Kati ya jambo muhimu ambalo unapaswa kulifahamu kwa undani zaidi ni kuhusu Roho Mtakatifu. Kwasababu Roho Mtakatifu ndio ukamilifu wa sauti ya Mungu kwetu..
Leo kwa neema za Mungu tutaenda kutazama kazi kuu tatu za Roho Mtakatifu katika huu ulimwengu, lakini awali ya yote kabla ya kwenda kuzitazama hizo kazi hebu tuweke msingi kidogo wa kuufahamu utendaji kazi wa Mungu, katika ofisi zake tatu.
Katika nyakati za agano la kale, Mungu alinena na watu kutoka mbinguni kupitia vinywa vya watumishi wake(Manabii), ila tukija katika agano jipya Mungu alizungumza nasi kupitia mwanaye wa pekee Yesu Kristo (Waebrania1:2), na Baada ya hapo Mungu hakuishia tu kuzungumza nasi kupitia ule mwili wa Bwana Yesu, ila alizidi kutusogelea zaidi kupitia Roho Mtakatifu, Ni sawa na kusema.. Mungu alizungumza nasi akiwa juu yetu(Kama Baba), kisha akashuka na kazungumza pamoja nasi katika mwili wa kibinadamu (Imanueli) na mwisho Mungu sasa anazungumza ndani yetu kama(Roho Mtakatifu)
Na kiufupi hatua hii ya mwisho ndio hatua timilifu kabisa kuliko nyingine kwasababu ndio sauti ya Mungu mwenyewe iliyo karibu na sisi zaidi ya ile iliyokuwa juu Yetu yaani (baba)
Ni mfano wa mtu azungumze na wewe kwa sauti kuu akiwa juu kabisa kwenye ghorofa au juu ya mti mrefu kiasi kwamba humuoni ila unachoweza kusikia ni sauti yake tu na wewe upo chini ya hilo ghorofa au huo mti, ni wazi kuna maneno hautayasikia vizuri kwasababu yupo mbali, hivyo maneno mengine unaweza kuyaelewa kinyume na alivyosema..
Lakini huyo mtu akitoka huko aliko na kushuka chini ukamwona, akawa kama mita 6 kutoka mahali ulipo, akiongea na wewe ni rahisi kumsikia vizuri kuliko alivyokuwa kule juu, ambapo ulikuwa unasikia sauti tu na sasa unamsikia na kumwona, lakini pia bila shaka wakati anazungumza kuna maneno unaweza usiyasikie vizuri, hata wewe unapozungumza na mtu aliye mbali na wewe ni lazima utapitia vipindi vichache vichache vya kuomba arudie alichosema…
Lakini hebu tafakari tena endapo huyo huyo mtu akikukaribia sana kiasi kwamba mdomo wake unafika katika sikio lako, bila shaka hapo utakuwa unamsikia vizuri zaidi kuliko alivyokuwa mita sita mbele yako..hapo huwezi kumwambia arudie rudie yale anayoyasema.. Hivyo utamsikia vizuri kuliko kawaida, na utamwelewa, kwasababu amesogea karibu sana na wewe.
Sasa kwa mfano huo ndivyo hivyo na utendaji kazi wa Mungu ilivyo, Roho Mtakatifu ni sauti ya Mungu iliyo karibu sana na sisi, haijaishia kusikika masikioni tu, bali inasikika hadi mioyoni mwetu. Ni sauti isiyo na chenga chenga. Sauti ya Bwana Yesu ilikuwa ni kamilifu, lakini ilikuwa na chenga chenga kwetu, hatukuweza kumwelewa vizuri kwasababu alikuwa anazungumza nje ya miili yetu. Ndio maana ilimpasa Bwana aondoke ili Yule Roho aje juu yetu.
Yohana 16:7 “ Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu”.
Umeona hapo? Bwana hana budi kuondoka ili Roho Mtakatifu aje…(Na kumbuka Roho Mtakatifu ndiye Yule Yule Bwana Yesu mwenyewe, isipokuwa anakuja katika roho (soma 2Wakorintho 3:17),
Sasa baada ya kuweka huo msingi na kuelewa kwa ufupi kuhusu utendaji kazi wa Mungu katika ofisi tatu, sasa tukazitazame kazi kuu tatu za Roho Mtakatifu kwa ulimwengu.
1) Kazi ya kwanza ni kuuhakikisha ulimwengu kwa habari ya DHAMBI 2) Atauhakikisha kwa habari ya HAKI 3) Atauhakikisha kwa habari ya HUKUMU.
Hizo ndizo kazi kuu tatu za Roho Mtakatifu kwa Ulimwengu, tutaziangalia moja baada ya nyingine.
Kwa habari ya dhambi:
Yohana 16:8 “Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.
9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi”
Kuhakikisha maana yake ni “kuweka sawa jambo”. Kitu ambacho hakikukaa vizuri sasa kimewekwa vizuri maana yake kitu hicho“kimehakikiwa”. Kadhalika Hapo Bwana Yesu anasema huyo Roho atakapokuja atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, maana yake hapo kwanza yeye alizungumza kuhusu dhambi lakini hakueleweka vizuri, lakini atakapokuja huyo Roho ataizungumzia vizuri dhambi kwa sauti ya ukaribu zaidi, na atafanya wengi kuelewa dhambi ni nini, kuliko jinsi wangemwelewa Bwana.
Ndio sababu Bwana Yesu anasema hapo “kwa habari ya dhambi, KWA SABABU HAWANIAMINI MIMI” … maana yake yeye (Bwana Yesu) aliihubiri sana kuhusu dhambi, lakini watu hawakumwamini. Kwahiyo sasa Roho Mtakatifu atakuja kuielezea vizuri na wengi wataamini. Na elewa dhambi ni “kutomwamini Mwana wa Mungu, kwamba yeye ndiye mkombozi wa ulimwengu”. Hiyo ndiyo dhambi….hayo mengine kama ulevi, uzinzi, uuaji, ubakaji, uasherati, usengenyaji, uongo, wizi, n.k, ni matokeo ya dhambi, Kwahiyo Bwana Yesu alihubiri sana kwamba
“Kila amwaminiye atapata uzima wa milele lakini yule asiyemwamini atahukumiwa( atakuwa na dhambi) lakini pamoja na Bwana Yesu kuyahubiri hayo sana kwa muda wa miaka mitatu na nusu, watu hakumwelewa..ni wachache tu ndio waliomwamini, ndio maana injili haikufika duniani kote kipindi Bwana Yesu yupo duniani, ni wachache tu walisikia sauti yake na kumwamini, wengine walikuwa hawamwelewi.
Ila tunakuja kuona baada ya Bwana Yesu kuondoka duniani na Roho Mtakatifu kushuka katika ile siku ya Pentekoste, tunaona Petro alivyosimama na kuhubiri habari ya dhambi..watu wengi zaidi ya elfu 3 walibatizwa kwa siku moja baada ya kusikia hayo mahubiri aliyohubiriwa na Roho Mtakatifu kupitia kinywa cha Petro Mtume na wakakubali kumwamini Bwana Yesu na kutubu..soma (Matendo 2:41)
hapo ukirudi kipindi cha nyuma tu kama miezi miwili Bwana Yesu alikuwa anahubiri hayo hayo maneno ya Petro ila hakueleweka.. mwisho wa siku wale waliokuwa wakimsikiliza ndio waliokuja kumsulubisha kwasababu hawakumwelewa.
Yohana 12:37 “Walakini ajapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini;
38 ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani.”
Lakini miezi miwili tu kama tunavyosoma katika kitabu cha Matendo 2, Roho Mtakatifu alipozungumza kwa kinywa cha Petro, wale ambao hawakumwamini Bwana Yesu kule Yerusalemu, walianza kumwamini kwa kasi sana.
Kwa habari ya HAKI
Yohana 16:10 “Kwa habari ya haki, kwasababu mimi, naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena”
Katika jambo ambalo Bwana Yesu hakuligusia kabisa wakati akiwa hapa duniani, ni kuhusu HAKI, Na haki inayozungumziwa hapo, ni haki ipatikanayo kwa njia ya IMANI, hiki kipengele Bwana hakuigusia kabisa, na sababu ya kutoielezea ni kwasababu ya ugumu wa mioyo ya watu, ndio maana aliwaambia “yapo mambo ya kuwaambia lakini kwa wakati huo wasingeqeza kustahimili, mpaka huyo Roho atakapokuja.”
Yohana 16:12 “Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, LAKINI HAMWEZI KUYASTAHIMILI HIVI SASA.
13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye Kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.”
Umeona hapo..jambo mojawapo ambalo wasingeweza kustahimili endapo wangeambiwa ni hilo la “HAKI” ni wazi Bwana angewafunulia siri Mitume kwamba, sisi watu wa mataifa nasi ni warithi wa ahadi za Mungu, kwamba kwa NEEMA tunahesabiwa HAKI kwa kumwamini Yesu, kwamba na sisi ni warithi wa ahadi za Mungu, ni dhahiri kuwa wangerudi nyuma. wangesema Bwana Yesu hayupo sawa, inakuwaje yule aliyemwita yule mwanamke wa kimataifa “Mbwa” halafu leo tena anamwita mrithi, Yule ambaye aliwatuma na kuwaambia “msifike miji ya mataifa kuhubiri (Mathayo 10:5)” mara anageuka na kuwaita tena hao mataifa ni warithi!…yule aliyesema “sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli (Mathayo 15:24).” Leo hii ageuke na kututuma sisi huko kwao kuhubiri??..hakika Bwana amechanganyikiwa.
Kwahiyo Bwana aliliona hilo na kuliacha pamoja na mengine mengi ili yaje kufunuliwa na Roho Mtakatifu baada ya yeye kuondoka, kwasababu ni wazi kwa uchanga waliokuwa nao mitume, wangeambiwa hizo siri wangemwacha Bwana na kurudi nyuma (wasingestahimili kupokea kwa wakati huo)
Na siku yenyewe ilipofika ya kuifunua hiyo siri ya HAKI YA MUNGU, Roho Mtakatifu alimfunulia kwanza Petro, katika yale maono ambayo Mtume Petro aliyaona akiwa kule Kornelio, na baadaye alikuja kumfunulia tena Mtume Paulo.
Hebu fuatilia hiki kisa kwa umakini…
Matendo 11:1 “Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu.
2 Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye,
3 wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao.
4 Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema,
5 Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikilia.
6 Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani.
7 Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule.
8 Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu.
9 Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi.
10 Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni.
11 Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria.
12 Roho akaniambia nifuatane nao, nisione, tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule;
13 akatuelezea jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro,
14 atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote.
15 Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo.
16 Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.
17 BASI IKIWA MWENYEZI MUNGU AMEWAPA WAO KARAMA ILE ILE ALIYOTUPA SISI TULIOMWAMINI BWANA YESU KRISTO, MIMI NI NANI NIWEZE KUMPINGA MUNGU?”
Umeona hapo? Kornelio ambaye ni mtu wa mataifa anapokea Roho Mtakatifu baada ya kuamini. tena yule yule Roho ambao nao walio wa Israeli walipokea..ni wazi Petro alielewa ni kwanini Bwana Yesu
hawakuwambia hiyo siri kipindi yupo nao duniani, ingekuwaje ni ngumu wao kumeza!. Maana unaona hapo juu tu kama tulivyosoma, mitume wengine walipopata habari kwamba Petro aliingia kwa watu wa mataifa, walishanda naye vikali.. mpaka Petro alipowaelezea kwa utaratibu.
Hiyo ndiyo siri ya Mungu ambayo ilistirika tangu zamani, kwamba sisi watu wa MATAIFA, ni warithi wa ahadi za Mungu, kwamba tunahesabiwa HAKI YA KUURITHI UZIMA WA MILELE bure kwa njia ya IMANI YA KUMWAMINI YESU, mitume hapo mwanzo walijua wokovu ni kwa ajili yao tu!. (Waisraeli) kumbe hata watu wa mataifa nao wana hiyo haki ya kuurithi uzima wa milele kwa kumwamini Yesu Kristo,
Mitume Paulo naye alifunuliwa siri hii na akaelezea katika.. Wakolosai 1:26-27, na katika Waefeso 3:6 soma uone.
Ndio maana Bwana Yesu akasema…”kwa habari ya haki, kwasababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena”… maana yake alipaswa aelezee hiyo Haki, lakini anaondoka kwenda kwa Baba, na wala hawatamwona tena, na hataielezea hiyo siri, lakini Roho atakuja kuliweka hilo sawa!. Maana yake atalifunulia kanisa. Haleluya;
Kwa habari ya HUKUMU.
Yohana 16:11 “Kwa habari ya hukumu, kwasababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.”
Shetani ndiye mkuu wa ulimwengu huu(ndiye anayezungumziwa hapo) Na Bwana Yesu anasema… Mfalme wa ulimwengu amekwishahukumiwa…sasa hukumu inayozungumziwa hapo si ile ya ziwa la moto(ni kweli hiyo ilishapitishwa muda sana) lakini hukumu inayozungumziwa hapa si hiyo, bali ni hukumu ya kunywang’anywa mamlaka ya ulimwengu!! Na kwamba mamlaka yote ya duniani amekabidhiwa Bwana Yesu..yeye sasa ndiye anamiliki mamlaka yote ya duniani na mbinguni, ndiye MFALME wa WAFALME, Haleluya!.
Na shetani aliyapoteza hayo mamlaka.. kipindi Bwana Yesu akiwa duniani!.. wakati alipotoa uhai wake kwa ajili ya wengi, akakabidhiwa mamlaka yote ya duniani na mbinguni.
Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI.”
Sasa atakapokuja Roho Mtakatifu, ataliweka hilo sawa katika mioyo ya watu wengi, watu wataelewa kwa undani zaidi ni kwa jinsi gani sasa hivi YESU NDIYE ANAYETAWALA MBINGUNI NA DUNIANI, NA HAKUNA MFALME MWINGINE KAMA YEYE. Mitume hawakumwelewa Bwana Yesu vizuri kile kipindi walipokuanao hapa duniani, walikija kumwelewa vizuri baada ya kuondoka kwake!.. Kwamba alikuwa ni nani?
Yule Yohana ambaye alikuwa anaegemea kifuani pa Yesu, ambaye alikuwa anamwona Bwana Yesu kama kaka yake tu!(Yohana 13:23).. Huyo huyo anakuja kumwona Bwana Yesu Katika kisiwa cha Patmo kama miale ya moto, na anaanguka chini ya miguni yake kama mtu aliyekufa(soma Ufunuo 1). Roho Mtakatifu anamfunulia Yule Yule Yesu kama Mfalme wa Wafalme, ambaye enzi na mamlaka yote ni zake.
Waefeso 1:20 “aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho;
21 juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;
22 AKAVITIA VITU VYOTE CHINI YA MIGUU YAKE, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo
23 ndio mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”
Hivyo Roho Mtakatifu alipokuja aliweka wazi kwa ulimwengu kuwa YULE mkuu wa ulimwengu.. shetani, hana kitu, mbele za Bwana, kashanyang’anywa mamlaka yote.(kashashindwa)
Yohana 14:30 “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.”
Shetani hana mamlaka yoyote juu ya wote waliomwamini Bwana Yesu..kashahukumiwa na kunyang’anywa mamlaka ya duniani na kuzimu..wafu wote sasa wanamilikiwa na Bwana Yesu (Warumi 14:9) shetani sasa hana tena uwezo wa kushuka kuzimu na kuwapandisha wafu kama alivyofanya kwa Samweli (1Samweli 28:7-15) hilo jambo haliwezekani tena, kwasababu mkuu wa ulimwengu kashahukumiwa (kashanyang’anywa hayo mamlaka) anayewamiliki wafu wote kwasasa ni Mkuu wa Uzima, Bwana YESU!. Huyo peke yake ndiye mwenye mamlaka ya kuileta roho ya mtu juu na kuishusha chini, yeye peke yake ndiye mwenye mamlaka na uwezo wa kufufua au kuua!.
Hivyo kwa kazi hizo tatu, alizozitaja Bwana Yesu, ndizo zinazokamilisha ushuhuda kamili wa Roho Mtakatifu kwa ulimwengu!!!.
Na Roho huyo ndiye anayeshuhudia hata sasa kupitia kwa watakatifu wote waliojazwa Roho Mtakatifu, kwamba Yesu Kristo ni njia ya kweli, na uzima, na hakuna njia nyingine ya kufika mbinguni isipokuwa kupitia yeye, Na Bwana Yesu anawapokea watu wote wa mataifa yote na kabila zote na anawahesabia Haki ya kupata uzima wa milele bure iwapo watamjia, vilevile Bwana YESU ndiye mmiliki wa mbingu na nchi, na shetani hana kitu mbele zake. Hivyo Yesu ndiye tumaini pekee la kulikimbilia na kulitegemea.
Je umezitii ushuhuda hizo za Roho Mtakatifu?? Kwa kumpokea Yesu maishani mwako na kutubu dhambi zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa???.. kumbuka Bwana Yesu anawapokea watu wote bila kujalisha kabila wala taifa fulani,
Kama bado hujamwanini na kumpokea Bwana Yesu.. basi fahamu kuwa umeukataa ushuhuda wa Roho Mtakatifu maishani mwako..na hivyo utakuwa na HATIA kubwa, kwasababu Roho Mtakatifu amezungumza na wewe kwa sauti ya kueleweka kabisa.. Hivyo umekusudia kuukataa ushuhuda huu ulio mkamilifu kabisa.
Hivyo ndugu mpokee leo Yesu maishani mwako, ukubali ushuhuda wa Roho Mtakatifu, ili ufanikiwe katika roho yako, maandiko yanasema Roho Mtakatifu anatutamani kiasi cha kutuonea wivu(Yakobo 4:5) anatamani aingie ndani yako kuliko wewe unavyotamani aingie,. hivyo unachopaswa tu kufanya ni wewe kutii!!. Kwa kutubu dhambi zako na kwenda kubatizwa ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa JINA LA BWANA YESU sawa na Maandiko (Yohana 3:23 & Matendo 2:38)
Na baada ya kutii kwako.. kutubu na kubatizwa kwa usahii..Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukutia muhuri wake..na baada ya hapo atakuongoza na kukutia katika Kweli yote!.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.