Fahamu umuhimu wa Yesu maishani mwetu.

Maswali ya Biblia No Comments

Jina la Bwana Wetu Yesu Kristo lizidi kutukuzwa milele, karibu tujifunze Neno la Mungu,

Hili ni jambo la muhimu na kuu kulijua sana wewe ambaye ni mwanadamu na unavuta pumzi ambayo hatutoi malipo yoyote au kuigharamia kwa chochote, Jambo la kumfahamu Yesu Kristo ni la umuhimu kwetu kwasababu yeye ndiye chanzo cha ukombozi wetu, kuishi kwetu ni yeye, tusipojishuhulisha kuijua Neema ya Bwana Yesu aliyoileta ulimwenguni tutajikuta tunaangamia pasipo maarifa,

Wafilipi 1:21

[21]Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.

Maisha yako yote chanzo chake ni Yesu Kristo, hakuna namna hutaweza kuepuka hili, kwa kuwa kila msingi wa Mwanadamu yoyote unajengwa na Bwana, hivyo tuna sababu za kumjua yeye sana, na hatutafuti kumjua kwa jinsi alivyo sura yake,au mwonekano wake jinsi ulivyokuwa, hapana, bali tunamfahamu Yesu kwa ile nafasi aliyonayo yeye,ukifika kuijua nafasi ya Yesu na jinsi anavyotenda kazi utamfurahia Mungu sana na kuzidi kumjua kila wakati,

Kuna sehemu maandiko yanasema Hakuna Mwanadamu aliyeona uso wa Mungu akaishi, akimaanisha, hakuna aliyefikia kujua ile nafasi ya Yesu Kristo katika utimilifu wote, bali tunafahamu kwa sehemu na kadiri tunavyozidi kupiga hatua zaidi ndivyo tunavyozidi kumjua Mungu, na hiyo inatupelekea tuzidi kuuona uzuri wa Bwana Yesu,na ndivyo tunavyozidi kumpenda, kumtukuza,kumsifu na kumuheshimu zaidi..

Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo”

Ikiwa wewe umepata Neema ya kuwepo duniani unasababu kila wakati za kutafakari msalaba wa Yesu, jinsi kifo chake kilivyo na umuhimu mkubwa sana tangu tulipokuwa wenye dhambi, watu ambao hatukufaa kitu mbele za Mungu, ndo mana tunaona kabla ajaenda kusulubiwa Yesu, utawala wa kipindi hicho ulikuwa ni Rumi kupitia kiongozi wao Pontio Pilato, ili kuwapendeza watu na kwasababu makutano walitaka hivyo, ni kama ilipigwa kura nani afunguliwe kati ya Yesu au Baraba ambaye alikuwa muuaji na katili, lakini wote wakapiga kelele afunguliwe BARABA

Na huyu baraba sio kwamba alikuwa na makosa madogomadogo, maandiko yamemtaja kama mfungwa mashuhuri, mkatili mji mzima, alishuhudiwa na kila mmoja kwa ukatili wake na warumi walimfunga kwenye magereza akisubiri siku ya kuhukumiwa,na mtu kama huyu adhabu yake ni lazima itakuwa kubwa na kali, na watu ndivyo walivyokuwa wakifikiri.

hivyo,yani anastahili adhabu kubwa,na hakukuwa na mtu aliyekuwa na imani kuwa baraba anaweza kupona au kufunguliwa, kumbe hawakumjua Mungu ambaye anatengeza njia pale ambapo hapana njia, anafanya mambo ambayo Mwanadamu ameshindwa kabisa..

Kibinadamu hata baraba alijua tumaini lake la Kutoka gerezani limepotea,halipo tena,alijijua yeye ni wakufa tu, na pengine aliwaona wale wenye makosa madogo tu jinsi walivyotendewa, pengine waliuwa, walinyongwa kikatili, akajua na yeye atatendewa zaidi ya hayo, lakini gafla ulifika wakati fulani anasikia sauti ikimwambia atoke gerezani,yuko huru, si ajabu alipatwa na  mshangao mkubwa, akiwa nje anakutana na kundi kubwa,likiwa kwenye shangwe na furaha likimshangailia yeye kutolewa kwenye gereza, likipiga kelele, baraba afunguliwe, afunguliwe!

Akiwa tena bado kwenye mshangao zaidi anamuona aliyeruhusu apelekwe kwenye magereza anamtangazia kwamba yupo huru kujumuika na familia yake na kuendelea na maisha yake, na wakati huo huo ,Bwana, Yesu yupo karibu, pembeni yao akitazama kinachoendelea huku taji ya miiba ipo kichwani, mfano wa Mwanakondoo aendaye machinjioni, taarifa inatoka kwa Pilato inamjulisha baraba unayemwona hapo amekubali kufa kwa ajili yako na amechukua hukumu yako uliyokuwa umepangiwa ufe nayo, si ajabu baraba aliendelea kubaki na mshangao,

Katika hali ya kawaida,kuishi kwake baraba kuanzia wakati huo kulianza kubadilika,hakuishi tena yale maisha aliyokuwa akiyaishi,alifahamu uzima wake,kuishi kwake tena ni kwasababu kuna mmoja Yesu alikubali kujitoa kwa ajili yake, alifahamu uzima wangu upo Kwa Bwana Yesu alikataliwa ili mimi niwe huru, uhuru wangu unatokana na yeye,ilimpa kujua kama Yesu asingekataliwa basi na habari yake ingeisha kabisa

Sasa mtu wa namna hii atakuwa na ujasiri gani,wa kurudia yale mambo maovu aliyokuwa akiyatenda, atapata wapi nguvu za kwenda kuiba na kudhulumu, atapata wapi nguvu za kumdharau Yesu wa msalaba tena, lazima atakuwa anafahamu nikitoka nje ya njia lazima yapo mabaya zaidi yakayompata zaidi ya yale aliyoyatarajia..

Ni wakati wa kujitathmini sana, mfano wa baraba ni wewe na mimi ndugu, Bwana Yesu alikubali kuchukua dhambi zetu na maovu si kuyaweka begani, hapana, mateso aliyoyapitia Bwana kwa ajili yangu na wewe ni makubwa sana,hayachukuliki, alipigwa sana, uso wake uliharibiwa kweli Kweli, walimtemea mate, wakamdhihaki, na mwisho wakamsulibisha akiwa mtupu bila nguo, kusudi mimi na wewe tuwe huru kama Baraba alivyowekwa huru, Bwana alikubali yeye ashuke lakini sisi tupande juu, alikubali yeye akataliwe ili sisi tupate kibali..

Kwanini usiuthamini msalaba wa Yesu Kristo Mwokozi Wetu, kwanini unaichezea hii Neema unayoiyona leo, Kumbuka haya yote tunayoyaona tunayapata katika huu ulimwengu, fahamu ni kwasababu ya kifo cha Yesu, bila hivyo hata duniani tusingekuwepo kabisa, tungeshaangamizwa na ghadhabu ya Mungu, hii dunia isingekuwepo kabisa na kusingekuwa na haya maisha unayoyanona na kuyafurahia..

1 Wakorintho 1:18

[18]Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.

Leo hii unaendelea kufanya dhambi, unazini na kila mwanamke au mwanaume, umekuwa mwizi, mtukanaji,unavaa nguo zilizo utupu, unazidi kutenda maovu, lakini bado upo unaendelea na maisha yako, elewa ndugu ni kwasababu ya kile kifo cha Bwana alichokufa miaka 2000 iliyopita, kama si Bwana kukubali kuteseka vile hakuna mwenye dhambi angeishi wote ilikuwa ni watu wa kufa na kupotea kabisa,

Mathayo 5:45

[45]ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

Jua kuna siku itafika Neema hii ya Yesu unayoidharau na kuichezea itaondoka, hapo ndipo Yesu atawachukua watu Wake, watakatifu waliojua kuitumia Neema kwa tendo la unyakuo,watanyakuliwa , hapo ndipo hasira ya Bwana itawaka kwa wale wote watakaobaki Katika ulimwengu, mapigo yatakayokuwepo usifikirie kubaki kabisa, majipu mabaya yatazuka kwa wanadamu,maji kugeuzwa damu, wakati huo utatamani utubu na kugeuka lakini utakuwa umechelewa..

Sasahivi unayafurahia na kuyapenda haya maisha lakini siku ya hasira ya Bwana ikifika utatamani ufe kwasababu  maandiko yanasema wanadamu watatami kufa lakini kifo kitawakimbia, yani hakitakuwepo kabisa, mambo yatakayotokea ni ya kutisha, matetemeko makubwa, jua litatiwa giza,jua litawaunguza wanadamu kwa mateso makali, jiulize ndugu upo tayari uyapite haya?

Habari njema ni kuwa unayo nafasi ya kutengeneza sasa, ni wakati wako wa kutubu, yaani kugeuka Katika njia zako zote mbaya kwa kumaanisha kabisa kumfata Bwana Yesu na kisha ubatizwe ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu, utapokea Roho Mtakatifu atakayekuongoza Katika njia zako zote na kukupa uthibitisho kuwa wewe ni Mwana wa Mungu,

Unasubiri nini?

Shalom,Maran atha…

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *