Je! una nia gani na kile unachoomba kwa Bwana.
Shalom, jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe
Mara nyingi tumekuwa tukipeleka maombi yetu kwa Mungu na hatuoni kujibiwa mpaka wakati mwingine tunakata tamaa na kusema labda Mungu hasikii.
Ukweli ni kwamba Mungu wetu anasikia sana na anajibu kabisa kwa wakati wala hakawii kujibu… anasema sikio lake si zito, hata asiweze kusikia (Isaya 59:1).
Sasa, kinachochelewesha majibu ya watu wengi pale waombapo, ni wao wenyewe na wala si Mungu, utauliza kwa namna gani? Hebu tusome haya maandiko..
Yakobo 4:1-3 Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu?
[2]Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!
[3]HATA MWAOMBA, WALA HAMPATI KWA SABABU MWAOMBA VIBAYA, ilii MVITUMIE KWA TAMAA ZENU.
Umeona hapo, ni kweli wengi tunaomba sana, lakini hatupati tunachokiomba, kwasababu gani, ni kwasababu huenda tunaomba vibaya ili tutumie kwa tamaa zetu.
Kwa mfano utamkuta mtu anaomba usiku na mchana Mungu ampatie hitaji fulani, tena anatoa na sadaka ili yamkini ajibiwe kwa haraka zaidi akidhani Mungu anaweza kuhongwa, sasa mtu huyu huenda alichokiomba kwa Mungu ni jambo jema kweli, lakini kutokana na nia yake ya ndani kuwa mbaya..anaweza asipokee hitaji hilo kama yeye anavyotaka..badala yake atasubiria sana au Mungu anampa hitaji au kazi nyingine kulingana na mapenzi yake.
Kwa mfano, hebu tumtazame mtu mmoja kwenye biblia ambaye alienda mbele za Mungu na hitaji lake tena akatoa na sadaka mara tatu akidhani labda Mungu atamfanikisha hitaji lake, ambalo kimsingi asingepaswa kupeleka mbele za Mungu.
Hesabu 23:1-8 Balaamu akamwambia Balaki, Nijengee hapa madhabahu saba, ukaniandalie hapa ng’ombe waume saba, na kondoo waume saba.
[2]Balaki akafanya kama Balaamu alivyonena. Balaki na Balaamu wakatoa sadaka, ng’ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.
[3]Balaamu akamwambia Balaki, Simama karibu na sadaka yako, nami nitakwenda, LABDA BWANA atakuja kuonana nami; na lo lote atakalonionyesha nitakuambia. Akaenda hata mahali peupe juu ya kilima.
[4]Mungu akakutana na Balaamu; naye Balaamu akamwambia, Nimetengeneza madhabahu saba, nami nimetoa sadaka ng’ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.
[5]BWANA akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie Balaki; ukaseme maneno haya.
[6]Akarudi kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye.
[7]Akatunga mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli.
[8]Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye BWANA hakumshutumu?
Zingatia hilo neno ”LABDA” huyu Balaamu alijua kabisa Mungu hapendezwi na maombi yake.. lakini yeye alibaki kung’ang’ania kutakia laana adui zake ambao ni watu wa Mungu waliobarikiwa.
Bwana Yesu alisema maneno haya..
Mathayo 5:43-48 Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;
[44]lakini mimi nawaambia, WAPENDENI ADUI ZENU, WAOMBEENI WANAOWAUDHI,
[45]ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.
[46]Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?
[47]Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?
[48]Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
Ni kweli katika Agano la kale imeandikwa mpende jirani yako, na umchukie adui yako, lakini aliye mkuu wa maagano hayo, yeye anasema inatupasa tuwapende adui zetu tena tuwaombee kwa bidii sana kwa kuwa adui wetu mkubwa ni ibilisi na majeshi yake.
Unapokwenda mbele za Mungu kwa maombi au unapotoa sadaka, je una nia gani na vitu unavyovihitaji kwa Bwana? Fahamu kabisa kuwa, ikiwa nia yako ni kwa ajili ya kuwaombea wanadamu wenzako mabaya, au kuwakomoa, fahamu kuwa hayo maombi hayawezi kujibiwa kabisa tena ni MACHUKIZO kwa Mungu, badala ya mabaya yanakuja mema kwa hao hao unaowatakia mabaya, ndivyo ilivyo.
Kama unahitaji Bwana akupe mafanikio Fulani ya kiroho au ya kimwili, hakikisha Nia yako ni njema, kwamba utokane tu na ugumu unaoupitia, na pia upate kitu cha kuwasaidia wengine, na si kwa lengo la kuwakomesha wanaokudharau. Ukiwa na Nia ya kupata vitu ili wengine waone, maombi hayo yanaweza yasijibiwe kabisa.
Bwana atusaidie.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.