KUBALI KUPITISHWA KATIKA MOTO UWE SAFI.
Hesabu 31:23 kila kitu kiwezacho kuuhimili moto, MTAKIPITISHA KATIKA MOTO, NACHO KITAKUWA SAFI, pamoja na haya kitatakaswa kwa hayo maji ya farakano; na kila kitu kisichouhimili moto mtakipitisha katika hayo maji.
Unapozaliwa mara ya pili kwa kumwamini Yesu Kristo na ukatubu dhambi kwa kumaanisha kuziacha kabisa kisha ukabatizwa ubatizo sahihi, basi ni vizuri kufahamu kuwa upo moto wa Roho Mtakatifu ambayo wewe kama mwana wa Mungu huwezi kukwepa ni lazima tu upitishwe katika huo..na kusudi la kupitishwa katika moto huo ni ili uwe safi, kama vile dhahabu inavyosafishwa..
Kwa kawaida sio kila uchafu hutoka kwa maji, mwingine huitaji moto ili kuundoa. Kwamfano ukiupata mwamba wenye dhahabu ndani yake ukipitisha maji huwezi toa uchafu uliogandamana nao,
hivyo wale wafuaji, wanaupitisha kwenye moto, kisha unayeyuka na baada ya hapo uchafu na dhahabu hujitenga kisha wanaikusanya dhahabu. Ndivyo ilivyo na Mungu kwa watoto wake. Upo moto ambao wewe kama mwana wa Mungu ni lazima tu utapitishwa hata iweje, kuondoa mambo sugu yaliyogandamana na wewe yasiyoweza kutoka kwa Neno tu bali kwa hatua ya kimaisha, ndio huo unaoitwa “ubatizo wa moto”. Mfano wa huu ndio ule uliompata mfalme Nebukadreza (Danieli 4), kukaa miaka saba maporini kula majani ili tu aondolewe kiburi ndani yake.
Na ndio maana tunaona pale tu mtu anapoanza kuamini! mara anaanza kuona mambo ya nje yanabadilika, ghafla anachukiwa na ndugu au kutengwa, mwengine atapitia misiba, mwingine magonjwa, mwingine vifungo, mwingine mapigo, mwingine anadorora kiuchumi, mwingine atatengwa n.k. mfano kama walivyopitia akina Ayubu, Yusufu n.k….Lakini Mungu kumpitisha mtu hivyo huwa sio kwa ajili ya kumwangamiza hapana bali ni kumuimarisha hivyo mtu kama huyo Bwana huwa anampa neema ya ziada kuyashinda hayo majaribu, Ni aina Fulani ya maisha ambayo kwako yatakuwa kama moto, lakini mwisho wake hukuletea faida ya roho yako
1 Petro 1:6-7 Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;
[7]ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.
Hivyo, wewe kama mwana wa Mungu, tambua kuwa ni lazima upitishwe katika moto ili uwe safi. Usidhani kusafishwa tu na damu ya Yesu ndio basi, utatakaswa na hiyo ni katika maisha yako yote. Haiwezekani mtu aliyeokoka ambaye amepokea Roho maisha yake yote awe Yule Yule wa zamani, hizo sio kanuni za wokovu, wala sio kusudi la Mungu. Ukubali utakaso, au usiwe mkristo kabisa. Kwasababu hivi viwili huenda sambamba wala haviwezi kutenganishwa. Huo ndio upendo wa Mungu.
Utukufu na heshima ni vyake milele na milele.
Bwana akubariki.
Shalom.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.