MWANZO WA MWAKA MPYA VAA SILAHA ZOTE ZA MUNGU

Biblia kwa kina No Comments

MWANZO WA MWAKA MPYA VAA SILAHA ZOTE ZA MUNGU

Jina la Bwana YESU mkuu wa wafalme wa dunia (ufunuo1:5) na mkuu wa uzima libarikiwe daima.

Heri ya mwaka mpya wa 2026, Karibu katika masomo yanayohusiana na mwanzo wa mwaka mpya..ili tuanze mwaka wetu na Bwana na tukapokee baraka tele za rohoni na mwilini.

Ikiwa we ni mwana wa Mungu.. Namaanisha umeokoka na upo ndani ya Kristo…basi huu ni wakati wa wewe kuvaa silaha za vita na kuingia kwenye mapambano..huu sio wakati wa kukaa nyumbani na kutazama mambo yasiyo na maana au kwenda kuzurura zura huku na huko.

Unajua kosa kubwa alilolifanya Daudi mpaka ikapelekea ashindwe kumjengea Mungu nyumba/hekalu na badala yake Sulemani mwanawe alikuja kujenga ile hekalu kama tunavyojua..kosa kubwa alilolifanya ukiachilia mbali makosa ya kumwaga damu ya watu wengi, kosa lingine kubwa ambalo ilipelekea ashindwe kutimiza malengo yake aliyoiweka kwa Mungu wake ni kulala/kuzini na mke wa Uria (Jemedari wake) na haijaishia tu hapo ila pia alimwua huyo shujaa wake.

Jambo hili ilimwaibisha sana Daudi na kumshushia hadhi.. japokuwa alikuja kutubu na kujutia kosa lake na Mungu akamsamehe ila mpaka leo tunasoma habari zake, kwasababu Mungu alimwambia ulifanya jambo hili kwa siri, bali mimi nitalifanya liwe mbele ya Israeli wote na mbele ya jua..ndio maana hadi leo tunajua huo uasi aliyoifanya mfalme wa Israeli (Daudi) japokuwa alililifanya kwa siri akijua hakuna anayemwona.

Kwa tendo kama hili alilolifanya Daudi lilitoa pia nafasi kwa adui kumfukuru Mungu na kulitukana jina lake. Sasa biblia inatuambia Daudi aliyafanya haya mwanzoni mwa mwaka mpya. Hebu tuisome hiyo habari kwa ufupi..

2Samwueli 11:1 Hata ikawa, MWANZO WA MWAKA MPYA, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. LAKINI DAUDI MWENYEWE AKAKAA YERUSALEMU.

2 Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho.

3 Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti?

4 Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.

Sura ya 12:13 Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi. Nathani akamwambia Daudi, BWANA naye ameindoa dhambi yako; hutakufa.

14 Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za BWANA nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.

Tena Bwana akamwambia Daudi…

2Samweli12:10 Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako. nawe umemwua huyo kwa upanga wa wana wa Amoni.

11 BWANA asema hivi, Angalia, nitakuondokeshea uovu katika nyumba yako, nami nitawatwaa wake zako mbele ya macho yako, na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako mbele ya jua hili.

12 Maana wewe ulifanya jambo lile kwa siri; bali mimi nitalifanya jambo hili mbele ya jua.

Sasa nataka tuitazame kwa makini hili tukio alilolifanya Daudi.. ilikuwa ni MWANZO WA MWAKA MPYA, mwanzo wa wafalme kwenda vitani, yeye Daudi akabaki nyumbani tena kitandani mpaka shetani akamwingia.

Na sisi tukiwa kama wafalme huu ni mwanzo wa mwaka mpya, tuvae silaha za Mungu na tuingie vitani,

Waefeso 6:10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake

11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani.

12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, 

15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16 Zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;

18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha Kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

Paulo Mtume wa Bwana alisema….

Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; (2Timotheo 4:7)

Maana yake kila siku tupo vitani…hatulali maana adui yetu naye halali..kila siku anazunguka-zunguka akitafuta mtu ammeze…ndiyo yule aliyemwingiza Daudi kwenye dhambi alipomkuta analala kitandani akampa mawazo ya kwenda kuzini, laiti Daudi angezivaa silaha zake akaingia vitani kama wafalme wengine asingekutwa na hayo.

Biblia pia inatuambia Hamjafanya vita mpaka kumwagika damu, mkishindana na dhambi; (Waebrania 12:4)

Tupo mwanzo wa mwaka mpya wa 2026..kama askari wa Bwana vaa silaha za vita ingia vitani..nenda kashudie habari njema ya wokovu kwa wale walioshikiliwa na adui, kawaeleze kusudi la Mungu kuwaingiza katika mwaka huu ingali bado wanatenda matendo ya giza.. ukahaba, uasherati, uchafu, ulevi, usengenyaji, uhuni, uchawi, n.k, kwanini mpaka sasa wajaenda motoni?

Na pia huu ni wakati wa kuvaa hiyo silaha ya maombi kuharibu kalenda zote zilizopangwa juu yako katika mwaka huu, fahamu kuwa kama vile wanadamu walivyo na kalenda ya mwaka mzima na tayari wameshajua matukio yatakayotokea ndani ya siku kadha wa kadha, vivyo hivyo naye shetani anayo kalenda yake ambayo ameiandaa kwa mwaka wote wa 2026 na tayari kashaweka tageti zake kwamba kuna siku fulani kila mwenzi au baada ya miezi fulani atafanya tukio fulani baya kwako, Kwahiyo ni wakati wa kusimama hali tumevaa hizo silaha za Mungu ambayo ni pamoja na maombi..tuiharibu na kuzichana hiyo kalenda yote aliyokuandalia shetani kwa mwaka huu, acha kuzurura zura ama kushinda kutazama simu, Tv, n.k katika mwanzo wa mwaka mpya. Ingia kwenye maombi ya mikesha, vifungo..peleka mwaka wote kwa Bwana, weka wakfu kila mwenzi na kila siku, weka kalenda yako na futa ile ya shetani, yamkini shetani amepanga siku fulani ukose ibada, au akuletee jaribu ama janga fulani..futa na haribu hiyo kalenda.

Na ikiwa wewe unayesoma huu ujumbe ndio bado ujampokea Yesu..au umempokea nusu.. katika hali ya uvuguuvugu, nataka nikuambie ni kwa rehema za Mungu umevuka mwaka wa 2025 na kuingia mwaka huu wa 2026, na Bwana alikuvumilia katika hizo miaka zote ambazo umekuwa ukisikia injili na kushupaza shingo yako usitake kugeuka na kuacha ulimwengu, kuacha njia zako mbaya, hayo Matendo ya giza unayoyafanya kwa siri kama kujichua, usagaji, kutazama pornography, Bwana amekuvumilia kwasababu ya upendo wake ulio mwingi, bado anajali na roho yako hataki uende kwenye ziwa la moto, sasa yamkini huu ndio mwaka wako wa mwisho, yamkini hii ndiyo nafasi yako ya mwisho Bwana amekupa.. Sasa usiendelee kufanya moyo mgumu, tubu dhambi zako na mgeukie Bwana Yesu akuokoe na moto wa Jehanum, akupe uzima wa milele.. maanisha kabisa kufuata Yeye aliye mkuu wa Uzima, maanisha kumfuata kwa kuamua kukana nafsi yako, na kukubali kuonekana hauna akili, acha kuchezea hatima yako, acha kuchezea hii neema ya mwisho ambayo unapewa, kumbuka baada ya kufa ni hukumu wala hakuna tena kutubu na kusamehewa soma Waebrania 9:27, tubu mgeukie Bwana Yesu akuoshe dhambi zako na akupe Roho wake Mtakatifu akusaidie uishi maisha yanayompendeza Mungu (maisha ya utakatifu), na tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa JINA LA BWANA YESU ili ukamilishe wokovu wako, kumbuka siku zako zinahesabika na vile vile ile siku kuu inayotisha ya Bwana inazidi kukaribia, unyakuo upo karibu, dhiki kuu imekaribia.

Huu ni mwaka wako wa kuzaa matunda yapatanayo na toba.. maana shoka limekwisha kuwekwa tayari.. muda wowote utakatwa usipozaa matunda ya toba.

Mathayo 3:10 Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.

Luka 13:6 Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.

7 Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?

8 Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi;

9 nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate”.

Jiulize ni miaka miangapi sasa imepita tangu uanze kusikia injili inayohuburia utubu? Na Leo hii yamkini huu ni mwaka wako wa kumi hakuna matunda uliyoyazaa..ule usengenyaji, uasherati, uongo, kiburi, wivu na kutokusamehe ambao ulikuanao mwaka juzi bado leo hii unayo..wala hakuna matunda yoyote uliyozaa kulingana na ulichokitubia, sasa yamkini huu ni mwaka wako wa mwisho na usipozaa matunda yapasayo toba fahamu shoka limekwisha kuwekwa tayari kwa ajili ya kuukata huo mti usiozaa matunda maana anaendelea tu kuharibu nchi. Na wewe ndio huo mti!!

Bwana atusaidie tuzae matunda yapasayo toba katika mwaka huu.

Nikutakie heri ya mwaka mpya.

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea.

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *