Fahamu maana ya Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake

Maswali ya Biblia No Comments

Shalom, karibu tujifunze Maneno maneno ya Uzima.

 

Mithali 27:18

Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa. “

Kuna Jumbe mbili za muhimu sana katika mstari huu navyo ni

Autunzaye mtini atakula MATUNDA yake, pili ni Amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa.

1. AUTUNZAYE MTINI ATAKULA MATUNDA YAKE 

Injili imeandikwa; si kwenye kitabu pekee Bali hata katika Asili, Ndio maana Bwana Yesu alitumia mifano mingi ( kama vile Wafalme, mabwana,mimea, wakulima, wafanyabiashara n.k) katika hiyo kuzifundisha habari zake mwenyewe.

“..Autunzaye mtini atakula MATUNDA yake..” kumbe kula matunda ni baada ya”kutunza” huwezi kula kama hujatunza yaani kuweka mbolea, kumwagilia, kupiga dawa n.k halafu Sasa Mwisho ndipo unakula matunda.

Angalia, suala hili kiroho linatufunulia hivi… Kila mwamini au aliyeokoka anao mtini ndani yake nao ni Yesu Kristo, Sasa pindi unapompokea Yesu anakuwa mchanga ndani yako, badae kijana na mwishowe mtu mzima hata kuianza kazi yake ndani yako. Kama alivyoishi hapa duniani na wazazi wake, hakuianza kazi yake akiwa mtoto! Kumbe hatuwezi faidi matunda yake ndani yetu bila kumlea vyema.

Tutafakari kidogo kuhusu mfano wa mpanzi

Luka 8:5-7

5“Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda, nyingine zilianguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila.

6 Nyingine zikaanguka penye mwamba; zilipoanza kumea zikakauka kwa kukosa rutuba.

7Nyingine zikaanguka kati ya miiba, na miiba ikamea pamoja nazo ikazisonga.”

 Anaendelea kwa kusema zingine zilizaa thelathini, zingine sitini zingine mia akifafanua kuhusu zilizo zaa kwamba zilitokana na kuvumilia, naam, Kuvumilia hatua ngumu za mwanzo yaani dhiki kwa ajili ya Yesu, kujiepusha na Anasa, Udanganyifu wa Mali, kutendea Neno la Mungu.

Na huo ndio ukuaji wa kiroho yaani Kristo kukua ndani yako. Utalithibitisha hili kwa kuona mtu yupo katika wokovu miaka mingi lakini hatuoni matunda ya wokovu wake katika kuujenga ufalme wa Mbinguni; Tatizo lilianzia hapo “Kushindwa kuutunza mtini wake”

Baada ya kuokoka unapaswa ulijaze neno la Mungu ndani yako, uepuke maisha ya kidunia, Usiwe mvivu wa Maombi na uwe karibu zaidi na Mungu wako, ndipo Umuone Kristo akitenda kazi ndani yako.

2. AMHUDUMIAYE BWANA WAKE ATAHESHIMIWA 

Ni hekima ya kawaida, Mtendakazi Bora kwa bwana wake, huyo hupendezwa nae na humpa heshima hata nyumba ya bwana huyo itampa Heshima yule mjakazi.

JE SI zaidi kwa Mungu wetu?

Heshima inayoongelewa hapa si ya kupiga magoti, kuinamisha kichwa ibadani, kusema shikamoo!! Wala Wala kusema Nakuheshimu! Bali Heshima hupimwa kwa kutii Maagizo yake na kueneza Injili yake kwa Wengine pamoja na kusimama katika nafasi yako kama MTU uliyeokoka.

Basi wapendwa tutafute kuheshimiwa na Bwana wetu Yesu Kristo na kuzishuhudia habari zake njema kwa Wengine.

Ubarikiwe

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *