Je kuna tofauti gani kati ya sauti ya Roho Mtakatifu na sauti ya malaika?

Maswali ya Biblia No Comments

 

Ili tuelewe vizuri, kwanza tufahamu kuwa Mungu anaweza kuzungumza na mtu moja kwa moja, au akatumia malaika wake kumpa mtu ujumbe au akamtumia mwanadamu…na pia wakati mwingine hutumia hata wanyama na vitu, kwa mfano kama wewe ni msomaji wa biblia utakumbuka ile habari ya Balaamu, wakati alikuwa anaenda kuwalaani wana wa Israeli, Mungu alimtokea njiani na akasema naye kupitia punda ambaye Balaamu alikuwa amempanda(Hesabu 22:30)

Kwa kulithibitisha hilo kwamba Mungu anaweza kuzungumza na mtu kupitia wanyama na vitu vya asili..soma (Ayubu 12:7-9). Hiyo ni njia ambayo Mungu anaweza akazungumza na mwanadamu japo huwa ni mara chache chake.

Sasa linapokuja suala la Mungu kuzungumza na mwanadamu kupitia Roho Mtakatifu au Malaika..ni vizuri tufahamu kuwa wanadamu na wanyama ni viumbe wa mwilini, hivyo Mungu hawezi kuzitumia roho zao kuzungumza na sisi…kwamfano Mungu hawezi kutumia roho yangu au ya mtu fulani kuzungumza na roho ya mtu mwingine…atakachokifanya Mungu akiamua kutumia hiyo njia ya mwanadamu kusema na mwanadamu mwenzie..ni kumpa mtu ujumbe katika roho kisha huyo mtu atafikisha huo ujumbe kwa mhusika. Ni Roho Mtakatifu pekee na Malaika watakatifu ndio wenye huo uwezo wa kuzungumza na sisi kwa njia hiyo ya rohoni kwasababu wao ni wa rohoni..

Malaika anaweza akaja kwa mwonekano wa kibinadamu na kumpa mtu ujumbe wa Mungu, au pia anao uwezo wa kuzungumza na mtu moja kwa moja kwenye roho yake bila kutumtokea wala kuonekana.

Sasa jambo la muhimu unalopaswa kufahamu kuhusu sauti ya malaika pindi anapozungumza na mtu ni kwamba…Malaika wa Mungu hawazungumzi kitu kama watakavyo wao…kila wanachokisema au kila ujumbe wanaotupa ni ujumbe kutoka kwa Roho Mtakatifu kama ulivyo (haujaongezwa wala kupunguzwa).

Kwahiyo sauti zao ni sauti za Roho Mtakatifu mwenyewe…Ikiwa na maana kuwa Malaika anapozungumza na wewe rohoni, ujue kuwa ni Roho Mtakatifu anazungumza na wewe, kwasababu Malaika anazungumza kitu alichoambiwa na Roho Mtakatifu akiseme vile vile.

Kwamfano hebu tusome mistari michache ifuatayo..

Mwanzo 22:10 “Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.

11 Ndipo MALAIKA WA BWANA AKAMWITA KUTOKA MBINGUNI, AKASEMA, IBRAHIMU! IBRAHIMU! NAYE AKASEMA, MIMI HAPA.

12 Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee.

13 Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.

14 Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire,kama watu wasemavyo hata leo,Katika mlima wa BWANA itapatikana.

15 MALAIKA WA BWANA AKAMWITA IBRAHIMU MARA YA PILI KUTOKA MBINGUNI

16 akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,

17 katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao”

Umeona katika habari hiyo…hapo tunaona ni Malaika wa Bwana anazungumza na Ibrahimu kama Mungu mwenyewe…jambo ambalo ni ngumu kujua kama huyo ni Malaika au Mungu anayezungumza hapo..

Tusome tena..

Kutoka 3:1 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu.

2 MALAIKA WA BWANA AKAMTOKEA, KATIKA MWALI WA MOTO uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. 3 Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei

4 Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.

5 Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.

6 TENA AKASEMA, MIMI NI MUNGU WA BABA YAKO, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu”.

Bila shaka wengi wetu tunaijua hii habari ya Musa kuona kijiti kilichokuwa kinaungua lakini hakiteketei, na wengi wetu tunajua kwamba ni Mungu ndiye aliyemtokea Musa…lakini kiuhalisia sio Mungu aliyemtokea Musa…Bali ni Malaika wa Mungu ambaye alibeba maneno ya Mungu kama yalivyo, ndiye aliyemtokea Musa katika kile kijiti kilichokuwa kinawaka lakini hakiteketei, Siku zote Malaika anapotoa ujumbe ni kama tu msemaji wa Raisi anayesoma waraka wa Raisi mbele ya watu..atasoma mpaka sahihi ya mwisho iliyoandikwa (mimi Raisi nimesema haya yote yafanyike)!.

Hebu tusome tena katika kitabu cha Waamuzi 2:1

Waamuzi 2:1 “Kisha malaika wa Bwana alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nalisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi.”

Umeona na hapo? Malaika anasema “Mimi nimewatoa Misri na kuwaleta katika nchi niliyowaapia baba zenu,… milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi.” Bila shaka hakuna mahali popote malaika alishawahi kuingia agano lolote na wana wa Israeli, ni Mungu ndiye aliyeingia agano na wana wa Israeli,.. kwahiyo hapa ni Malaika anazungumza ujumbe wa Mungu. Ni kama vile anarudia kuzungumza kile kitu Mungu alichomwambia azungumze (ni kama ule mfano wa msemaji wa Raisi anaposoma waraka wa Raisi mbele ya watu ndicho malaika anachokifanya)

Malaika anapotoa ujumbe wa Mungu..mara nyingi hasemi ni “Mungu kasema” bali huwa atarudia kuzungumza kile Mungu alichokizungumza, sasa hali kama hiyo inatupa ugumu wa kutofautisha sauti ya Roho Mtakatifu na ya malaika,.. Kwani wakati malaika anapozungumza na wewe katika roho yako hutasikia akisema Mungu kasema fanya hiki na kile…utasikia tu sauti akisema “Mimi Mungu nimesema” na wewe unaweza kudhani ni Mungu kazungumza na wewe kumbe ni Malaika wake.

Sasa tufanyaje ili tuweze kuzitofautisha hizi sauti?

Kitu cha msingi na muhimu ambacho unapaswa kutafuta si namna ya kutofautisha sauti ya Roho Mtakatifu na ya malaika kwasababu haikusaidii, unachopaswa kutafuta ni kujifunza kutii kile unachoambiwa na sauti ya Mungu, iwe ni kupitia malaika au Roho Mtakatifu mwenyewe.kilicho cha muhimu na cha maana zaidi ni sisi kutii kile tulichokisikia maadamu tumehakiki ni ujumbe kutoka Kwa Mungu..

Hebu jitafakari je! Umewahi kutii sauti ya Mungu? Pale ambapo inakuhubiria uache ulevi,uasherati, usengenyaji,wizi, uongo, rushwa, kamari, na mambo yote maovu, je unatii sauti ya Mungu??

Ikiwa we ni mwanamke na umesikia sauti ya Mungu ikikuambia uache huo uvaaji wako mbaya wa kuvaa vimini, suruali, nguo za kubana zinazochora mwili wako, hizo vipodozi unazojibuanacho ngozi yako, hayo mapambo ya kidunia unazotia Kwenye mwili wako(makeup, lipstick, wigi, wanja, hereni, mikufu, n.k) hiyo rangi unazopakaa kwenye kucha, nywele, na kila aina ya mapambo, ni mara ngapi umesikia sauti ya Mungu ikisema nawe uachane na huo uchafu, hiyo njia unayoiendea maana itakufikisha Jehanum,

kama hukuwahi kusikia sauti ya Mungu ikisema kwa namna hiyo na kukujulisha kuwa hayo yote ni machukizo mbele zake..basi leo umesikia, chukua hatua ya kutii kwa kuamua kubadilika na kuachana na njia zako, acha kabisa udunia, futa picha zote chafu unazozitazama, futa hizo miziki yote ya kidunia maana zitakupeleka kuzimu, hizo filamu,gemu,mipira, mwisho wake ni jehanum, tii sauti ya Mungu..

1Samweli15:22 “Naye Samweli akasema, je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kutii sauti ya BWANA?
Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.”

Shalom: Bwana atusaidie

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *