
JILINDENI NA CHACHU YA MAFARISAYO NA MASADUKAYO.
Mathayo 16:6 “Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.
Chachu ni nini?. Chachu kwa lugha ya sasa ni HAMIRA, na kwa kawaida ukiitazama hamira unaweza ukadhani ni unga Fulani hivi, lakini kiuhalisia ule si unga bali ni mkusanyiko wa wadudu wenye uhai kwa lugha ya kitaalamu wanaitwa YEAST, hawa wanadudu ndio wanaofanya kazi ya kumengenya ule unga, na kutoa gasi maalumu ambayo ndiyo inaufanya ule unga uumuke. Kwahiyo hamira sio kama chumvi au sukari ambavyo havina uhai ndani yake, Hamira ni kitu chenye uhai kwasababu ni wadudu wale. Na ndio maana ikiwekwa mahali inaweza kubadili maumbile ya kitu na kukifanya kuwa kingine kabisa..
Hivyo wakati fulani Bwana Yesu aliwatahadharisha mitume wake, wajilinde na chachu, ya hao Mafarisayo na Masadukayo. Mwanzoni walidhani, wajilinde na ile hamira ya kwenye mkate inayotolewa na wao, lakini kumbe sio bali ilikuwa ni mafundisho yao.
Mathayo 16:7 ‘Wakabishana wao kwa wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate.
[8]Naye Yesu akafahamu, akawaambia, Mbona mnabishana ninyi kwa ninyi, enyi wa imani chache, kwa sababu hamna mikate?
[9]Hamjafahamu bado, wala hamkumbuki ile mikate mitano kwa wale elfu tano, na vikapu vingapi mlivyoviokota?
[10]Wala ile mikate saba kwa watu elfu nne, na makanda mangapi mliyoyaokota?
[11]Imekuwaje hamkufahamu ya kuwa si kwa sababu ya mkate naliwaambia? Ila jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.
[12]Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Akiwa na maana gani?
Akiwa na maana kuwa mafundisho yao, wakiyasikiliza kwa nje yanaweza kuonekana hayana madhara yoyote, lakini kwa ndani yana uhai wa kuweza kuupindua wokovu wao ulio wa kweli na kuwafanya wawe wengine kabisa.
Hii ni hatari kubwa, kwasababu siku hizi za mwisho, Mafarisayo na Masadukayo ni manabii na makristo wa uongo, na mafundisho yao yana chachu, ambayo kwa hayo yanawafanya watu waishi Maisha ya uvugu uvugu kama sio ubaridi kabisa, na hivyo wanaukosa uzima wa milele.
Na Bwana amesha tuonya mapema tujihadhari nao.
Mathayo 24:24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.
[25]Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.
Ikiwa upo mahali haugusiwi dhambi, au mafundisho ya utakatifu, bali mafanikio tu ya mwilini, na kutumia mafuta na maji ya upako, kama ndio kigezo cha kukubaliwa na Mungu, fahamu kuwa hiyo ni chachu ya Mafarisayo, ikiwa vimini uvaavyo, rushwa ulazo, uasherati uufanyayo, ulevi, chuki, kutokusamehe , ushirikina, wivu, anasa, hauhubiriwi mahali hapo ulipo, unaambiwa tu pokea gari, pokea nyumba, n.k kimbia haraka, kwasababu hivyo ndivyo vitakavyokupeleka jehanumu.
Biblia inasema, pasipo utakatifu hatuwezi kumwona Mungu (Waebrania 12: 14), Kiini cha ukristo sio kuwa mabilionea hapa ulimwenguni, bali ni kukombolewa na Yesu, na kuishi maisha ya ukamilifu, kujiepusha na hukumu inayokuja.
Hivyo tutawezaje kujilinda nao?
Kwanza ni kwa kumaanisha kumjua Yesu, halikadhalika kupenda kusoma BIBLIA. Ikiwa hatusomi maandiko, utapotea na kudanganywa moja kwa moja. Hivyo chukua tahadhari, penda BIBLIA, kama upendavyo chakula, isome kila siku.
Ikiwa hujaokoka, na utapenda kupata msaada huo wa mwongozo wa kumkaribisha Yesu maishani mwako, basi wasiliana nasi kwa namba zilizopo chini ya somo.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.