Fahamu umuhimu wa Ubatizo,

Maswali ya Biblia No Comments

 

Bwana Yesu asifiwe,

Karibu tujifunze maneno ya Mungu na kukumbushana mambo mbalimbali ambayo pengine tulishawahi kujifunza kabla.

Leo tutaona umuhimu wa ubatizo. Ni muhimu sana mtu kupata ubatizo na shetani anajua siri iliyopo katika ubatizo na hivyo amekuwa akizuia watu wengi wasiijue.

Wana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri, tunaona farao na majeshi yake walikuwa bado wakiwafuata nyuma. Baada ya Israel kuvuka bahari ya shamu Farao na majeshi yake walizama ndani ya bahari na huo ndio ukawa mwisho wao wa kuwafuata wana wa Israeli.

Kutoka 14:26 “Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao.

27 Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na Bwana akawakukutia mbali hao Wamisri kati ya bahari.

28 Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja.

29 Lakini wana wa Israeli wakaenda katika nchi kavu katikati ya bahari; na hayo maji yalikuwa ni kuta upande wao wa kuume, na upande wao wa kushoto.

30 Ndivyo Bwana alivyowaokoa Israeli siku ile mikononi mwa Wamisri; Waisraeli wakawaona Wamisri ufuoni kwa bahari, wamekufa

Tunaweza kujiuliza kuna siri gani hadi mwisho wa Farao ulikuwa kwenye bahari ya shamu? Bila shaka ni huo ubatizo wa wana wa Israeli waliobatizwa kwa kupita katikati ya maji ya bahari ya shamu.

Unaweza kujiuliza, kumbe wana wa Israeli walibatizwa katikati ya bahari ya shamu? Ndio Israeli walibatizwa katikati ya bahari ya shamu.

1Wakorintho 10:1 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;

2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;”

Kumbe wana wa Israeli walipopitishwa katikati ya maji ya bahari ya shamu na kutoka salama jambo hili linafananishwa na ubatizo. Na huo ubatizo ndio uliomaliza kazi ya adui na majeshi yake asipate kuwafuata tena.

Hata sasa ubatizo sahihi wa maji mengi hufanya kazi hiyohiyo, kitendo cha kuzamishwa ndani ya maji kwa kutumia jina la Yesu na kisha kuibuka juu humpa mtu furaha na amani lakini si hivyo tu bali kitendo hicho huua majeshi yote ya pepo wabaya ambayo yamekuwa yakimfuata.

Kwa hiyo maji hutupa wokovu na pia humuangamiza shetani na majeshi yake. Bwana Yesu alisema pepo anapomtoka mtu hupitia njia isiyo na maji ili apumzike anaporudi nakukuta nyumba yake imefagiliwa anakwenda kuwachukua pepo wengine saba waovu kuliko yeye, na hali ya yule mtu huja  kuwa mbaya kuliko ile ya kwanza.

Hii maana yake ni kwamba pepo anapomtoka mtu, na mtu yule asipochukua uamuzi wa kakamilisha wokovu wake ikiwa ni pamoja na kupata ubatizo sahihi tena asipokaa katika hali ya usafi basi mtu huyo yupo katika hatari kubwa ya kurudiwa na zile nguvu za giza ambazo zilikuwa zimeshamtoka.

Kwa hiyo ubatizo ni muhimu sana, ni agizo kutoka kwa Bwana Yesu tena lenye faida kwetu kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli, maji yaliwaokoa lakini yakamuangamiza Farao na hakuwafatilia tena.

Mtu asipokamilisha wokovu wake shetani ataendelea kumfatilia. Neno linasema ‘aaminiye na kubatizwa ataokoka’ mambo hayo mawili ni muhimu huwezi kufanya moja ukaacha lingine la sivyo adui hatakuacha.

Kumbuka kisa cha yule mtu aliyekuwa na pepo waliojitambulisha kama JESHI, Yesu alipoamuru mapepo yatoke yalimtoka na kuingia kwenye kundi la nguruwe kisha wale nguruwe wakaondoka na kukimbilia baharini wakafa kwa maji ni sawa tu na Farao na jeshi lake walivyoangamia ndani ya maji. Hii inatupa picha ya uhusiano uliopo kati ya maji na jeshi la adui na hivyo ni muhimu mtu kubatizwa baada tu ya kumuamini Kristo.

Ni jambo la kushangaza kuona mtu ameokoka miezi kadhaa au hata miaka kadhaa iliyopita lakini bado hajabatizwa, sijui mtu huyo anaishi kwa kanuni zipi za wokovu… chukua hatua mapema

Bwana akubariki sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *