NINI MAANA YA KUOMBA KWA BIDII(YAKOBO 5:17)? 

Maswali ya Biblia No Comments

Nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo. 

Pengine umewahi kujiuliza maandiko yanaposema kuwa “Eliya nae alikuwa ni mwanadamu na mwenye tabia moja na sisi lakini aliomba kwa BIDII…nk” ni swali ambalo Wakristo wengi wanatamani kufahamu ni kwa namna gani Eliaya aliomba kwa bidii? Tunafahamu tu maandiko yanasema kuwa Aliomba kwa bidii lakini ni kwa namna gani?.

Sasa ili tuweze kuelewa Habari hii ni vyema tukavitazama/kuvirejerea vifungu hivyo kwa ufupi ili tupate kuona maandiko yanasema nini kabla ya kwenda kwenye kiini cha swali hili..

Yakobo 5:17 “Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.

18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.” 

Mistari hii inatuonyesha kwa ufupi tu tuangalie pia na Habari yenyewe kwa ufupi katika matukio yote mawili la kuzuia mvua na kunyesha mvua.

 

 1Wafalme 17:1 “Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.

2 Neno la Bwana likamjia, kusema,

3 Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani.

Tunaona katika habari hii inaanza tu Eliya anasema maneno hayo kuwa hakutakuwa na mvua biblia haijaweka maelezo mengine zaidi ya hapo ila tunaona tukio hilo linatendeka.

Lakini tukiendelea kusoma katika sura inayofata..

1Wafalme 18:41 “Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele.

42 Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini.

43 Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba.

44 Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.

45 Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli.” 

Ukisoma kwa makini hapo katika mstari wa 41 Eliya anamwambia Ahabu kuwa mvua itanyesha ikiwa kabla hata hajaenda kumuomba Mungu. Kwa maana nyingine Eliya tayari alikuwa ameamini moyoni mwake kuwa ni kweli na hakika mvua itanyesha.

Ndio maana utaona alikuwa na ujasiri wa kumwambia Ahabu kuwa mvua itanyesha tele.

Sasa jambo la kulitazama kwa kina hapa tunaona baada ya kumwambia vile alikwenda kuomba mbele za Mungu ikiwa tayari ameshakwisha kuamini moyoni mwake kuwa Mungu atanyeshea mvua Israeli yote..

Sasa tunaona hapa anaanza kuomba Eliya lakini hakukuwa na matokeo yoyote yale. Hata alipomtuma mtumishi wake akaangalie hakuona kitu. Akamrudishia taarifa. Eliya akaingia tena mara ya pili magotini kuomba mara ya pili tena akijua baada ya hapo itakuwa tayari lakini haikuwa hivyo.. akamtuma tena mtumishi wake akaleta majibu kuwa hakuna dalili yoyote ni jua na ukame tu. Lakini Eliya hakukata tamaa akafanya hivyo tena kwa mara ya tatu na ya 4 mpaka mara ya 7. Huenda Eliya alitumia zaidi ya masaa 7 akiomba bila kukata tamaa maana alikuwa na uhakika kuwa mvua itanyesha.

Lakini mara ya 7 mtumishi wake akaleta taarifa kuwa kuna kawingu kadogo kama mkono wa mtu. Tunaona hakuendelea kuomba tena baada ya kupata taarifa hiyo akaamini kuwa tayari imeshakuwa akaondoka.

Tunaona Eliya alienda mara 7 maana yake asingetoka kama kusingekuwa na ishara hiyo hata ingelikuwa mara 100 angeenda magotini akijua Mungu tayari ameshakwisha kutenda kile alichokiomba maombi ya namna hii huko ndio kuomba kwa bidii bila kuchoka wala kukata tamaa. 

Hivyo kwa namna hii pia sisi inatakiwa tuwe nako. Hata tunapoamini Mungu ametusikia na atatutendea pale tunapompelekea maombi Yetu. Tuendelee kudumu uweponi mwake/magotini pale majibu/kile tunachotarajia kukiona kinachelewa lakini kuzidi zaidi sana kumwamini Mungu. 

Hivyo kuomba kwa bidii kunaozungumziwa hapo katika maandiko ni kuendelea kumwamini Mungu hata kama kile tunachohitaji hakijaja kwa wakati mpaka pale kitakapokuja kuendelea kuweka imani na kumshukuru. 

Ubarikiwe sana. 

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *