Shalom Mwana wa Mungu, Nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tujifunze maneno ya uzima ya Mwokozi wetu Yesu Kristo.
Mtume Paulo katika mstari huu ametaja mambo makuu matatu kabla ya kwenda kuyatazama kwa undani tusome mstari huo unasemaje!
Wafilipi 3:2 “Jihadharini na mbwa, jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao”
Mtume Paulo alikuwa akilionya kanisa lililokuwa Filipi lijiepushe na watu hawa wa aina Tatu. Ambao tutatazama hapa kundi moja baada ya kundi jingine.
makundi makuu matatu Mtume Paulo aliyowaonya Wafilipi wajiepushe nayo.
1.WATU WATENDAO MABAYA.
2.WATU WAJIKATAO.
3. MBWA.
tutatazama kundi moja baada ya jingine ili pia na sisi watu wa nyakati hizi za Mwisho tujiepushe nayo vivyo hivyo.
1. WATU WATENDAO MABAYA.
watu wanaozungumziwa hapa ni watu ambao tayari wapo katika Imani lakini wanatenda mambo mabaya wakati mwingine kwa siri siri lakini pia hata wazi. Ni watu wasioweza kujizuia katika kutenda mabaya.
Watu wa namna hii Biblia imetuonya tujiepushe na wala tusichangamane nao maana mwisho wa siku tukichangamana nao tutakuwa kama wao. Jambo kama hili mtume Paulo aliliandika katika nyaraka zake nyingi kulionya kundi/kanisa la Kristo linalomtafuta Kristo.
1 Wakorintho 5:9-11.
1Wakorintho 5:9 “Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi.
10 Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang’anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia.
11 Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang’anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye”.
Moja ya kusudi pia la kutokuchangamana nao ni wao watakapoona mbona watu hawataki kuchangamana nao? Ili waone pia kile wanachokifanya sio kitu kizuri na mwisho wa siku wabadilike na kuipita njia iliyo sahihi wakiuacha uovu wao.
2. WATU WAJIKATAO.
watu wanaozungumziwa hapa ni Wayahudi ambao walikuwa wakiwataabisha watu wa Mataifa waliomwamini Yesu Kristo kuwa pasipo tohara pia ya mwilini hawawezi kukubaliwa na Mungu mfano wa makanisa waliyoyataabisha ni yale ya Galatia.
Kundi hili lilikuwa pia limemwamini Yesu Kristo lakini lilikuwa linaendeshwa na torati. Hawakufahamu kuwa torati haiwezi kumkamilisha mtu isipokuwa neema pekee ya Mwokozi wetu Yesu Kristo.
Ndio maana mtume Paulo analisema hili.
1Wakorintho 7:19 “Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu.
20 Kila mtu na akae katika hali ile ile ambayo alikuwa nayo alipoitwa”
Hivyo kushika miezi,sikukuu,miaka,kutokula vyakula fulani,kushika sabato haya yote hayamkamilishi mtu.
3. MBWA.
Sasa kama ni msomaji wa Biblia kabla Bwana Yesu hajatoka hapa duniani kundi hili alilisema wazi wazi kabisa kuwa mbwa ni wakina na nani? Tusome…
Mathayo 7:15 “Jihadharini na MANABII WA UONGO, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni MBWA-MWITU WAKALI.
16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti”
Unaona hapo!, kumbe mbwa wanaozungumziwa hao ni Manabii wa uongo, na Bwana Yesu hakuishia kutaja mbwa peke yake bali anasema mbwa mwitu wakali. MBWA WAKALI yaani wasio Jali kundi wala kulihurumia hata kidogo wao wapo kuliangamiza kabisa.
Ni watu wanaoonekana kuwa ni watumishi wa Mungu kabisa kwa nje lakini kumbe sivyo wanafanana kabisa na watumishi wa kweli wa Mungu lakini Bwana Yesu anasema “…..mtawatambua kwa matendo yao…” yaani kile wanachokifundisha na wanachokiishi.
Maana haiwezekani kufundisha kitu mtu asichokiishi.
ili kuliweka wazi hili Biblia inapozungumzia manabii wa uongo haimaniishi manabii tu peke yao bali ni mjumuisho wa wachungaji wa uongo,waalimu wa uongo,mitume wa uongo,waimbaji wa uongo yaani watu wote wanaosimama kuitangaza injili. Maisha yao kwa nje yana akisi Ukristo lakini sivyo.
Hivyo mtu awaye yote anaehubili injili inayomfanya mtu aendelee kukaa katika dhambi basi huyo kwa lugha ya biblia ni mbwa tena mbwa mwitu mkali asiejali kitu kabisa.
Kumbukumbu 13: 1 “Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,
2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;
3 wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.
4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye”
Jambo la kujiuliza je? Unaongozwa na nani? Miujiza, manabii wa uongo, au Neno la Mungu?.
Kumbukumbu 6:4 “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.
5 Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote”.
Basi tafakari vyema na chukua hatua fanya neno la Kristo kuwa ndio kiongozi wako kamwe hutapotea kabisa.
Ubarikiwe sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://Whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.