NI AINA GANI YA MARAFIKI ULIONAO?

Biblia kwa kina No Comments

Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo.  Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.

Kama watu tuliomwamini Yesu Kristo ni lazima kuwa makini na aina za marafiki tulionao. Kabla ya kuenda katika kiini cha somo letu ni vyema tufahamu rafiki ni nani?

Rafiki ni mtu wa karibu unayemwamini kwenye maisha yako ya kila siku. Anakuwa anafahamu siri zako na mambo yako mengi maana ikiwa unamwamini lazima utamshirikisha baadhi ya mambo yako ya ndani kabisa.

Tulipokuwa watoto wadogo tukiwa hatufahamu kupambanua vizuri wazazi wetu, walezi wetu na hata walimu mashuleni walikuwa wanatuonya kutokuwa na urafiki na watoto fulani ambao tabia zao hazikuwa nzuri. Tulikuwa tunaonywa na kukatazwa na wazazi lakini bahati mbaya wakati mwingine hatukuwa tunaelewa kwa nini wanatwambia hivyo tena wanakuwa ni wakali juu ya kuendelea kushikana na watoto wengine ambao walikuwa wanatambuliwa kuwa na tabia mbaya wakati mwingine tulikuwa tunakumbana na adhabu kutoka kwa wazazi/ walezi pia.

Lakini tuliona kama tunaonewa na kuona wale watoto mbona hawana tabia mbaya!, wako sawa tu.. lakini baada ya kuwa wakubwa na kujitambua na kuona hatima za wale watu ambao tulikuwa tunakatazwa kujenga nao urafiki ndio tunaona kwa nini wazazi/ walezi walikuwa wanatukaza kabisa kuwa pamoja nao.

Sasa maandiko yanasema..

Mithali 13:20“Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

Sasa siku zote mambo ya mwilini ni mfano halisia kabisa wa mambo ya Rohoni. Na ndio maana vivyo hivyo kwenye maisha ya rohoni tunaambiwa.

WATU WENYE HEKIMA KWA MUNGU NI WATU WA NAMNA GANI?

Ni watu walio mwamini Yesu Kristo yaani waliookoka na wenye hofu ya Mungu ndani yao.

Mtu yeyote alieokoka kweli kweli na anatembea kwenye njia za Mungu mtu wa namna hii ni mtu mwenye hekima mbele za Mungu na mtu wa namna hii ni mtu wa kukaa nae karibu sana na kutaka mashauri mengi kutoka kwake maana Roho wa Mungu yuko ndani yake.

Utajikuta unafata mwenendo wake utajikuta unakuwa muombaji,Muinjilisti,Mfungaji, mtu usietoa matusi mdomoni mwako, utajikuta unapata maarifa mengi zaidi ya Neno la Mungu maana unakuwa karibu na mtu ambae nguvu za Mungu ziko ndani yake na wewe utajikuta unakuwa mtu wa namna hiyo hiyo.

Hata Hekima na maarifa aliyokuwa nayo Mwokozi wetu Yesu Kristo haikutoka juu tu moja kwa moja lakini pia ilichangiwa pia na aina ya watu wale aliochagua kukaa nao.

Ni siri kubwa ipo hapa si kwamba Yesu asingepata hekima na maarifa yake kama asingelika na watu wao watu wa imani/viongozi wa dini lakini ilikuwa ni njia ama alikuwa anatuonyesha sisi na kutupa siri hii kubwa kuwa ili pia tuzidi kuwa na hekima na maarifa ya Ki-Mungu hatuna budi kukaa na watu sahihi.

 

Tunaona wakati walipokuwa wakitoka Yerusalemu kuila sikukuu ya pasaka Yesu pamoja na mama yake na baba yake tunaona katika maandiko wakati wa kuondoka wazazi wake hawakumuona baada ya kutoka katika mji ule lakini Yesu aliekuwa kijana wa miaka 12 angeliweza kwenda kucheza michezo na watoto wengine kama kombolela, kwenda kwenye michezo ya namna mbali mbali lakini tunaona alichagua kukaa na wale viongozi wa kidini hivyo akawa napata maarifa kwa watu wale mengi zaidi na yeye akipata mambo mengine mengi zaidi. 

 

 Luka 2:40  Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.

 41  Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka.

42  Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu;43  na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari.

44  Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao;

45  na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. 46  Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, AMEKETI KATIKATI YA WAALIMU, AKIWASIKILIZA NA KUWAULIZA MASWALI.

47  Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake.

48  Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.

49  Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?

50  Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia

Kuna mahali katika ukuawaji wa kiroho kama Mkristo huwezi kukua kama hutachagua aina za marafiki wa kuwa nao leo hii ni Mkristo lakini marafikiwa wake wakubwa ni wanachuo wenzake, wafanya biashara wenzake,wafanyakazi wenzake wa ofsini wenzake nk.

Ndugu kuna tabia zingine hazitatoka na zingine hazitazalika kabisa kama hutaamua kukaa na marafiki ambao ni wazuri(wenye hofu ya Mungu) 

Leo hii unakuwa Mkristo lakini ni mzito wa kuomba, kusoma Neno, kufanya uinjilisti ukiangalia unashinda na marafiki ambao si Wakristo wala si waombaji unatazamina mambo hayo yatokee. Haitawezekana kamwe ndugu. 

Hivyo ili uwe muombaji ni lazima utembee/kampani yako iwe ni ya wabaji,wasomaji wa neno, washuhudiaji. Bila hivyo hata kama una moto kiasi gani na unamfahamu sana Mungu hutaenda mbali utapoa tu. Huwezi kuwa mwenyewe mwenyewe tu na ukapiga hatua kubwa zaidi akushinda ungelikuwa na watu wenye tabia za uombaji, usomaji neno nk.

Hivyo ndugu angalia marafiki uliona ndio wanaotoa mwenendo wako upoje katika roho. Ukombowe wakati hizi ni siku za mwisho.

Ubarikiwe sana.

Maranatha. 

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *