Fahamu ni jinsi gani unaweza kuvuta uwepo wa Roho Mtakatifu karibu yako,

Maswali ya Biblia No Comments

 

Shalom karibu tujifunze Neno la Mungu..

Leo kwa Neema za Bwana tutaangalia mambo makuu matatu yanayouvuta uwepo wa Roho Mtakatifu karibu yetu

Jambo la kwanza: MAOMBI

Maombi ni jambo la kwanza linalovuta uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu. Tunapokuwa watu wa kuomba mara kwa mara tunamkaribisha Roho Mtakatifu azidi kutusogelea kwa ukaribu na kutusaidia kuomba pamoja nasi (Warumi 8:26) na vile vile anasogea kuzungumza na sisi.

Ukirejea katika biblia utakumbuka kipindi kile Bwana Yesu alipokuwa akibatizwa na Yohana katika mto Yordani utaona Roho Mtakatifu alishuka juu ya Bwana kwa njisi ya HUA (Yaani Njiwa).

Sasa kuna siri moja imejificha katika tukio hilo, ambayo kwa haraka haraka ukisoma unaweza usiigundue. Na siri yenyewe ni MAOMBI!. Utaona baada ya Bwana kutoka majini, na kusogea pembeni utaona alianza KUOMBA!, na wakati akiwa katika maombi, ndipo Mbingu zilipofunguka na Roho Mtakatifu kushuka juu yake, hebu tusome kwa umakini…

Luka 3:21 “Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, NAYE ANAOMBA, mbingu zilifunuka;

22 Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe”.

Umeona hapo? Roho Mtakatifu alimshukia wakati akiwa anaomba, na sio wakati anabatizwa tu peke yake.

Ila pia utaona baada ya Bwana Yesu kupaa mbinguni.. baadaye Roho Mtakatifu alishuka kwa wanafunzi wa Bwana na Mitume wake siku ile ya Pentekoste, biblia inasema Mitume na wanafunzi wengine walikuwa wamekusanyika mahali Pamoja katika ghorofa wakidumu katika kusali, na huko huko wakiwa katika kuomba ndipo Roho Mtakatifu akashuka juu yao na kuwajaza nguvu (Soma Matendo 1:13-14, Matendo 2:1-2).

Hata ukiangalia sehemu nyingine nyingi, utona kuwa Roho Mtakatifu alishuka wakati watu wakiwa kwenye maombi.. soma Matendo 4:31

Matendo 4:31 “Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri”.

Vivyo hivyo na sisi tukitaka kuuvuta uwepo wa Roho Mtakatifu karibu yetu kiasi cha kumhisi kuwa yupo ndani yetu, yupo katikati yetu basi hatuna budi kudumu kwenye MAOMBI, vile vilevile tukitaka tumsikie anataka nini kwetu au anasema nini, njia pekee ni Maombi!

Sasa pengine yaweza kuwa hujui namna ya kuomba na unatamani kujua, ni rahisi sana..iwapo utatamani kupata mwongozo wa namna ya kuomba basi tutumie ujumbe inbox, ili tuweze kukutumia somo linalohusu “Njia bora ya kuomba”

Jambo la pili:KUSOMA NENO.

Hii ni moja ya njia nyingine iliyo ya muhimu ya kuuvuta uwepo wa Roho Mtakatifu karibu nasi. Na kazi mojawapo ya Roho Mtakatifu ni kutuongoza na kututia katika Kweli yote (Yohana 6:13-14), na Kweli ni Neno la Mungu (Yohana 17:17). Hivyo tunapotenga muda wa kuishika biblia na kuisoma kwa lengo la kujifunza, basi Roho Mtakatifu anasogea karibu nasi sana. Ni lazima atusogelee kwasababu ndio kazi yake yeye kutufundisha na kutufunulia maandiko.

Hebu tujifunze kwa yule Mkushi aliyekuwa anarudi nchini kwao, ambapo njiani alijikuta anafungua kitabu cha Isaya 53, kilichokuwa kinazungumzia Habari za Masihi, (Yesu) lakini hakuwa na ufunuo wowote juu ya hilo, Ndipo Roho Mtakatifu akaingia kazini kujisogeza karibu naye ili amtie katika kweli yote!!..

Roho Mtakatifu akaanza kuzungumza kwanza na Filipo siku kadhaa kabla hata ya Mkushi huyo kufikiria kusoma hilo andiko, Roho Mtakatifu akaanza kutengeneza njia ya kumkaribia Mkushi huyo, ndipo alipowaambia Filipo ashuke kuelekea njia ya jangwa, na alipokutana na yule Mkushi yupo matatani haelewi maandiko, ndipo Roho Mtakatifu akaanza kuzungumza kupitia kinywa cha Filipo. Na hatimaye kumfunua macho yake na kumtia katika kweli yote.

Matendo 8:29 “Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.

30 Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?

31 Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.

32 Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.

33 Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.

34 Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?

35 Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.

36 Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji, yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

37 [Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]

38 Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza.

39 Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.”

Yule Roho aliyemsaidia yule towashi,(Roho wa Yesu) hajawahi kubadilika..tabia zake ni zile zile, tukitaka atukaribie na kutusaidia, tumwone na tumsikie akisema nasi, basi hatuna budi kuwa wasomaji wa Neno la Mungu. Penda kujifunza biblia kwa kina kwa kutafakari…utauvuta Roho Mtakatifu karibu yako..na hatimaye utaanza kumsikia akikufunulia maandiko.

Jambo la tatu: KUHUBIRI/KUSHUHUDIA.

Tunajua agizo kuu ambalo tumeachiwa na Bwana Yesu ni kufikisha injili duniani (ulimwenguni) kote..

Marko 16:15 “akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.

16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini, atahukumiwa.”

Unapomhubiri Kristo au Kushuhudia habari zake kwa watu wa aina zote ili kuwafanya wamjue na wamwamini na kumpokea.. wakati unachukua hilo jukumu..Roho Mtakatifu anakuja ndani yako ili akusaidie kuhubiri kwa hao watu unaowashudia au unaowahubiria, kwani maneno yako tu mwenyewe hayawezi kugusa mioyo ya watu na kuwafanya wamgeukie Kristo..

Roho Mtakatifu hana budi awe pamoja na kinywa chako pale unapohubiri au unaposhudia..na hii Ndiyo sababu ni muhimu kumhubiri Kristo mahali popote pasipo kujalisha ni watu gani unaohubiria..we shuhudia tu habari za Yesu pasipo kufikiri fikiri kwamba watakuelewa au hawatakuelewa..

jambo la wewe kueleweka si lako bali Roho Mtakatifu atakusaidia kusema na kuugua ndani ya huyo mtu au hao watu unaowahubiria..we kuwa tu tayari kuhubiri/kushuhudia habari za wokovu wa Yesu Kristo mahali popote ulipo iwe ni kazini, njiani, nyumbani n.k na kwa kufanya hivyo utauvuta Roho Mtakatifu ndani yako na hatimaye utakuwa karibu na Mungu sana..

Mathayo 10:18 “nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.

19 Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayoyasema.

20 KWA KUWA SI NINYI MSEMAO, BALI NI ROHO WA BABA YENU ASEMAYE NDANI YENU.”

Kwahiyo kama wakati wote tutakuwa kwenye hayo mazingira ya ushuhudiaji, basi vinywa vyetu wakati wote itatawaliwa na Roho Mtakatifu, na hivyo uwepo wake utakuwa karibu nasi muda wote. Kinyume chake kama hatutajishuglisha na injili, kama hatutafunua vivywa vyetu kumhubiri Kristo itakuwa ni vigumu Roho Mtakatifu akae ndani yetu kwa wakati wote.

Je! Na wewe leo umefanyika mwana wa Mungu (umeokoka)?

Kama umempokea Bwana Yesu na ukafanyika mwana wa Mungu sawa sawa na (Yohana 1:12) je! wewe ni MWOMBAJI?… wewe NI MSOMAJI WA NENO LA MUNGU?… wewe MSHUHUDIAJI? Kama hufanyi hayo basi usitegemee kusikia wala kuhisi uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yako,

Wakristo wengi wamempa shetani nafasi ya kuwazuilia wasiuvute uwepo wa Roho Mtakatifu karibu yao.. utakuta mkristo hajawahi kutenga hata lisaa limoja kuomba kama yeye binafsi,..ni kusikiliza na kusoma tu mahubiri!. Na kuombewa, lakini kuomba mwenyewe hataki, utamkuta mkristo hana utaratibu wa kutenga muda maalumu wa kusoma na kujifunza biblia, yeye ni kusubiri tu jumapili ndiyo atafungua biblia yake..

Ni wiki nzima ameweka tu ndani, ndio huyo ukimwambia hiyo biblia ina vitabu vingapi hajui!. akiambiwa afungue kitabu fulani labda Sefania, hata hajui Kuna kitabu kama hicho, atatumia zaidi ya dakika 10 Kufungua..hadi akatafute kwenye orodha, hiyo ni kuonyesha kuwa hajalipa Neno la Mungu uzito zaidi kwenye maisha yake, na anategemea kusikia sauti ya Mungu, anategemea kujazwa Roho Mtakatifu,..

Leo hii ukimwuliza mkristo mara ya mwisho kushuhudia habari za Yesu kwa mwingine hata hakumbuki, lakini shuhuda za wachezaji maarufu, wanamziki wakubwa, filamu mpya zilizotoka, ndio zimejaa katika kinywa chake!.

Kumbuka Bwana anatutamani hadi kutuonea wivu..anatamani awe karibu yetu, atembee nasi, aongee nasi tumsikie, kuliko sisi tunavyomtamani (Yakobo 4:5) hivyo ni wajibu wetu kuongeza bidii katika kuomba, kusoma Neno, kushuhudia, pamoja na kuishi maisha matakatifu kwa kujitenga na kawaida za dunia,

“BWANA YESU ANARUDI”

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *