Tusome..
1Wakorintho 12:3 “Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu.”
Kikawaida kila mtu anaweza kusema “Yesu ni Bwana”, hata walevi, waasherati,wauaji,wachawi, n.k, kwa ujumla mtu yoyote anaweza kusema “Yesu ni Bwana” pasipo kujalisha hali yake, tofauti iliyopo katika kutamka hilo neno kuwa “Yesu ni Bwana” ni ufunuo ambao mtu aliyempokea Bwana Yesu na kujazwa Roho Mtakatifu anakua nao kuhusu Yesu ni nani!.
Kwahiyo biblia inaposema hawezi mtu kusema Yesu ni Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu, maana yake mtu ambaye hajampokea Roho Mtakatifu hana ufunuo wa Yesu kuwa ni nani, na alikuja duniani kufanya nini, na sasa yuko wapi, anaweza tu akaishia kutamka kwa kinywa chake kuwa Yesu ni Bwana ila asiwe amemaanisha, au ameujua uzito wa hilo jina, akawa amelitaja tu kama majina mengine ya kawaida, Lakini kwa mtu ambaye amejazwa Roho Mtakatifu, na kufunuliwa kwa Roho kuwa Yesu ni nani, kwanini amekuja duniani, kwanini amwage damu yake, afe na kufufuka, na yupo wapi sasahivi?..Mtu wa namna hiyo kama akitamka “Yesu ni Bwana”,… kutamka kwake kunakuwa na maana sana na nguvu kubwa. Kwasababu ametamka katika Roho.
Hivyo Mtu anayetaja “Yesu ni Bwana” katika Roho Mtakatifu ni lazima atakuwa ni mtakatifu, kwasababu amemjua Mungu, kadhalika atakuwa anamheshimu Mungu na kumwogopa, kutokana na ufunuo mzito alioupata kumhusu Yeye (Yesu).
Lakini kwa yule anayetamka tu “Yesu ni Bwana” pasipo kuwa na Roho, hawezi kuwa na ufahamu/ufunuo wowote kumhusu Yesu, wala hana mpango na maneno yake, mtu wa namna hiyo kutamka kwake kuwa Yesu ni Bwana haimpi manufaa yoyote, ndio maana hapo Maandiko yanasema.. “mtu hawezi kusema Yesu ni Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu”..maana yake atakuwa anasema tu kinywani, na si kwa kuelewa na kumaanisha.
Ndio maana Bwana Yesu alisema maneno haya…
Mathayo 7:21 “SI KILA MTU ANIAMBIAYE, BWANA, BWANA, ATAKAYEINGIA KATIKA UFALME WA MBINGUNI; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”
Umeona?.. Kusema tu “Yesu ni Bwana” bila ya kuwa na badiliko halisi la ndani, ambalo hilo linaletwa na Roho Mtakatifu mwenyewe, haisaidii kitu,ni kazi bure!.. na pia huwezi kuwa na Roho Mtakatifu halafu useme Bwana Yesu kalaaniwa.. hilo haliwezekani.
Hivyo ili tuweze kuyafanya mapenzi ya Mungu, na maneno ya vinywa vyetu pamoja na maombi yetu zikubalike mbele za Bwana, Ni lazima tuzaliwe mara ya pili, na kuzaliwa mara ya pili kunakuja kwa kudhamiria kutubu dhambi, kwa kumaanisha kuziacha kabisa kwa vitendo, na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa JINA LA YESU pamoja na kupokea Roho Mtakatifu.(Matendo 2:38)
Tukishatimiza hiyo kanuni,(kuzaliwa mara ya pili) basi lolote tunalolitamka la kumwadhimisha Mungu, kumsifu, kumwomba, na kumkiri linakuwa katika Roho, na hivyo linaleta matokeo makubwa sana. Lakini kama hatutatubu kwa kumaanisha kuacha dhambi, hata sala zetu na maombi yetu yanakuwa ni bure, hata sifa zetu kwake zinakuwa ni bure…
2Timotheo 2: 19 “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu”
“BWANA YESU ANARUDI”
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.