Msaada wa Mungu unategemea jitihada zako.
Kuna vitu hatuwezi kuvipokea kwa Mungu mpaka tuweke bidii kuvitafuta au kuvifanya ndiyo msaada wa Mungu utokee. Wengi tunashindwa kupiga hatua mbele kwasababu ya kumuachia Mungu afanye mambo yote…tunataka tuende tu mbele za Mungu tuombe atusaidie halafu turudi kukaa kusubiria huo msaada, nataka nikuambie leo ondoa hiyo mtazamo ndani yako.
Ni kweli Mungu anatusaidia kwa kiasi kikubwa, lakini anasaidiana na sisi, kwahiyo sio jambo la kusema nimemwachia yeye halafu unaenda kulala.
Hebu tujifunze kwa mtu mmoja katika biblia ambaye alikuwa karibu na Mungu katika kila jambo, na mtu huyo sio mwingine zaidi ya Daudi, kama tunavyojua Daudi alikuwa anamtegemea Mungu kwa kila kitu na Mungu alimsaidia sana, lakini ilifika mahali aliomba msaada kwa Mungu zidi ya maadui zake, na Mungu alikuwa pamoja naye kama siku zote, lakini alimwambia Neno moja ambalo leo nataka tuitafakari kwa undani. Tunasoma
2 Samweli 5:22 Lakini wakapanda hao Wafilisti tena mara ya pili, wakajitawanya bondeni mwa Warefai.
[23]Naye Daudi alipouliza kwa BWANA, alisema, Usipande; zunguka nyuma yao, ukawajie huko mbele ya miforsadi.
[24]Kisha itakuwa, hapo utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, NDIPO NAWE UJITAHIDI; kwa maana ndipo BWANA ametoka mbele yako awapige jeshi la Wafilisti.
Umeona hilo neno ”NDIPO NAWE UJITAHIDI ” ni kweli msaada upo lakini jitihada inahitajika.
Unataka Bwana akusaidie kushinda vita vya kiroho lakini huna jitihada katika kuomba, kufunga na katika kukesha, husomi biblia, unasubiria tu kusomewa kila jumapili. Nataka nikuambie huo msaada utasubiri sana na shetani ataendelea kukusumbua.
Halikadhalika unataka Bwana akupe sauti nzuri ya kuimba na kumsifu yeye..ni kweli Bwana anaweza kukupa lakini “NAWE UJITAHIDI” jitahidi kufanya mazoezi, jitahidi kuimba hata kama sauti yako ni mbaya..we usijali wala usiangalie udhaifu wako.. Bwana mwenyewe atakusaidia.
Vilevile hata katika eneo la kuomba, usikae tu kusema mimi sijui kuomba.. Mungu atanisaidia! Hapana, we anza kuomba hivyo hivyo, kidogo kidogo Bwana atakusaidia. Na hatimaye utajikuta umekuwa hodari wa kuomba.
Hebu leo anza kuweka jitihada katika mambo ya kiroho, Anza kuwa mwombaji, anza kushuhudia na kuhubiri Injili..we usiangalie udhaifu wako wala usiwatazame watu, yupo Roho Mtakatifu msaidizi wetu.
Na Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.