Ili ubarikiwe hakikisha unatoa sadaka yako mahali sahihi,

Maswali ya Biblia No Comments

 

Shalom: Jina la Bwana Yesu Kristo Mkuu wa Uzima libarikiwe;

Karibu katika darasa fupi tujifunze baadhi ya mambo ambayo yanapuuziwa na kuchukuliwa kirahisi na Watu wengi ila ni mambo makuu sana katika kukuza Imani..japokuwa yanaonekana ni madogo.

Ipo tofauti kati ya sadaka na msaada. Wakati ambao unajitoa kuwasaidia wasiojiweza hapo unatoa msaada, na Mungu atakubariki, ila matokeo ya kutoa sadaka ni makubwa zaidi ya kutoa msaada.

Sasa swali: Nini maana ya sadaka??

Matoleo yoyote yanayohusisha madhabahu huitwa Sadaka!. Tukirudi katika agano la kale sadaka ambayo Mungu aliikubali ni ile ambayo Wana wa Israeli walipeleka madhabahuni ndani ya hema au nyumba ya BWANA, Sadaka zote kama ya kutoa kafara ya wanyama, au mazao ya shambani, au kitu chochote zilipelekwa madhabahuni pa BWANA ndani ya hema ya kukutania au Hekaluni.

Kama unatoa Sadaka usitoe kwa maskini kama Sadaka bali kama msaada, maana ukipeleka sadaka yako kwa watu wenye uhitaji itahesabiwa umetoa msaada na sio Sadaka, na haimanishi hautabarikiwa, la hasha! Mungu hataacha kukubariki kwa vile ulivyowatolea wenye uhitaji, tofauti tu ni kwamba haitakuwa kama ungetoa kama Sadaka, unapotoa Sadaka huna budi kupeleka madhabahuni pa Mungu aliye hai.

Ukiangalia hata watu ambao wanaenda kutafuta misaada kwa waganga na kwa mashetani ni lazima wapewe masharti ya kwenda na sadaka..Na wakishapeleka hiyo sadaka hawatupii tu mahali popote bali wana madhabahu yao ndiyo wanaiweka, kusudi wapate matokeo ya wanachokihitaji, mtu hawezi kwenda Kwa mganga halafu akapewa maagizo kwamba aende nyumbani achukue kuku wa rangi fulani kisha amchinjie hapo hapo nyumbani, hapana!. Ni lazima apeleke huko kwa mganga akamchinjie hapo hapo, na si kunjichia nyumbani kisha na kuwapa maskini au kupeleka kwa mganga mwingine!. Hicho kitu hakipo, ni lazima tu atakuambia njoo nayo hapa kwangu (kwenye hiyo madhabahu) iwe ni chochote kulingana na masharti yake, hilo ni Kwasababu ili sadaka iitwe sadaka ni lazima kuwepo na madhabahu husika,

Hivyo tunaweza kusema sadaka isiyohusisha madhabahu siyo sadaka.

Tusikie maneno ya Bwana Yesu Katika…

Mathayo 23:18 “Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga”.

Hapo Bwana Yesu anatupa picha halisi kuwa kuna ushirika kati ya sadaka na madhabahu.

Hivyo ikiwa wewe ni mkristo sadaka zako unatakiwa kupeleka kanisani au sehemu ambayo inakulisha kiroho.. labda kwenye mikutano ya Neno la Mungu, kwenye semina ya Neno la Mungu, n.k, ukifanya hivyo utabarikiwa zaidi, ila usiache pia kutoa misaada kwa watu mbalimbali wenye uhitaji maana huko nako kuna thawabu kubwa Mungu atakupa. Lakini fahamu tu kuwa sadaka ina nguvu mara nyingi kushinda kutoa tu msaada, Iwapo utapata kuelewa zaidi ufunuo huo!.. Jitahidi sana kutoa sadaka kuliko kutoa michango yako mahali pengine.

Shetani amesambaza mawazo mabaya sana ndani ya bongo za watu wengi, na hiyo imewapelekea watu wengi kutopokea baraka walizostahili, Na mawazo yenyewe ni kuwa ukienda kutoa sadaka yako kanisani ni kuwanufaisha wale watumishi wanaohudumu hapo, Kwahiyo ni bora kupelekea wanye uhitaji, Hayo ni mawazo ya adui ibilisi usiyakubali kabisa yakukoseshe baraka zako kutoka Kwa Mungu.

Ila pia sehemu nyingine Bwana Yesu alihubiri akisema…

Mathayo 5:23 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,

24  iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako”.

Haya ni Mambo ambayo hayazingatiwi..yanapuuziwa kana kwamba ni mambo madogo sana, ndio ni mambo madogo kwa uelewa wetu ila yana umuhimu mkubwa sana Katika utoaji wetu, Hivyo hatuna budi kuyafahamu na kuyachukulia maanani. Utoapo fungu la kumi peleka madhabahuni pa Mungu, na sadaka zako zote iwe ni shukurani, ipeleke nyumbani kwa Bwana.

Shalom..

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *