea uharibifu.
Sasa utauliza ni kwa namna gani? Bwana ana njia nyingi ya kutupandanisha nao, lakini moja ya njia ambayo ni ya wazi ni kwa kuwageuza mioyo yao watubu na kumuacha ibilisi na kazi zake yaani matendo yote ya giza, na hii inakuja kwa sisi kumpendeza kwanza Mungu (yaani tukiwa tunafanya mapenzi yake/utakatifu ambayo ni pamoja na kuwaombea maadui zetu, yaani watu wanaotuchukia). Tukiwa watu wa namna hiyo, hatutahudhurika na mabaya yote yanayotumwa kwetu, utashangaa wale watu ambao wanakupangia njama wakudhuru, Ndio kwanza wakifika kwako wanachomwa mioyo yao na mwisho ni wao kutubu, kipindi Fulani Sauli alituma wajumbe wakamkamate Daudi, lakini kwa kuwa Daudi alikuwa ni mtu aliyempendeza Mungu..wale wajumbe walipofika kwake, Mungu akawageuza mioyo yao.. mbadala wamkamate Daudi wakaanza kutabiri matendo makuu ya Bwana na hatimaye Sauli baadaye alipofika naye akaanza kutabiri. Tunasoma.
1 Samweli 19:19-24 Naye Sauli akaambiwa, kusema, Angalia, yule Daudi yuko katika Nayothi, huko Rama.
[20]Basi Sauli akatuma wajumbe ili kumkamata Daudi; nao hapo walipowaona jamaa ya manabii wakitabiri, na Samweli amesimama kama mkuu wao, roho ya Mungu ikawajilia wajumbe wa Sauli, nao pia wakatabiri.
[21]Naye Sauli alipoambiwa, alituma wajumbe wengine, wao nao wakatabiri. Naye Sauli akatuma wajumbe tena mara ya tatu, na wao pia wakatabiri.
[22]Kisha yeye mwenyewe akaenda Rama, akafika kunako kile kisima kikubwa kilicho huko Seku; akauliza, akasema, Je! Wako wapi Samweli na Daudi? Na mtu mmoja akajibu, Tazama, wako Nayothi, huko Rama.
[23]Basi akaenda Nayothi huko Rama, na roho ya Mungu ikamjilia yeye naye, akaendelea mbele, huku anatabiri, mpaka kufika Nayothi huko Rama.
[24]Naye akavua nguo zake, akatabiri mbele ya Samweli, akalala uchi mchana kutwa na usiku kucha siku ile. Kwa hiyo watu husema, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?
Hauhitaji kutumia nguvu kubwa kupambapana na wanadamu wenzako, kuwaombea mabaya na kuwasema vibaya.. ukifanya hivyo unakosea na hautakuwa na amani katika maisha yako. kwasababu Roho Mtakatifu hatatembea na wewe katika utumilivu wote, utaishia tu kuwa mtu wa visasi na chuki, Kwahiyo unachopaswa kufanya ni kuwapenda watu wote na kuwaombea wale wanaokuudhi. Ndivyo Bwana alivyotufundisha
Mathayo 5:43 Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;
[44]lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,
[45]ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.
[46]Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?
[47]Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?
[48]Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
Bwana wetu Yesu Kristo ni mfano kamili wa sisi kujifunza?..Alikuwa na maadui lakini waligeuzwa wote kuwa Rafiki zake, Hata wale waliomsulubisha msalabani aliwaombea msamaha na kwa kupitia damu yake kwa yeye ulimwengu umepatanishwa na yeye…Ndio maana mpaka leo Rafiki wa kweli amebakia kuwa Yesu tu!
Lakini maandiko yanatuambia katika..
Wafilipi 2:5 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu”
Je! Waislamu ni maadui zako?”
Jifunze kwa Bwana Yesu aliye njia na kweli, yeye alichukiwa na watu wa kila kabla lakini aliwapenda wote..hata kipindi ambapo wale Wasamaria walimkata kumkaribisha huyu mkuu wa uzima, wanafunzi wake walimwambia agiza moto ushuke na kuwa ngamiza wote, yeye alikuwa na huo uwezo wa kufanya hivyo lakini aliwaambia ”hamjui ni roho ya namna gani mliyonayo” (Luka 9:52-56). Na mbele kidogo..Wasamaria wote walihubiriwa Neno la uzima wakaokoka karibu mji wote.
Hebu jiulize je! Majirani zako ni maadui zako kiasi cha kutaka hata moto ushuke uwateketeze? Kama ndivyo basi Bwana Yesu anakuambia “hamjui ni roho ya namna gani mliyonayo!..Jifunze kwa Bwana Yesu hapo juu Paulo anasema Iweni na nia iyo hiyo …Je! Wafanyakazi wenzako ni maadui zako kiasi kwamba hawataki hata kukuona upo karibu nao?..Jifunze kwa Bwana Yesu hapo juu…Na likumbuke hili neno : Njia za mtu zikimpendeza Bwana hata adui zake hupatanishwa naye!…
Tafuta kupatanishwa na maadui zako na si kugombanishwa nao. Kwasababu hiyo ndio Nia ya Kristo kwetu.
Epuka injili iliyotoka kuzimu ambayo inakuhubiria kuwa maadui zako ni wanadamu wenzako, na hivyo tunapaswa kuwapiga na kuwashushia moto, hiyo ni roho ya adui shetani. Hata kama Daudi aliwapiga maadui zake na kuwaombea mabaya, Bwana YESU Mkuu wa Uzima anatuambia, ”MIMI NAWAAMBIA WAPENDENI ADUI ZENU WAOMBEENI WANAOWAUDHI” Daudi alifanya hivyo kwasababu hakujua kweli yote, na zaidi ya yote Agano la Kale ni kivuli cha cha Agano letu jipya. Amri kuu tuliyopewa ni upendo kwa Mungu wetu na majirani zetu. Ikiwa unaona hili Neno ni gumu kwako na huwezi kupokea, kama umeokoka..msihi Bwana akujaze Roho wake Mtakatifu yeye atakutia katika kweli yote.
Na Kama hujampa Yesu Kristo Maisha yako. Mlango upo wazi ila hautakuwa hivyo siku zote. Wakati dunia inafurahia anasa…Ujio wa Kristo unazidi kukaribia kila sekunde inayosogea, ujio wake upo karibu kunashinda tunavyofikiri. Watu wa ulimwengu wataomboleza siku ile watakapokuja kugundua kwamba walikuwa wanapoteza muda kujifurahisha na anasa za ulimwengu. Bwana atusaidie tusiwe mimi na wewe. Hivyo Tubu kama hujatubu, na pia tafuta ubatizo kama hujabatizwa, na Upokee Roho Mtakatifu. Kwa hatua hizo tatu utakuwa umekamilisha wokovu wako.
Maran atha!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.