
KUWA MTU WA KUTAFAKARI
Mwanzo 24:63 Isaka akatoka ili KUTAFAKARI kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja.
Nakusalimu katika jina tukufu la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
Siku ya leo tutaenda kujifunza jambo moja ambalo ni muhimu kulitendea kazi katika safari yetu ya Imani,
Na jambo lenyewe ni KUTAFAKARI! kutafakari ni moja jambo la msingi mkristo anatakiwa awe nalo katika maisha yake ya ukristo,
Kutafakari ni nini?
Kutafakari ni hali ya kufanya ubongo ufikiri, au uwaze au ukumbuke jambo fulani lililopita, linaloendelea au linalokuja, Kwa mfano mwanafunzi mzuri ni lazima atafakari juu ya maisha yake ya elimu, kwamba alitoka wapi? na kwanini yupo shuleni, na anatarajia nini mbeleni, anarajia afike wapi kielimu au aje awe nani baadaye, na nini afanye ili afanikiwe kufaulu kifika anakotaka afike? hiyo ndiyo sifa ya mwanafunzi bora, huwa akifeli hatumii muda mwingi kulaumu na kulalamika, bali anatumia muda mwingi kutafakari kwanini amefeli, na anatakiwa afanye nini asifeli tena, vile vile wafanya biashara, n.k, huwa wanatumia muda mwingi kutafakari juu ya maendeleo ya biashara zao, kazi zao, n.k, Hiyo ndiyo maana ya kutafakari kwa ufupi.
Sasa tukirudi katika ukristo, lazima mkristo uwe mtu wa kutafakari, juu ya mahusiano yako na Mungu, utafakari mwenendo wako wa kila siku, je unapoa au unazidi kuimarika, je! tangu ulipookoka umemzalia Mungu matunda kwa kiwango gani? ni watu wangapi umewashudia habari njema ya wokovu?
Wakati watu wengine wa kidunia wanatafakari na kufanya hesabu ya mavuno yao waliyoyavuna katika mwaka mzima, je! na wewe unaweza ukatumia muda wako kutafakari mavuno uliyoyavuna kwa Kristo ndani ya mwaka huu, ni watu wangapi umewaleta kwa Kristo?
Wakati wengine wanatafakari na kufanya hesabu ya biashara zao, mipango yao, na kutafakari namna ya kuboresha kazi zao, je na wewe kama mkristo unaweza ukatumia muda wako kutafakari kazi ya Mungu, namna ya kuiboresha, namna ya kupeleka Injili kwa watu wote, ukatafakari ni wapi umekuwa ukianguka na ni kwanini? na ufanye nini ili usianguke tena katika eneo hilo?
Kama mkristo lazima uwe mtu wa kutafakari, Jifunze kutenga muda wako na kutafuta sehemu tulivu utafakari kwa kina, kuomba, kusoma Neno hakukutoshi tu, tumia pia muda wako kutafakari, na utapata faida nyingi, utaweza kuvumbua namna bora ya kufanya kazi ya Mungu, utaweza kugundua udhaifu wako na kutafutia suluhisho, utaweza kupokea ufunuo kirahisi kwa Mungu..kwani mara nyingi Mungu anasema na mtu katika mazingira ya utulivu.
1Wafalme19:11 Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za BWANA. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za BWANA; lakini BWANA hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi;
12 na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini BWANA hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto SAUTI NDOGO, YA UTULIVU.
13 Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, SAUTI IKAMJIA, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya?
Uombapo jifunze kukaa uweponi mwa Mungu, usiombe tu na kuondoka, wakati mwingine ukimaliza kuomba, anza kutafakari ukuu wa Mungu, kaa tulia kwenye utulivu, huku ukitafakari, ndipo utasikia sauti ndogo ikisema nawe, na utapokea maelekezo kwa Bwana,
Daudi ambaye alikuwa ni mtu wa kutafakari sana muumba wake, alisema…
Zaburi 27:4 Neno Moja nimelitaka kwa BWANA, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa BWANA Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa BWANA, Na KUTAFAKARI HEKALUNI mwake.
Anza leo kuwa mtu wa kutafakari, tafakari juu ya ukristo wako, ukristo sio kwenda tu kanisani kila week na kurudi na zaidi ya hapo! yapo mambo mengi Bwana anatarajia uyafanye, hivyo amka hapo anza kutafakari na Bwana atasema nawe, tafakari njia bora ya kuhubiri injili tuliyoagizwa kuhubiri kwa watu wote, tafakari namna bora ya kufunga na kuomba, tafakari mwenendo wako, tafakari namna ya kumpendeza Mungu kila siku.
Waefeso5:10 mkihakiki ni nini impendezayo Bwana.
Je! Umeokoka? Kama bado hujampokea Yesu kwa ukamilifu, yaani hujatubu kwa kuziacha dhambi zako, hujabatizwa ubatizo sahihi, hujapokea Roho Mtakatifu! Hi ndiyo nafasi yako! dhamiria kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi na kuacha ulimwengu na tamaa zake kisha tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa JINA LA BWANA YESU upokee kipawa cha Roho Mtakatifu ili uweze kumzalia Mungu matunda, Roho Mtakatifu ni ahadi kwa kila mmoja atakayemwamini Yesu na kusalimisha maisha yake kwake.
Matendo 2:39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
Na wote wasio na Roho wa Kristo hao sio wake..(Warumi 8:9), unahitaji kumpokea Roho wa Mungu ili ufanyike mwana wa Mungu, upokee nguvu ya kushinda dhambi, upokee nguvu ya kuwa shahidi wa Kristo, sawasawa na..
Matendo 1:8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu…”
Ndugu, dada uliye nje ya Kristo, tafakari leo juu ya hatima yako, kisha ufanye maamuzi sahihi ya kumgeukia Kristo, Bwana amekupa akili ya kufanya maamuzi, tumia akili yako vizuri.
Kumbukumbu 32:29 Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya, Ili watafakari mwisho wao.
Usikubali mwaka huu upite hujampokea Yesu maana haujui yatakayotokea mwakani. (Unyakuo umekaribia).
Maranatha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.