Shalom…
Swali:
Naomba kuuliza, je ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena, tunaotakiwa kuwa nao ni wa Roho mtakatifu peke yake ambao Yohana mbatizaji aliuzungumzia katika Mathayo 3:11?
“Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto”?
Jibu:
Tukiangalia katika hiyo mistari Yohana hajasema watu waache ubatizo wa maji na kufuata wa Roho Mtakatifu peke yake. Dhana hii inatokana na baadhi ya walimu ambao hufasiri neno la Mungu vibaya bila kuongozwa na Roho Mtakatifu
Bibilia imemtaja mtu mmoja ambaye alielewa hilo andiko na akaamua kuchukua hatua kuwaelekeza watu wengine wapate kuijua njia ya kweli.
Katika kitabu cha Matendo sura ya 10 tunamuona mtu mmoja alijulikana kwa jina la Kornelio, mtu huyu alikuwa akimcha Mungu kumtolea sadaka zake na siku moja malaika alimtokea na kumwambia amuite Petro ili amwelekeze nini cha kufanya. Petro alipopewa taarifa alienda na kisha alianza kuwaambia habari za Yesu, punde tu Petro alipoanza kuongea Roho Mtakatifu alishuka mahali hapo na watu wakajazwa nguvu za Roho Mtakatifu na kuanza kunena kwa lugha..
Matendo 10:44 “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.
45 Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.
46 Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,
47 Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?
48 Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha.
Petro aliona watu wamejazwa na Roho Mtakatifu lakini hakusema kuwa inatosha watu hawahitaji tena ubatizo kwa sababu Yohana alisema hivyo, Petro alilifahamu hilo andiko hata wakati anawahubiri watu alilikumbuka. Wakati amerudi Yerusalemu aliwasimulia wayahudi jinsi watu wa mataifa walivyopokea nguvu za Roho Mtakatifu kama wao tena aliwaambia kuhusu lile andiko la Yohana.
Matendo 11:15 “Ikawa nilipoanza kunena Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo.
16 Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, YOHANA ALIBATIZA KWA MAJI KWELI, BALI NINYI MTABATIZWA KWA ROHO MTAKATIFU.
17 Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu?.
Tunaona hapo Petro alilielewa andiko kuwa hatutakiwi kuucha ubatizo wa maji na hii ndiyo sababu hata watu walipojazwa nguvu za Roho Mtakatifu bado aliwaagiza wakabatizwe. Hata sisi hatutakiwi kuliacha hili agizo kwa sababu ni muhimu kwa kila anayemwamini Bwana Yesu, Maandiko yanasema, ‘aaminiye na kubatizwa, ataokoka, asiyeamini atahukumiwa’ (Marko 16:16)
Tena tukumbuke kuwa ubatizo sahihi ni ule wa kuzamishwa katika maji mengi (Yohana 3:23)na kwa jina la Yesu(Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5)kama umebatizwa ubatizo tofauti na huu basi unapaswa kubatizwa tena…
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.