Maono yako ni nini katika mwaka mpya 2025
Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuongeze maarifa zaidi.
Ni muhimu kwanza tukaelewa nini maana ya maono katika Muktadha wa kawaida kabisa.
Maono ni nini? Ni dira au ndoto kuhusu maisha yako au malengo yako ya baadae. Tunaweza kusema.. ni muelekeo wa kimkakati unaolenga kufanikisha jambo fulani kubwa maishani.
Au
Ni picha halisi ya hatima itarajiwayo. Ambayo Mtu anatazamia kuifikia baadae katika kipindi fulani cha maisha yake.
Sasa karibia watu wote huwa tunamaono ambayo tunayatazamia kuyafikia katika kipindi fulani cha maisha yetu au katika mwaka fulani..
Sasa Wakristo wengi wanakuwa maono ya kuyafikia katika mwaka mpya unapoanza lakini bahati mbaya sana wanaishia kuwa na maono ya mwilini tu wanasahau kuwa na maono na mikakati na mipango ya mambo ya rohoni.
Hivyo kupelekea kupoteza nidhamu ya mambo ya rohoni.
Kwa sababu siku zote maono ndio yanayotengeneza kitu kinachoitwa NIDHAMU.
“Pasipo maono hakuna nidhamu na pakikosekana nidhamu hakuna mafanikio yoyote iwe katika mambo ya mwilini au ya rohoni “
Ni rahisi sana kupuuza mambo ya rohoni (Ki-Mungu) kama hauna ono lolote juu ya unataka kufikia katika viwango fulani katika kumjua Mungu ndani ya kipindi fulani.
“Kama huna ono lolote kuhusu mambo ya rohoni ni vigumu kuwa na Nidhamu na mambo ya rohoni utakuwa na nidhamu katika mambo mengine ambayo una maono juu yake”
Ni muhimu sana kuangalia na kutafakari hali yako ya kiroho toka mwaka huu uanze mpaka leo tumepakisha masaa machache kuumaliza. Na kuangalia ni katika eneo gani hauko sawa sehemu pa kuboresha/kujirekebisha na ni jambo gani jipya unatamani liumbike ndani yako ili uzidi kuboresha zaidi mahusiano yako na Mungu na kuzidi kuwa mtu wa rohoni zaidi.
Lakini kama mwaka unaanza unaisha huna cha kuboresha,kuongeza,kujirekebisha, na hutamani kupanda katika viwango fulani vya kiroho na unaona uko sawa ndugu unatatizo. Mbegu uliyoipokea asili yake ni kukua kila siku.
Sasa ukiona kuna tatizo mahali popote na unataka kufikia katika viwango vingine tena zaidi chukua hilo kama ono lako kuelekea 2025 na tamani na kuwa na shauku ya kufikia hapo.
Kumbuka maono ni zao la kitu kinachoitwa wazo. Hivyo wazo siku zote ndio linalozaa maono. Na maono yakishazalika inapelekea kuzaliwa kitu kingine kinachoitwa NIDHAMU na nidhamu ndio inakupelekea kufikia malengo.
Nidhamu. Uwezo wa kuzitawala hisia zako na kufanya jambo unalotakiwa kulifamya kwa wakati sahihi pasipo kuangalia unajisia au hujisikii.
Changamoto zinazoweza kujitokeza katika kuyafikia maono unayojiweke.
Changamoto hazikosi kuwepo kutoka kwa adui hasa pale unapodhamiria kwenda hatua nyingine katika mambo ya rohoni. Nazo zinaweza kuwa…
1.Vishawishi
Shetani atakuletea Vishawishi vya kila namna ili kuhakikisha unaishia njiani juu ya safari uliyoianzisha na fahamu dhambi ndio kitu kikubwa sana kinachoua maono ya Mkristo.Tusingemsoma Yusufu leo hii kama angekubali kulala na mke wa potifa.
2.Uvivu.
Ili kutimiza maono yako uliyojiwekea lazima ushindane na huyu adui.
3.kukatishwa tamaa.
Kuna wakati utakatishwa tamaa na watu wa namna zote wanaokuzunguka ikiwemo familia yako na wapendwa wenzako pia.
Vipo Vishawishi vingi sana na unapaswa kuvishinda..
Ni faida gani tunazipata tunapokuwa na maono ya Ki-Mungu?
Ziko faida nyingi sana tunazozipata pale tunapodhamiria kweli kutimiliza maono tunayojiwekea juu ya kuutafuta ufalme wa Mungu.
1.kujizuia(kuwa na mipaka).
Unapokuwa na maono ni lazima utakuwa ni mtu wa kujizuia katika mambo mengi sana maandiko yanasema..
Mithali 29:18“Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.”
Mkristo asiyekuwa na maono hawezi kujizuia katika mambo mbali mbali. Wala hawezi kuwa na Nidhamu na mambo ya Ki-Mungu kabisa. Atakuwa ni Mkristo jina.
2.Kutokupoteza muda kwenye mambo yasiyo ya lazima(Msingi).
Unapokuwa na maono katika mwaka kufikia katika hatua fulani ni lazima hutapoteza muda wako mwingi kufanya/kukaa katika mambo yasiyo ya lazima..
Utakuwa na mipaka,huwezi kwenda kila mahali,huwezi shiriki katika kila kitu. Utakuwa ni mtu unajali sana muda maana maono yako yamefungwa ndani ya muda husika.
3.kuyaheshimu na kuyathamini mambo ya Ki-Mungu.
Ni lazima utaanza kuwa na Nidhamu na mambo ya rohoni na unapoanza kuwa na nidhamu ndio unapoanza kupiga hatua katika kulielekea ono lako.
Kama Mkristo unatakiwa kuwa na Maono gani mwaka 2025.
Kama Mkristo kuwa na maono haya kuelekea mwaka 2025 nakuhakikishia ni swala la muda mfupi sana hutakuwa kama ulivyokuwa 2024. Angalia sehemu ambayo hauko sawa shughulika nayo weka mikakati ya kuimarika. Usiseme “ipo siku haitakuwepo hiyo siku kama hutakusudia.”
1.Imarisha zaidi mahusiano yako na Mungu.
Kila siku tafuta kumpendeza Mungu zaidi kwa kufanya yale yanayokupasa kufanya.
Waefeso 5:17“Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.”
2.Weka ratiba ya kuisoma biblia yote kila siku kwa mtiririko.
Ni muhimu sana kuweka ratiba ya kusoma Biblia yako kila siku ikiwa kila siku kurasa 5 au 4 kwa siku zitafakari. Acha kusoma kwa kudonoa donoa Soma ukurasa baada ya ukurasa.
Ni aibu Mkristo kuanzia January mpaka December hujamaliza kusoma biblia yote wala hujawahi kumaliza kusoma hata kitabu kimoja leo mwisho wa mwaka.
3.jiepushe na Dhambi na kujitenga na ubaya wa kila namna.
Weka jambo hili kama ono lako mwaka 2025 uwe wa kitofauti kumbuka unapojiepusha na dhambi ndio unatoa mlango wa Mungu kuwa na ushirika nae mzuri.
1 Wathesalonike 5:22“jitengeni na ubaya wa kila namna.”
Tambua wewe kama Mkristo dhambi ni kitu kibaya kwako kuliko vyote hivyo epuka. Kama ulikuwa na kampani za marafiki wabaya wakate kuanzia leo,ikiwa unaangalia tamthilia za kidunia achana nazo,kama unasikiliza miziki ya kidunia acha kuanzia leo,nk utaanza kuona mabadiliko makubwa.
4.Tengeneza ratiba ya kuomba kila siku.
Huwezi kuomba usipoamua kuwa muombaji. Maombi ni Mawasiliano kati yetu na Mungu na sio adhabu Leo hili. Ikiwa unataka kuwa ni mtu mwingine basi anza jambo hili kama Huwezi kuomba hata lisaa 1 anza na dakika 20 kesho ongeza tano hivyo hivyo utajikuta unaenda hata masaa 2 na zaidi na utaelewa maombi ni mazuri sana.
Yesu pamoja na kuwa Mungu alikuwa ni muombaji wa masafa marefu mno na alikuwa na matokeo makubwa katika huduma yake kuliko mtu yeyote ulimwenguni hapa.
5.Anza kuwashuhudia wengine.
Ikiwa umeokoka na hujawahi kuwashuhudia wengine anza mwaka huu unaonanza kesho.. utaanza kuona furaha ya wokovu pale unapolitimiliza agizo kuu.
Usikae kae nyumbani tu nenda mtaani kamtoe shetani ndani ya watu Pelika habari njema watu wafunguliwe ni aibu wewe ulitolewa dhambini kwa kuhubiriwa na wewe hujawahi hata kufumbua kinywa chako kuwatoa watu dhambini acha ubinafsi.
6.komboa wakati (epuka kusitisha sitisha)
Ukijijengea nidhamu hutakuwa mtu wa kusitisha maana utafanya mambo yote haya kwa wakati uwe hujisikii ama unajisikia kwa sababu ya maono yaliyotengeneza nidhamu ya hali ya juu.
Hili ni tatizo linalowasumbua wengi. Hvyo jitahidi kuzitawala hisia zako.
Naimani mambo haya ukiyazingatia ndani ya mwaka wote 2025 kufikia mwaka 2026 hutakuwa kama ulivyokuwa utakuwa ni mtu mwingine kabisa wa viwango vya juu.
“UKUWAJI WA KIROHO SIO BAHATI BALI NI MIKAKATI NA KUKUSUDIA.”
hivyo pasipo kukusudia hakuna ukuwaji wa kiroho.. ukuwaji wa kiroho sio bahati au hautokei tu bali ni mchakato amua leo kuanza mchakato huu.
Naamini unaweza nimekuombea.
Ubarikiwe sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.