USILALE USINGIZI WAKATI HUU WA KUMNGOJEA BWANA

Siku za Mwisho No Comments

USILALE USINGIZI WAKATI HUU WA KUMNGOJEA BWANA

Biblia inatusihii tusilale usingizi sisi tulio wana wa nuru..hasa katika wakati huu wa kungojea parapanda ya mwisho, huu ni wakati wa kukesha kweli Kweli.

1 Wathesalonike 5:1 Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.

[2]Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

[3]Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.

[4] Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.

[5]Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.

[6]BASI TUSILALE USINGIZI KAMA WENGINE, BALI TUKESHE, NA KUWA NA KIASI.

[7]Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.

[8]Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.

Kuna hatari kubwa ya kulala usingizi wa kiroho katika wakati huu, na hatari ni kuachwa na Bwana bila kutarajia.. kama tunavyojua siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku kuiba, wakati watu wamelala…ni wale tu waliokesha ndio watakaosalimika.

Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku”.

Mathayo 24:40 Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;

[41]wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.

[42]Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.

[43]Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.

[44]Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.

Samsoni alipolala usingizi, hakujua saa ambayo nguvu zake ziliondolewa, hakujua muda ambayo Bwana alimwacha, alikuja kushutukia tu ameachwa siku nyingi na nguvu zake zimeisha, na habari yake ikawa imeisha hapo..kilichobaki ni dhiki kuu tu kutoka kwa Wafilisti.

Waamuzi 16:19 Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka.

[20]Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. AKAAMKA KATIKA USINGIZI WAKE, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. LAKINI HAKUJUA YA KUWA BWANA AMEMWACHA.

[21]Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.”

Usilale usingizi wakati huu wa kumngojea Bwana!!

Bwana alikwisha kututahadharisha tuwe tayari muda wowote, tuwe kama watumwa wanaomungojea Bwana wao.

Luka 12: 35 “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; 

36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. 

37 HERI WATUMWA WALE, AMBAO BWANA WAO AJAPO ATAWAKUTA WANAKESHA. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. 

38 Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao. 

39 Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. 

40 Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.”

Soma tena..

Marko 13:35 “Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi; 

36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala. 

37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni”.

Huu ni wakati wa kukesha!!

Na kumbuka kukesha kunakozungumziwa kwenye biblia, si kuacha kulala usiku, ni heri kama ingekuwa hivyo…lakini kukesha kunakozungumziwa hapo ni kukesha katika roho.

Roho zetu zinalala, kama vile miili yetu inavyolala, roho zetu nazo zinasinzia kama vile miili yetu isinziavyo.

Mtu anapokuwa katika shughuli nyingi, na usiku unapoingia, ni kawaida mwili kusinzia wenyewe, na hata kupotelea kabisa usingizini, hali kadhalika katika ulimwengu wa roho, mahali penye giza nene, kunashawishi roho zetu kulala, hata kama sisi hatutaki.

Na sasa tunaishi nyakati ambayo ni ya giza nene kiroho, na hivyo roho za watu wengi zimelala. Tunajuaje kama tunaishi katika giza nene kiroho?

Tunatambua kwa matendo ya giza yanayoendelea sasa duniani.

Warumi 13:12-13 Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru.

[13]Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.

Umeona?.. matendo yote mabaya, biblia inayataja kuwa matendo ya giza. Mfano wa matendo hayo pia utaona yametajwa kwa wingi katika kitabu cha wagalatia 5:19-20.

Sasa ili tuwe salama hatuna budi kuyavua matendo ya giza na kuvaa matendo ya Nuru, ambayo ni “matendo matakatifu” kama vile kuomba, kusoma Neno la Mungu, kujihadhari na dhambi zote kama uasherati, ulevi, wizi, utukanaji, uongo, usengenyaji, uvaaji mbaya, kupenda dunia n.k

Na kwa kufanya hivyo tutahesabika mbele za Mungu kama watu wanaokesha, ambao hawajalala, na hivyo siku ile Bwana atakayokuja haitakuwa ya ghafula kwetu, kwasababu atatukuta tukiwa macho kiroho, hatujalala!.

1 Wathesalonike 5:4-8 Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.

[5]Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.

[6]Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.

[7]Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.

[8]Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.

Lakini kama bado hujaokoka!, fahamu kuwa upo usingizini, na siku ile ya Bwana itakujia ghafla kama mtego unasavyo, na hautakwenda na Bwana mawinguni.

Hivyo huu ni wakati wako wa kuamka usingizini, wala usingoje kesho!.

Waefeso 5:14 Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.

[15]Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;

[16]mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.

Na unaamka kutoka katika usingizi wa kiroho, kwa kutubu na kumaanisha kuacha dhambi zako zote (yaani kuokoka), na vilevile kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa jina la Bwana YESU KRISTO (Matendo 2:38). Na baada ya hapo unaendelea kuukulia wokovu kwa kudumu katika kufanya ushirika na kujifunza Neno la Mungu na kuomba, pamoja na watakatifu wenzako.

Kumbuka parapanda ya Bwana ipo karibu..dalili na ishara zote zinatuonyesha.

Mfalme anarudi!!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *