
Jinsi mitandao inavyowafunga watu na kuwaweka mbali na Mungu.
Biblia inasema..
1Wakorintho 10:23 “Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo.”
Hii ikiwa na maana kuwa mitandao ni mizuri inaturahisishia vitu vingi na tunapata faida lakini pia sio kila mtandao unafaa. Hivyo tunapaswa tuwe makini sana tunapoitumia.
Katika hizi siku za mwisho, shetani anawafunga watu wengi sana na kuwapeleka kuzimu kupitia mitandao.
Zamani ilikuwa ni rahisi kumtambua mtu anayefanya dhambi kwa kumtazama tu au kumwangalia mienendo yake kwasababu karibu kila uovu uliokuwa unafanyika, chanzo chake kilikuwa ni cha nje kabisa kinachoonekana, kwa mfano zamani ilikuwa ili kuwapata watu wanaotembea tupu au makahaba ilikuwa ni lazima uende mahali kama kasino, au disco za usiku, au kwenye madanguro lakini sasa hivi mambo hayo yote unayapata mitandaoni na kwenye simu za mikononi bure, maovu yanayotendeka sasa hivi kwa siri ni mabaya zaidi kuliko hata yale ya kipindi kile,..mtu anaweza akatembelea madanguro hata 30 katika simu yake kwa siku moja.
Unaweza ukajifanya mwema kwa nje, haunywi pombe, hauendi disco, hauzini na wanawake, au wanaume, tena umebatizwa, na unasema wewe ni mkristo, lakini ndani ya simu yako kwa siri ume download video za pornography unatazama na hakuna mtu anayejua, lakini biblia inasema..
Mhubiri 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja NA KILA NENO LA SIRI, likiwa jema au likiwa baya”.
Sasa hivi mitandao ya simu imewafunga watu wengi hata wale wanaosema wameokoka, kiasi kwamba mtu hawezi kujizuia kabisa.
Utakuta mtu anasema ni mkristo lakini kwenye simu yake amejaza miziki za kidunia, filamu za kidunia, picha za ajabu ajabu, vichekesho visivyo na maana, magemu ya kila aina, anaweza kukaa masaa mawili kucheza hayo magemu na kutazama hizo picha lakini kukaa lisaa moja kwenye maombi au uweponi mwa Mungu hawezi, mtu huyu hajaokoka! Haijalishi amekaa miaka mingi ndani ya kanisa, anahitaji msaada wa kiMungu.
Ukweli ni kwamba mitandao mingine zimetoka kuzimu moja kwa moja, na lengo ni kuchafua roho za watu na kuwaweka mbali na Mungu (hususani wakristo).
Ndio maana mkristo aliyeookoka kweli kweli na kujazwa Roho Mtakatifu hawezi kuingia huko mitandaoni na kuperuzi peruzi ovyo, hawezi tumia muda wake kukaa huko TikTok, Facebook, Instagram, Twitter n.k kufuatilia vitu visivyo na maana kama hizo vichekesho, picha za hovyo, filamu ambazo zimejaa maudhui ya uasherati.
Mwingine atasema ni kujifurahisha tu na kujiburudisha lakini hajui kuwa anajiingiza kwenye shimo refu la kuzimu.
Ndugu ni vizuri ufahamu ukweli ili uokoke na kuzimu, ukweli ni kwamba hayo magemu, movies, miziki na hizo vichekesho unazofuatilia huko, nyuma yake kuna mapepo na maroho chafu ambayo kazi yake sio kukuchekesha na kukufurahisha kama unavyodhani bali ni kukuweka mbali na Mungu na kukupeleka kuzimu.
Huwezi kusikiliza hizo miziki, na kutazama hizo picha na kucheza hayo magemu halafu ukawa na nguvu ya kuomba, au kusoma biblia huwezi.
Utakesha huko kwenye Fecebook na TikTok lakini kujishughulisha na ibada kwa Mungu huwezi. Unategemea vipi usiwe mtu wa hasira, mtu wa vinyongo, visasi, uchungu, na mawazo mabaya na tabia zote mbaya ikiwa upo katika maisha hayo ya kutojizuia na burudani za kidunia.
Haiwezekani kabisa, mwisho wa siku utaishia kubaki kuwa vuguvugu, sio moto wala sio baridi na hatimaye utatapikwa na Mungu, na ndicho ibilisi anachotaka kwako, Ndio lengo kuu la mitandao hizi, ni kuwafanya wakristo wawe vuguvugu ni ajenda ya ibilisi kwa kizazi hiki cha siku za mwisho. Kumbuka tunaishi katika kanisa la mwisho ambalo linaitwa Laodikia na uvuguvugu ndio ishara kuu kuwa tunaishi katika kanisa hili na Bwana yupo mlangoni.
Ufunuo wa Yohana 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
[15]Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
[16]Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.”
Sasa huu uvuguvugu ni Pepo maalumu lililotoka kuzimu, na kutumwa duniani ili kufanya kazi maalumu ya ushawishi, na hili pepo halijatumwa kwa mtu mmoja hapana bali limetumwa kwa kizazi…Ni pepo lenye nguvu mara saba zaidi ya mapepo mengine yote..Ni pepo linalotenda kazi katika viwango vya juu kabisa vya utendaji kazi wa shetani, ambalo kazi yake hasa ni kuwakosesha wanadamu wa kizazi cha siku za mwisho wamkosee Mungu wao, ili Mungu awakatae kabisa kabisa na kuwakana.
Na anafanya kazi yake kwa kutumia mitandao pamoja na mashirika ya dini za uongo.
Anatenda kazi kwa akili sana kiasi kwamba pasipo Roho wa Mungu, ni rahisi kuwadanganya hata yamkini walio wateule. Atahikikisha anatumia ushawishi mkubwa kumfanya mtu ajione yupo sawa na Mungu wakati bado ni mwasherati, mlevi, mla rushwa, anaishi na mwanamume au mwanamke ambaye hawajafunga ndoa, na bado mtu huyo ajione yupo sawa na Mungu n.k.
Na ili alifanikishe hili kwa urahisi anatumia mitandao kumtenga kwanza mtu na Mungu kwa kumnajisi nafsi yake na kumfanya akose muda wa ibada kabisa. Ndio maana ukiingia huko ni kama umeingia gerezani, kila ukitaka kutoka huwezi..unajikuta unakesha usiku kucha huko, Na hata ukiamka unaamkia huko TikTok, Facebook n.k, utakuwa radhi ukose kumtolea Mungu lakini usikose bando la kuperuzi mitandaoni. Huoni hilo sio jambo la kawaida.
Na mtu akishakuwa vuguvugu hawezi tena kusikia, ni kama amepigwa gazi. Hata akihubiriwaje na kushuhudiwa maandiko mengi kiasi gani hawezi kubadilika, atajiona yupo sawa kumbe amepotea.
Lakini habari njema ni kwamba ipo neema ya Mungu inaachiliwa kutusaidia pale tunapomgeukia na kuamua kuacha uvuguvugu kabisa.
Roho Mtakatifu anajaa ndani yetu na kutusaidia kulishinda hili pepo la uvuguvugu, akiingia na kujaa ndani yako utashangaa ile hamu ya kutazama hayo mambo inaondoka kabisa, hautakuwa tena na hamu ya kusikiliza wala kufuatilia makala za kishetani, hata kufungua hizo mitandao bila sababu hautaweza tena.
Lakini sharti kwanza useme nimeamua kwa moyo wangu wote, na akili zangu zote, na nguvu zangu zote kuanzia leo kumfuata Kristo. Ukafuta video zote ulizozidownload, ukaacha kutembelea website zote za ngono unazotembelea, ukafuta miziki yote ya kidunia, ukafuta magemu yote, na ukakaa mbali na wazinzi wote, basi Mungu atakubadilisha haraka sana.
Ni heri ukatupilia mbali hiyo simu kama inakukosesha kuliko kuwa mtumwa wa ibilisi na ukaenda kuzimu, biblia inasema kiungo chako kimoja kikikukosesha kikate kuliko kuwa nayo na kwenda kutupwa katika ziwa la moto.
Hivyo kama upo tayari kumkabidhi Bwana YESU maisha yako tena, basi sali sala hii ya toba : hapo ulipo Piga magoti, kisha chukua muda mchache mweleze Mungu kuwa ulimkosea, kwa kuwa vuguvugu, na kutenda dhambi nyingi kwa siri, mweleze bila kumficha chochote kwasababu mambo yote uliyokuwa unayafanya kwa siri yote anayajua, hivyo mweleze kuwa hutaki kufanya hivyo tena, na kwamba umedhamiria kuacha maisha ya kidunia na sasa unamfuata Kristo..
Ukishasema hivyo kwa kumaanisha kabisa..Ujue kuwa Bwana YESU amekusikia,..baada ya sala hiyo, ni kufuta sasa hivi bila kuangalia kushoto wala kulia kila picha, mziki, video chafu yoyote uliyonayo kwenye simu, flash, laptop au popote pale na Hatua inayofuata ni kutafuta kanisa la kiroho wanalobatiza ubatizo sahihi wa maji mengi kwa jina la YESU KRISTO nenda ukabatizwe kwa ajili ya kukamilisha wokovu wako, kulingana na Matendo 2:38, Kisha Mungu atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu bure atakayekuwa msaidizi wako, kukufundisha na kukuongoza kulielewa Neno na kuishi Maisha ya utakatifu…Vile vile usiache kwenda kanisani kuanzia leo ili Mungu ayakamilishe maisha yako mpaka siku ile ya wokovu.
Bwana akubariki sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.