
JE! BABA ALIYE MBINGUNI HATAZIDI SANA KUWAPA ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO?
Je! unaweka jitihada zako kumwomba Mungu nini?
Shalom! Mwana/binti wa Mungu, karibu tuyachunguze maandiko, natumai leo utajifunza jambo jipya litakalotusaidia katika maisha yako ya maombi.
Ikiwa maombi yako yameegemea sana mahitaji ya mwilini, mfano chakula, kazi, fedha, ndoa, elimu, n.k zaidi ya mambo ya rohoni kama upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, kiasi n.k ambayo ni tunda la Roho Mtakatifu, basi leo anza kubadilisha mtazamo wako katika kumwomba Mungu.
Haimaanishi tusimuombe Mungu mahitaji ya mwilini kabisa! hapana, lakini hatupaswi kutumia nguvu nyingi sana kuomba mambo hayo maana ni haki yetu kupewa na Mungu ikiwa tu watoto wake.
Hauhitaji kufunga na kuomba ili Mungu akupe chakula au mavazi, hauhitaji kukesha kumuomba Mungu akupe fedha. Ni jambo la kwenda mbele za Mungu na kumweleza haja zako zote na ikiwa ni mapenzi yake atakupa papo hapo au baadaye aonavyo yeye, unahitaji tu kuwa mvumilivu.
Lakini unahitaji kufunga na kuomba ili Mungu akujaze Roho wake Mtakatifu, unahitaji kukesha na kumuomba Mungu akupe hatua nyingine ya kiroho.
Hebu tusome maandiko yafuatayo ili tuelewe vizuri jambo linalomgusa moyo wa Mungu katika kuomba kwetu.
Luka 11:9 “Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
[10]Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
[11]Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?
[12]Au akimwomba yai, atampa nge?[13]Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, JE! BABA ALIYE MBINGUNI HATAZIDI SANA KUWAPA ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO?
Hapo mstari wa mwisho anasema kama sisi tulio waovu tunawapa watoto wetu vipawa vyema, kama chakula kizuri, nguo nzuri, shule nzuri, n.k je! si zaidi Baba yetu aliye mbinguni HATAZIDI SANA KUWAPA ROHO MTAKATIFU hao wamwombao.
Maana yake Baba yetu hatoi tu hayo mahitaji ya mwilini ambao watu wa dunia hii wanatoa kwa watoto wao, lakini yeye anatoa zaidi ya mahitaji. Na kipawa kikubwa anachotoa Mungu kwa watoto wake ni ROHO MTAKATIFU na wala sio nyumba nzuri, sio gorofa wala sio magari. Kwasababu itatufaidia nini tukipata hayo yote halafu tukakosa amani, furaha, upendo, uvumilivu, utu wema, utakatifu na kisha uzima wa milele.
Hivyo Bwana YESU hapo anatuambia Baba yetu aliye mbinguni hatazidi kutupa Roho Mtakatifu tukiomba, na sio hatazidi kutupa mali tukiomba. (Kumbuka ni mapenzi ya Mungu tuwe na maisha mazuri, tuwe na nyuma nzuri na mafanikio lakini zaidi anapendezwa tukimuomba atujaze Roho Mtakatifu zaidi ya hayo mahitaji, kwasababu hata tusipomuomba anajua tunahaja nazo na hivyo si kazi yeye kutufanikisha)
Luka 10: 5 Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu,
6 kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake;
7 na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?
8 Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.
9 Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
10 Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
11 Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?
12 Au akimwomba yai, atampa nge?
13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni HATAZIDI SANA KUWAPA ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO?.
Unaona hapo? HATAZIDI SANA KUWAPA ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO?.Kwanini hakusema MALI,au AFYA, bali Roho Mtakatifu?..
Ndugu kumbuka hii dunia isingekuwa hivi ilivyo kama Roho wa Mungu asingetua juu yake na kufanya uumbaji upya..Hata mtu yeyote anayesema amemwamini Yesu, hakumwamini hivi hivi kama hakuvutwa na Roho wa Mungu kwake (Yohana 6:44).. Hata leo hii anayesema amesimama, au anamtumikia Mungu, hafanyi hayo yote kama sio Roho wa Mungu amekufanya uwe hivyo. Roho wa Mungu ndio kila kitu kwenye maisha yetu..Ndio muhuri wa Mungu (waefeso 4:30), na ndio maana biblia inasema wale wote wasio na Roho wa Mungu hao sio wake (Warumi 8:9)..haijalishi utakuwa mwema kiasi gani…
Roho Mtakatifu ni karama ya bure kabisa, mtu anampokea pale tu anapoitii sauti yake na kumkaribisha ndani yake..Hii inakuja pale mtu anapokusudia kabisa kwa weupe wa moyo wake kutoka moyoni KUTUBU dhambi zake na kuacha maisha yake ya kale, kisha akaenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zake kulingana na (Matendo 2:38). Basi kuanzia hapo mtu wa namna hiyo anakuwa ametiwa muhuri na Mungu kwa Roho wake mtakatifu..Lakini hiyo peke yake haitoshi,.Kumwamini tu, bila ya kumtamani ROHO MTAKATIFU katika maisha yako, hutafika mahali popote…Wengi wameishia hapo na ndio mwisho wa siku Roho Mtakatifu amezimika ndani yao.
Pindi tu unapompokea BWANA kuanzia huo wakati na kuendelea ni jukumu lako kumtamani Roho Mtakatifu awe pamoja nawe. Na ndio hapo linakuja hilo ombi kuu la Bwana, Akupe Roho mtakatifu, au kwa lugha rahisi tunaweza kusema AKUJAZE Roho Mtakatifu…Ulikuwa katika kipimo cha chini lakini sasa unataka AKUJAZE mpaka kwenye kipimo cha juu kabisa. Kumbuka Roho Mtakatifu sio kunena kwa lugha, ni jambo lingine, Na kwa jinsi utakavyozidi kuendelea kuomba bila kukata tamaa, basi ujue ndivyo unavyojijengea daraja zuri la Mungu kuyatawala maisha yako yote, na kuruhusu madarasa Fulani upitie kwa kukuandaa kwa kazi yake teule ya utumishi mwema..Kama tunavyoona ilivyokuwa kwa Yohana mbatizaji, ilivyokuwa kwa Bwana Yesu na ilivyokuwa kwa mitume wake..Wote walipokea Ujazo wa Roho Mtakatifu,lakini hiyo ilikuja kwa jinsi walivyotamani kipawa hicho tunaona baadaye walikuja kuvipokea, Roho mtakatifu aliposhuka juu yao na kuwatia mafuta ya utumishi, ndipo hapo Mungu alitembea nao kwa namna ya kipekee sana.
Hivyo ni maombi yangu, mimi na wewe kila siku na sisi tusikate tamaa kuomba Roho Mtakatifu zaidi ya mambo ya kimwili.
Waefeso 5:17 “Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.18Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; BALI MJAZWE ROHO;”
Ubarikiwe sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.