
Kwanini watu wengi watakataliwa siku ile?
Kristo alisema watu wengi watakuja siku ile wakisema Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? (Mathayo7:22).
Lakini yeye atawaambia sikuwajua kamwe, maana yake tangu mwanzo wakiwa wanalitumia jina lake hawakujulikana, japo kuwa walikuwa wanatoa pepo na kufanya miujiza mingi kwa jina la Yesu.
Hii inamaana kuwa kufanya hivyo vyote, yaani kutoa unabii, kutoa pepo kwa jina lake, kufanya miujiza n.k sio kigezo cha kuingia mbinguni.!!
Sasa kigezo ni kipi? Tusome..
Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; BALI NI YEYE AFANYAYE MAPENZI YA BABA YANGU ALIYE MBINGUNI.
[22]Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
[23]Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.
Umeona hapo! Kumbe kigezo cha kuingia mbinguni ni kufanya mapenzi ya Mungu na sio kujiita tu mkisto, sio kujiunga na kikundi cha kwaya, sio kutoa sadaka nyingi hapana, hayo yote ni vizuri kufanya, lakini kama huyafanyi mapenzi ya Mungu hayo yote sio kitu!! Haijalishi ulikuwa unafunga na kukesha, haijalishi ulikuwa unaimba vizuri, haijalishi ulikuwa unanena kwa lugha, haijalishi unafanya nini kwa Mungu!!
Wengi watakataliwa siku ile sio kwasababu walikuwa hawajabatizwa , sio kwasababu walikuwa hawajui biblia, sio kwasababu walikuwa sio waombaji!, bali ni kwasababu hawakuwa wanafanya mapenzi ya Mungu!!
Sasa utauliza mapenzi ya Mungu ni yapi? Je kufanya hayo yote sio mapenzi ya Mungu?
Ndiyo kufanya hayo yote sio mapenzi ya Mungu bali ni wajibu wa kila mkristo, yaani kumtumikia Mungu kwa kutoa sadaka, kuwaombea wengine, kuimba, n.k ni wajibu na wala sio ombi.
Lakini mapenzi ya Mungu hasa ni yapi? Ambayo tusipozingatia hata hayo yote hayana maana.
Tunasoma..
1Wathesalonike 4:1-5 “Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana.
[2]Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu.
[3] MAANA HAYA NDIYO MAPENZI YA MUNGU, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati;
[4]kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake KATIKA UTAKATIFU NA HESHIMA;
[5]si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu.
Umeona mapenzi ya Mungu!!
Ni kutakaswa na kuepukana na uasherati.
Maana yake bila utakaso wa nafsi, roho na mwili hakuna atakayemuona Mungu haijalishi yeye ni nani au anafanya nini katika kanisa.
Waebrania 12:14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;
Kumbuka ni utakatifu wa nje na ndani!!
Maana yake mwili wako wote uwe safi na roho yako pia mpaka ile siku ya kuja kwake Bwana.
1Wathesalonike 5:23 Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu NA MIILI YENU mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
Wewe leo binti unayesema Mungu anaangalia moyo tu haangalii mwili, nataka nikuambie usipotubu na kuondoa hayo mapambo uliyoweka kwenye mwili wako, usipotubu na kuondoa mavazi yasiyopasa jinsia yako (suruali) na nguo za nusu uchi (vimini), na zile zinaonyesha maungo yako/shepu yako (zinazobana) fahamu kuwa utakuwa miongoni mwa watakaokataliwa siku ile, haijalishi leo malaika wanakutokea, haijalishi unaimba vizuri, haijalishi unanena kwa lugha, hayo yote haijalishi.
Kinachojalisha ni kufanya mapenzi ya Mungu, yaani kuishi katika utakatifu wote nje na ndani.
Hivyo dada/kaka hebu amua kubadilika leo. Amua kumfuata Yesu kwa moyo wako wote, amua kujikana nafsi na kuchukia ulimwengu, amua kuokoka kweli kweli.
We Askofu, mchungaji, nabii, mwalimu, mwanakwaya, tafuta kufanya mapenzi ya Mungu usije ukakataliwa siku ile maana itakuwa ni siku ya majuto makuu mno.
Hiyo siku imekaribia sana, huwenda ni leo au kesho au mwaka huu nani ajuaye, kama vile mtu asipojua siku yake ya kufa ndivyo ilivyo hakuna aijuaye ile siku ni lini! Lakini tumepewa kutambua majira na nyakati. Hivyo tunaishi katika hayo majira ya kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Fumbua macho yako angalia majira na nyakati tunayoishi sasa.
Bwana wetu Yesu anarudi
(Maran atha)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.