Elewa maana ya dhambi isiyo na msamaha,

Maswali ya Biblia No Comments

Kuna dhambi ambayo huleta mauti, mkristo akiifanya dhambi hiyo wakati ambao bado ana neema ya Mungu atakufa lakini siku ya mwisho atapata wokovu. Mfano Musa alipomkosea Mungu alisamehewa lakini hakuondolewa adhabu ya kifo…Mungu alimwambia kutokana na lile kosa hataiona nchi ya ahadi na hakika atakufa lakini alipokufa aliungana na watakatifu na kuna wakati alitokea na kuzungumza na Bwana Yesu yeye pamoja na Eliya katika ule mlima mrefu. (Mathayo 17:1-9)


Hii ni dhambi inayopelekea mauti, yaani unaadhibiwa mwili kwa ajili ya kuokoa roho yako (1 Wakorintho 5:5)

Lakini kuna dhambi ambayo haina msamaha kabisa nayo ni kumkufuru Roho Mtakatifu. Mtu asipoijua ni rahisi sana shetani akamtumikisha mtu huyo kwa sababu shetani anamjua mwanadamu tangu mwanzo wa ulimwengu pale bustani ya Edeni hivyo kati ya njia anazotumia kumpotosha mwanadamu ni kumletea mawazo mabaya afikirie kuwa ana dhambi ambayo hawezi kusamehewa na Mungu.

Leo tunajifunza ni kwa namna gani mtu ana mkufuru Roho Mtakatifu..

Mathayo 12:31 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa.

32 Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao”


Hapa neno linatuonyesha bayana kuwa mtu atayenena neno lolote juu ya roho Mtakatifu hawezi kusamehewa lakini juu ya mwana wa Adamu atasamehewa hii haimaanishi Mungu amegawanyika hapana Mungu wetu ni mmoja ametupa Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani yetu katika ulimwengu wa kiroho. Roho Mtakatifu ndiye Roho wa Yesu mwenyewe, kwa sababu yeye aliondoka katika umbo la mwili ili arudi kwetu katika mfumo wa roho (Yohana 16:16), maana yule atendaye kazi katika roho huleta faida kubwa kuliko yule atendaye katika mwili, ..

Mfano mchawi anayeenda sehemu katika ulimwengu wa kiroho anaweza kuleta madhara makubwa ukilinganisha na kama angeenda katika hali ya kimwili. Hivyo Roho Mtakatifu anafanya kazi kubwa zaidi yenye matokeo makubwa kuliko Mungu alivyokuwa katika ulimwengu wa mwili, ili kumvuta mtu kwa Mungu na akubali inahitajika nguvu ya Roho Mtakatifu kwa hivyo ni hatari sana kumkufuru.

Ikiwa mtu hajampokea Kristo katika maisha yake na ndani ya moyo wake kuna sauti inamuambia habari za wokovu basi huyo ni Roho Mtakatifu anamtaka atubu na kumuamini Yesu sasa iwapo mtu huyo akaamua yeye mwenyewe kuikataa ile sauti na kutamka maneno ya kufuru kwa kinywa chake dhidi ya ile sauti basi Roho Mtakatifu huondoka ndani yake na hawezi kamwe kumsikia akimwambia habari njema za wokovu,na hapo ndo tunasema mtu huyo amemkufuru Roho Mtakatifu, hawezi kusamehewa kamwe si kwa sababu Mungu ataikataa toba yake hapana ila ndani yake hawezi kupata hata hamu ya kutubu hadi atakapokufa kwa sababu ili mtu atubu ni lazima Roho Mtakatifu aseme nae ndani yake. Yeyote mwenye kusikia hatia ndani yake anaye Roho Mtakatifu lakini yule asiyetaka kuungama dhambi zake hana kabisa uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha yake…

Na ikiwa mtu tayari ni mkristo amekubali kabisa kumfata Yesu na ameuona wema wa Mungu anatambua kuwa Kristo alimfia msalabani, anaujua uwepo wa Roho Mtakatifu lakini akaamua kuasi na kuiacha njia ya wokovu kisha akanena maneno ya kufuru juu ya Roho Mtakatifu au juu ya mtu anayehubiri injili ya Kristo, basi Roho Mtakatifu ataondoka ndani yake wala hatarudi tena ile sauti iliyokuwa inamshitaki anapokuwa katika njia mbaya hataisikia tena, hatapata hamu ya kutubu na hawezi kamwe kuupenda wokovu kwa sababu Roho ambaye angemvuta kufanya hivyo hayupo tena ndani yake.

Waebrania 6:4 “Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5 na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,

6 wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.

7 Maana nchi inayoinywa mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuzaa mboga zenye manufaa kwa hao ambao kwa ajili yao yalimwa, hushiriki baraka zitokazo kwa Mungu;

8 bali ikitoa miiba na magugu hukataliwa na kuwa karibu na laana; ambayo mwisho wake ni kuteketezwa.”

Lakini kuna namna mtu wa Mungu anarudi nyuma au kupoa , hali hii hutokea pale ambapo mtu anapunguza kufanya mambo ya kiroho kwa mfano mtu alikuwa muombaji sana lakini badae anapunguza alikuwa anahubiri injili sana lakini badae anapunguza. Mtu huyu anapoa lakini haimaanishi amekuwa baridi, aliyekuwa baridi ni yule aliyeacha kabisa njia ya wokovu ni vigumu kwake kurudi tena katika njia ya wokovu na anaweza kuangukia katika dhambi isiyo na msamaha ila yule aliyerudi nyuma bado ana nafasi ya kutubu na kurudi kwa Bwana kwa sababu Roho Mtakatifu bado anamshuhudia ndani yake juu ya habari za wokovu.

Shetani nae akiona mtu karudi nyuma kitu cha kwanza anaweka uzio ili asiweze kurudi mahali alipokuwa, hufanya hivyo kwa kumwambia HUWEZI KUSAMEHEWA DHAMBI ZAKO au anamwambia TAYARI UMEMKUFURU ROHO MTAKATIFU.

Mtu wa Mungu akiisikiliza hiyo sauti huvunjika moyo na kupata mawazo mengi. Ndani yake hasikii hamu ya kusonga mbele, mtu huyu hajamkufuru Roho Mtakatifu kwa sababu bado anatamani kurudi kwa Bwana, ndani ya moyo wake anataka kuziungama dhambi zake hali hii hutokea kwa sababu Roho Mtakatifu yupo ndani yake kusema naye japokuwa shetani anamwambia ana dhambi isiyo na msamaha milele.

Kwa mfano, mtu mmoja aliyepata changamoto kama hiyo alinituma ujumbe inbox akiwa hajui nini cha kifanya. Ujumbe wake ulkuwa kama ifuatavyo

Shalom, swali langu ni kwamba je mtu akiokoka halafu akakengeuka ila akarudi tena kuomba toba madhabahuni je mtu hyo atakuwa kasamehewa au hajasamehewa? Na jina lake litaendelea kuwepo kwenye kitabu cha uzima?

Nilimpa majibu ya swali hilo kisha nikamtumia somo linalohusiana na swali lake , lakini akaendelea kuniambia.

‘Asante sana mtumishi wa Mungu… Mimi nimeokoka lakini kuna kipindi nilianguka nikazaa kabla ya kuingia kwenye ndoa, wakati naishi ma mwanaume wangu nilkuwa nikishika mimba ananiambia nitoe na mimi nafanya hivyo lakini badae nikaanza kuishiwa amani kwa kitendo nilichokuwa nafanya, nikaenda kwa mchungaji nikamwelezea akanikemea na kunitenga nisifanye huduma kwa muda kisha akaniambia nisirudie tena kufanya dhambi Mungu ataniacha, siku moja nikiwa nmehudhuria ibaada kuna mpendwa akauliza swali nililokuuliza na mchungaji akajibu akasema mtu huyo hasamehewi tena ila tunaendelea kufarijiana lakini hakuna msamaha hapo basi toka siku hiyo lile neno linaniumiza sana sijui nifanye ili niweze kurudisha amani yangu katika kumwabudu Mungu “

Nilipousoma ujumbe wake nilimwambia kuwa alichofanya mchungaji wako ni sahihi kabisa ulitakiwa kutengwa kwa dhambi uliyofanya kama maandiko yanavyosema(1 Wakorintho 5:9-13) tena alikuwa sawa kukwambia usirudie tena dhambi ile, yaani utubu ila alipojibu lile swali la mpendwa mwenzio kusema kuwa mtu huyo hasamehewi sijui kwa nini alitoa jibu hilo yamkini alimjibu vile lakini si kwa kulinganisha na tatizo ulilonalo wewe, yawezekana alimaanisha mtu aliyekengeuka na kuuacha kabisa wokovu na kukufuru huyo kweli hatuwezi kumfariji kwa sababu hana tena hamu na maisha ya wokovu ataendelea kudanganywa na adui na kuishia kutamani mambo maovu..

2 Timotheo 3: 13 “lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika”..

Lakini sio wewe maana wewe bado unapata msukumo wa kutubu ndani yako yaani Roho Mtakatifu.


Endapo huo msukumo usingekuwepo ndani ya huyo dada na akaendelea kufurahia tabia hiyo basi hapo angepata dhambi isiyosamehewa kwa sababu Roho Mtakatifu mwenye kumpa msukumo wa kutubu hayupo tena ndani yake (Yohana 6:44)

Tatizo hili limewapata watu wengi hasa wale wanaofanya dhambi ya kuua, ubakaji, kutoa mimba, mizaha iliyovuka mipaka katika madhabahu ya Mungu.

Mtu anaweza kufanya dhambi hizo ndani yake anasikia sauti inamuambia atubu pindi tu anapokumbuka alishaua kuna sauti inamwambia huwezi kusamehewa tayari anavunjika moyo kabisa, mtu mwingne yawezekana alifanya kitu kibaya ambacho hawezi hata kusema mbele za watu lakini yanapokuja mawazo kama haya wakati unataka kutubu mtu wa Mungu inakupasa UYAKATAE tena uyashinde kwa sababu ni mawazo mabaya adui anaweka ndani yako.


Lakini pia jitahidi usitende dhambi ili usipate madhara kama hayo ya kuletewa mawazo ya kukukandamiza, usipofanya dhambi shetani hapati nafasi ya kupitisha mawazo yake mabaya kwako. Na kuna uwezekano mkubwa kabsa Roho Mtakatifu akaondoka ndani ya mtu ambaye tayari alishaamini na lakini badae akatenda dhambi na kumkataa Roho Mtakatifu, na mtu huyu hatasikia hamu ya kumpenda Mungu matokeo yake ataishia kuipinga injili na wokovu milele.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *