Uchambuzi wa warumi 13:14 ” WALA MSIUANGALIE MWILI HATA KUWASHA TAMAA ZAKE” 

Maswali ya Biblia No Comments

Jina la bwana Yesu Kristo libarikiwe. Karibu Tuyatafakari Maandiko 

Warumi 13:14

Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata KUWASHA TAMAA ZAKE.”

Kuuangalia mwili kama ilivyoandikwa japo juu inamaanisha kuujali au kuutii sana mwili kupitiliza, Naam hatimae kuziwasha tamaa zake.

Mtu anapofikia hatua hii kuwa ni teja wa mwili wake na huutii kwa kila jambo Lasivyo mtu huyo hupitia wakati mgumu na wa shida sana.

Kwanza yatupasa kujua kwamba tamaa za mwili hazikutoka kwa shetani, La! Bali ni zawadi kutoka kwa Mungu ili sisi tuzitawale na si zenyewe kututawala sisi

Leo tutaziangalia tamaa tatu{3} za mwili na jinsi ya kudhibiti kwa mwamini, zipo nyingi sana Lakini Leo tutaziangazia hizi

Kwa ufupi sana

 1. USINGIZI

Mwili huhitaji kupumzika, Mungu mwenyewe aliweka usingizi katika miili yetu, na ndio Maana kuna muda usingizi huja wenyewe bila mtu kuukaribisha. Lakini ni hasara kubwa kulala Kila muda maana SI Kila muda ni WA kulala

Soma…

 Mithali 20:13

” Usipende usingizi usije ukawa maskini; Fumbua macho yako nawe utashiba chakula.”

Angalia, Usingizi unapoendekezwa huzuia mtu kuwahi kazini, shuleni, maombi ya Usiku hata na mengine mengi ya faida.

Lakini si tamaa isiyoweza kuzuiliwa! Wapo wengi wameishinda kwa namna mbalimbali. Mfano mtu aliyeweka ratiba ya kuamka Kila sa11 alfajiri kuwahi shuleni au kazini, ifikapo muda huo tu usingizi wake huisha mara! Sababu ni utaratibu ulio kichwani kwake.

Hivyo tunaona hata ingalikuwa sa nane au tisa za usiku ingalikuwa vivo hivyo.

Cha kusikitisha ni kwamba kuna wengine wameshindwa! Na inakuwa ni mitihani mzito sana kwao, lakini tukirudi nyuma wale walioweza hawakuwa na nguvu yoyote ya ziada ni utayari tu, ndipo tunagundua yule anayeshindwa kuumiliki basi Ameuendekeza ndio Maana unamshinda. Lakini yule mwingine kaweza kwasababu amefanikiwa kuudhibiti, japo kwa shida mwanzoni, lakini pole pole alijaribu mpaka akaweza.

2. CHAKULA

Mungu alimuumba Kila mmoja ahisi njaa na kiu. Hivyo kuna nyakati tu utasikia kuburudisha koo lako kwa kinywaji au kuweka chochote tumboni

Lakini tunapokosa kiasi katika hayo huleta uraibu, unakuta mtu Kila mda anataka kunywa au kula tu{ulafi} mwishowe ni uzito kupindukia, Ulevi, kuvimbiwa na hata magonjwa.

Tukichukulia mfano Ulevi, je mtu alikuwaje mlevi? Ni kwa kuitii kupitiliza kiu ya mwili wake na kusahau madhara yaletwayo na Ulevi. Vivo hivyo na uvutaji sigara, madawa ya kulevya UTII kwa miili yao kupitiliza na kupelekea wawe mateja wa hayo.

Rejea..

Mithali 23:20-21

20 “Usiwe miongoni mwao wanywao mvinyo; Miongoni mwao walao nyama kwa pupa.

21 Kwa maana mlevi na mlafi huingia umaskini, Na utepetevu humvika mtu nguo mbovu.”

Wanaofanikiwa kuacha pombe, hawafanikiwi kwa kukosa kiu ya pombe Bali kwa kujua namna ya kudhibiti kiu ya miili yao katika Hilo, mwishowe mwili unazoea na wanapooza kiu yao kwa soda au vinywaji vya kawaida. Vivo hivyo kwa waraibu wa madawa ya kulevya na sigara. 

3. ZINAA

Tamaa hii Haina tofauti na zile zilizopita (chakula na usingizi) isipokuwa watu huiendekeza kwa matakwa yao wenyewe. Mungu kaiweka tamaa hii kwa wanadamu lakini ili itumike kwa wakati maalum na kiasi.

Mungu aliihalalisha kwa wanandoa tu, lakini pale inapochochewa kabla ya wakati wake hapo ndipo madhara yake kimwili na kiroho huanzia. _JE! Utakuwa SI unafiki kudhibiti chakula na usingizi na Kushindwa kudhibiti zinaa?

JIBU ni ndio utakuwa ni unafiki maana zinaa inadhibitika kiurahisi kabisa mtu akiamua kujizoesha kuiacha. Na usipofanya hivyo utaishia kuwa mzinzi Kila siku, mtazamaji wa pornography, mraibu wa masturbation n.k

 Wimbo Ulio Bora 3:5

” Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.”

SWALI ni JE utaacha kwa namna Gani?

Kwa kuepuka mazungumzo, kampani au vichochezi vyovyote vya kizinzi vilivyo karibu nawe.

Soma…

 Waefeso 5:3

” Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;”

Vilevile kwa kufuta movies na tamthiliya zenye maudhui ya kimapenzi katika simu yako na kuepuka kuviperuzi hata mtandaoni maana Maandiko yanasema..

 Mithali 26:20

“Moto hufa kwa kukosa kuni;…”

Epuka kuchat chat na jinsia tofauti mambo yasiyokuwa na msingi maana ndio mlango mkubwa shetani huutumia kuamsha ajenda hizo na kuwanasa wengi katika Hilo.

Utapozingatia hayo machache tamaa hizo zitazima na utazishinda kwa namna ya kushangaza sana, Utakaa navyo mbali pasi na ugumu wowote ule.

Jambo hili si kwa ambao hawapo katika ndoa tu, La! Bali hata walio katika ndoa wanaaswa kuwa na kiasi. Wanandoa wanapokosa kiasi shetani hutumia mlango huo kuingiza mambo yasiyompendeza Mungu mfano kutoka nje ya ndoa, ngono kinyume na maumbile n.k

 1 Wakorintho 7:5

“Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.”

Ningependa kuhitimisha kwa kusema imetupasa sote tuishi maisha ya kuto ufuatisha mwili na tamaa zake. Huo utakuwa ni ushindi dhidi ya mengi sana. Maana adui wa pili baada ya shetani ni MIILI YETU, na imetupasa kuishi kama watu wa Rohoni na si mwilini. Tutashinda yote kwa yote kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo

Amen

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *