Bwana Yesu asifiwe, karibu tujifunze maneno ya Mungu.
Tunaweza kujiuliza kuna tofauti gani kati ya ubatizo wa Yohana na ubatizo wa Bwana Yesu lakini ukweli ni kwamba hakuna tofauti yoyote maana ubatizo ni ule ule mmoja wa toba,tofauti inayotokea ni matumizi ya jina la Yesu.
Hata kabla Bwana Yesu hajaja duniani watu walikuwa wanasali, wanafanya maombezi na mambo mengine mengi ya kimungu lakini hawakutumia jina la Yesu kwa sababu Mungu hakuwa amewaruhusu kufanya hivyo.
Hata Yohana alipokuja na ufunuo wa ubatizo, aliwabatiza watu bila kutumia jina lolote. Watu walipotubu na kuwa na nia ya dhati ya kuacha dhambi zao basi walizamishwa katika maji na kuibuka juu ishara ya kuonyesha wametakasika lakini Yohana aliwabatiza bila kutaja jina lolote.
Baada ya Bwana Yesu kuja utaratibu ukabadilika jambo lolote lililohusu huduma ya Mungu lilifanyika kwa jina lake.
Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, KWA NENO AU KWA TENDO, FANYENI YOTE KATIKA JINA LA BWANA YESU, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”.
Hivyo baada ya agizo hilo wanafunzi wa Yesu na mitume walianza kulitumia jina la Yesu katika huduma zote zilizohusu wokovu walizozifanya kwa NENO au kwa MATENDO.
Katika maneno ambayo walitumia jina la Yesu ni wakati walipokuwa wanasali na kuhubiri. Tunaona walipokuwa wakitoa pepo au kuombea wagonjwa walitumia jina la Yesu.
Luka 16:17 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; KWA JINA LANGU watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya”.
Lakini pia wakati wanahubiri na kuwafundisha watu habari za wokovu walifundisha kwa jina la Yesu.
Luka 24:46 “Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu;
47 na kwamba mataifa yote watahubiriwa KWA JINA LAKE habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu”.
Hapo tumeona walitumia jina la Yesu kwa maneno, na hawakuishia hapo walifanya hivyo katika matendo pia kwa mfano tendo la ubatizo. Yohana aliwabatiza watu lakini hata wanafunzi wa Yesu walibatiza pia kwa sababu Yohana aliwafundisha kufanya hivyo.
Andrea kabla hajawa mwanafunzi wa Yesu alikuwa wanafunzi wa Yohana na aliujua ubatizo na yeye alibatiza pia kabla ya ujio wa Bwana Yesu. Baada ya ujio wa Bwana Yesu wanafunzi walianza kutumia jina la Yesu katika mambo yote, hata walipobatiza walitumia jina la Yesu hawakubatiza kama alivyofanya Yohana kwa kuzamisha bila kutaja jina lolote.
Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
38 Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”.
Unaona hapo? Kumbe ili ubatizo uwe na matokeo ni lazima kutumia jina la Yesu. Mtume Paulo alipokuwa Efeso alikutana na watu ambao walikuwa wameshabatizwa na Yohana lakini aliwaambia wabatizwe upya kwa jina la Yesu.
Matendo 19:1 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko;
2 akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.
3 AKAWAULIZA, BASI MLIBATIZWA KWA UBATIZO GANI? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.
4 Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu
5 WALIPOSIKIA HAYA WAKABATIZWA KWA JINA LA BWANA YESU.
6 Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.”
Mpendwa unayesoma ujumbe huu fahamu kuwa ubatizo sahihi ni ule unaotumia jina la Yesu, ikiwa hutapata ubatizo sahihi na kweli yote unaijua basi moja kwa moja utakuwa umemkataa Mungu. Tena kuna madhara ya kutopata ubatizo sahihi, kumbuka jambo hili siku zote.
Tupo katika nyakati za mwisho kama bado hujamwamnini Kristo tengeneza maisha yako sasa kabla nyakati mbaya hazijawadia.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.