TUONDOKEE HATUTAKI KUZIJUA NJIA ZAKO 

Uncategorized No Comments

TUONDOKEE HATUTAKI KUZIJUA NJIA ZAKO 

Ayubu 21:14 “Walakini walimwambia Mungu. Tuondokee; Kwani hatutaki kuzijua njia zako.

15 Huyo Mwenyezi ni nani, hata tumtumikie? Nasi tutafaidiwa nini tukimwomba?

Hayo ndio maneno ya watu wengi waliofanikiwa katika mambo ya duniani, wakamsahau Mungu aliyewaumba. Lakini biblia inasema..

Ayubu 21:16 “Tazama, kufanikiwa kwao hakumo mkononi mwao;..”

Tena anasema..

Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza.”(Mithali1:32)

Katika biblia wapumbavu ni watu wote wasiomcha Mungu wala hawataki kumtafuta huyo Mungu wa kweli, mungu wao ni tumbo na mali.

Wakiletewa habari njema za ufalme wa Mungu, habari za wokovu wa roho zao, Kwasababu ya kiburi chao wanasema “Tuondokee hatutaki kuzijua habari hizo” kwani huyo Mungu ni nani hata tumuogope? Kwani tumepungukiwa nini hata tumsikilize?. Ndio maneno ya wapumbavu. Wanaweza wasiseme hayo kwa vinywa vyao lakini mioyo yao inasema. Na huku kwa unafiki wanaingia huko katika hayo wanayoyaita makanisa na kusema tumeokoka.

Ndio hao ambao Ezekieli aliambiwa awe nao makini maana wanajionyesha kwa nje kuwa wema lakini ndani ya mioyo yao kumejaa unafiki, wamemkataa Mungu.

Ezekieli 33:30 “Nawe, mwanadamu, wana wa watu wako husimulia habari zako karibu na kuta, na ndani ya milango ya nyumba zao, na kuambiana, kila mtu na ndugu yake, wakisema, Haya! Twende tukasikie ni neno gani hilo litokalo kwa BWANA.

[31]Nao huja kwako kama watu wajavyo, nao hukaa mbele yako kama watu wangu, nao husikia maneno yako, wasiyatende; maana kwa vinywa vyao hujifanya kuwa wenye upendo mwingi, LAKINI MIOYO YAO INATAFUTA FAIDA YAO.

[32]Na tazama, wewe umekuwa kwao kama wimbo mzuri sana, wa mtu mwenye sauti ipendezayo, awezaye kupiga kinanda vizuri; maana, WASIKIA MANENO YAKO, LAKINI HAWAYATENDI.”

Tuondokee hatutaki kuzijua njia zako! Ndivyo wanavyosema katika mioyo yao.

Hawataki kusikia injili ya toba na utakatifu, wanataka kuhubiriwa tu mafanikio. Kisha waendelee kuishi na dhambi.

Kipindi fulani Bwana Yesu alipoenda kuhubiri injili sehemu fulani, wale watu walipoona kuwa mtu mmoja amefunguliwa katika vifungo vya giza, badala wamkaribishe Bwana ili awafungue, lakini walimsihi aondoke kwao. Hawakutaka kumjua Bwana Yesu kwa kina, waliona huyu amekuja kutufanya tuwe maskini.

Mathayo 8:28 “Naye alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile.

[29]Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?

[30]Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakilisha.

[31]Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe.

[32]Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini.

[33]Lakini wachungaji walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote na habari za wale wenye pepo pia.

[34]Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; NAO WALIPOMWONA, WALIMSIHI AONDOKE MIPAKANI MWAO”.

Hata leo, watu wengi wanamkataa Yesu ndani ya mioyo yao, utaona Bwana anawapeleka watumishi wake katika nyumba fulani au mji Fulani, lakini mtu yule/ watu wale wakisikia tu kuwa wameletewa habari za kutubu dhambi na kuokoka. Wanaanza kukataa wazi wazi ndani ya mioyo yao, kwa nje unaweza kuona kuwa wanakusikiliza lakini ndani wanasema ”Tuondokee hatutaki kuzijua njia hizo”.

Hebu na wewe leo jitathimini, huwenda Bwana amekujia mara nyingi na kukuambia hiyo njia unayopita inakupeleka jehanamu lakini kwasababu pengine una mali nyingi, una mafanikio Fulani ukakataa kumsikiliza Mungu.

Pengine ulipita mahali fulani au ulisoma ujumbe unaokuhusu, ukasikia kuwa mwanamke kuvaa mavazi yasiyopasa jinsia yake kama suruali ni machukizo kwa Mungu, kuvaa mavazi ya kubana, kuvaa vimini ni dhambi lakini kwasababu ya kiburi ukadharau huo ujumbe, ukasema moyoni mwako kwani huyo Mwenyezi ni nani? Itanifaidia nini nikimsikiliza?.

Lakini leo, Bwana anakusihii tena usikie sauti yake, kwani itakufaidia nini huo utajiri na uzuri wako ukiwa nayo, wanadamu wakakusifia lakini mwisho utaishia kwenda kutupwa jehanumu.

Marko 8:36 “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?

Leo hii umebadilisha maumbile Mungu aliyokuumbia nayo, umejitafutia nywele bandia, kucha bandia, rangi bandia, umekataa kope, kucha, ngozi Mungu aliyokuumbia. Na Mungu amekuonya mara nyingi lakini kwasababu ya Elimu yako hutaki kusikia, kwasababu ya fedha, cheo ulichonacho hutaki kusikia maonyo ya Mungu. Lakini Neno la Mungu halibadiliki milele, alishasema watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wake. (Wagalatia 5:19-21).

Haijalishi umefanikiwa kiasi gani, kama hutosikia sauti ya Mungu na kutubu/kubadilika na kuacha maovu yako, kuacha ulimwengu, kuacha matendo yote ya giza, rushwa, uchawi, wizi, uzinzi, ulevi, mavazi ya kiulimwengu na kikahaba, mapambo ya kiulimwengu n.k fahamu kuwa sehemu yako itakuwa ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti biblia inasema hivyo (Ufunuo21:8).

Hivyo ni heri leo uamue kutii sauti ya Mungu na kumaanisha kutubu kabisa na kuacha dhambi zote kisha ukabatizwe kwa maji mengi na Kwa jina la Bwana Yesu ili upokee muhuri wa Mungu (Roho Mtakatifu) atakayekusaidia kuishi mapenzi ya Mungu. (Utakutatifu).

Kumbuka tunaishi ukingoni mwa nyakati, Yesu anakuja muda wowote na anakuja kuwanyakua watakatifu.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *