JIHADHARI NA MAFUNDISHO YA YEZEBELI
Yezebeli ni nani?
Yezebeli alikuwa ni mwanamke mwenye asili ya nchi ya Lebanoni, mahali pajulikanapo kama Sidoni (1Wafalme 16:31), karibu sana na mji wa Tarshishi, ule ambao Nabii Yona alienda kuhubiri, na alikuwa ni binti wa kifalme, hivyo alitokea katika familia tajiri.
Mwanamke huyu hakuwa Mwisraeli, ila aliolewa na Mfalme wa Israeli aliyeitwa AHABU, ikambidi ahame kutoka katika Taifa lake hilo na kuhamia Israeli, katika mji wa Samaria pamoja na miungu yake, na tamaduni zake.
Mfalme wa Israeli akamfanya kuwa Malkia, jambo ambalo BWANA Mungu alishalikataza kwa kinywa cha mtumishi wake Musa kuwa wana wa Israeli wasioe wanawake wa kimataifa, kwasababu watawageuza mioyo waabudu miungu mingin, Lakini Mfalme Ahabu alifumba macho yake asione hilo, na badala yake akamwoa YEZEBELI.
Yezebeli licha tu ya kulichafua Taifa la Israeli kwa kumshawishi sana Mumewe Ahabu, alikuwa pia ni mchawi (2 Wafalme 9:22). Aliwaua manabii wengi wa kweli wa Mungu, na aliikosesha Israeli kwa sehemu kubwa sana. Mahali pengine Inamtaja Yezebeli kuwa ni Nabii wa Uongo. (Ufunuo 2:20)
Yezebeli pia ndio mwanamke pekee kwenye Biblia nzima aliyekuwa anapaka WANJA usoni na kupamba uso. Desturi za wanawake makahaba.(2 Wafalme 9:30). Mwanamke huyu ndiye Mwanamke pekee aliyeshindana na maagizo ya Mungu kuliko wanawake wote kwenye Biblia, ndiye aliyemsumbua sana Eliya na hata kufikia hatua Nabii Eliya kumkimbia, kuogopa madhara atakayoyapata kutoka kwake.
Na tunasoma katika Agano jipya, tunamuona Bwana Yesu akimtaja huyu mama, na kuliambia kanisa kuwa limemridhia na mafundisho yake ya uongo.
Ufunuo 2:18-22 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana.
[19]Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza.
[20]Lakini nina neno juu yako, ya kwamba WAMRIDHIA YULE MWANAMKE YEZEBELI, YEYE AJIITAYE NABII NA KUWAFUNDISHA WATUMISHI WANGU NA KUWAPOTEZA, ILI WAZINI NA KULA VITU VILIVYOTOLEWA SADAKA KWA SANAMU.
[21]Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake.
[22]Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;
Sasa, huyu Yezebeli tunayemsoma hapa, sio yule yule tunayemsoma kule katika Agano la kale amerudi tena, yule alikufa na damu yake ililambwa na mbwa(2Wafalme9.33-37), na sasa yupo huko kuzimu akiongojea kutupwa katika ziwa la moto. Lakini Yezebeli anayezungumziwa hapa ni utendaji kazi wa ile roho iliyo kuwa ndani yake.
Na moja ya roho iliyo kuwa ndani ya Yezebeli ni roho ya unabii wa uongo, ukiachilia mbali roho ya ukahaba na uchawi.
Na hata sasa, hii roho ya unabii wa uongo ndiyo inafundisha watu wazidi kuabudu sanamu na kumchukiza Mungu kama ilivyofanya kwa wana wa Israeli kipindi cha Ahabu.
Roho ya Yezebeli inawafundisha watu “Kuzini”.. Inawafundishaje?.. si kwa njia nyingine isipokuwa kwa injili ya kwamba “Mungu haangalii mwili anaangalia roho”… Injili hii, inawafanya watu wavae watakavyo..ili lile neno Bwana YESU alilolisema kuwa “amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye nafsini mwake” litimie juu yao kupitia yale mavazi ya kikahaba wavaayo.
Dada/mama fahamu kuwa uvaapo mavazi ya kikahaba kama Yezebeli halafu mwanaume akikutamani tayari umekwisha kuzini naye, hata kama hajakushika mkono. (wewe na yeye wote mmezini, na si yeye tu!.. bali hata na wewe, ambaye hujui kama umetamaniwa kwa mavazi yako). Sasa jiulize unapotembea mtaani umevaa nguo hizo za nusu uchi, umezini na wanaume wangapi!
Hii roho ya Yezebeli ipo makanisani leo!.. ipo kwa wengi wanaotambulika kama watumishi wa Mungu, hii ni roho ya Unabii wa Uongo, inayowafundisha watu UZINZI!, kwa kujua na kutokujua.
Hivyo jihadhari na injili hiyo ya adui, isemayo “Mungu anaangalia roho na haangalii mwili”.. Ulinde mwili wako usiwe chanzo cha kuipoteza roho yako moja kwa moja.
Na tabia ya hii roho ya YEZEBELI ni kushindana na Roho ya kweli ya Mungu.. Ndio maana utaona Malkia Yezebeli katika Uzinzi wake, na uchawi wake na unabii wake wa uongo, hakuwahi kamwe kupatana na Nabii Eliya, wala kujinyenyekeza kwake..zaidi sana utaona Yezebeli baada ya kusikia ishara Eliya aliyoifanya ya kushusha moto na kuwaua manaabii wake wa baali, aliapa kumlipa kisasi Eliya, na wala hakumwogopa hata Mungu. (Ni roho ya kiburi).
Roho hii ikishakita mizizi ndani ya mtu, inamfanya kuwa na kiburi, na mkatili hususani katika watumishi wa kweli wa Mungu, na inakuwa inamfanya mtu kuichukia njia ya kweli na watumishi wa Mungu wa kweli.
Jihadhari na roho ya Yezebeli. Hizi ni siku za mwisho!!
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.