NA HAPO PATAKUWA NA NJIA KUU
Isaya 35: 8 “Na hapo patakuwa na NJIA KUU, na njia, NAYO ITAITWA, NJIA YA UTAKATIFU; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; WASAFIRIO, WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO”.
Jina la Bwana na Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe daima. Karibu katika mafundisho ya biblia, Neno la Mungu wetu lililo Taa na Mwanga wa Njia zetu (Zab.119:105).
Zipo njia Mbili tu zilizowekwa mbele ya kila mwanadamu, Nazo ni njia ya UZIMA, na njia ya MAUTI.
Yeremia 21:8 “Nawe waambie watu hawa, Bwana asema hivi, Tazama naweka mbele yenu NJIA YA UZIMA, na NJIA YA MAUTI”.
Njia ya Uzima, inamwongoza mtu “Uzimani”..na Njia ya Mauti inamwongoza mtu “Mautini (ziwa la moto)”.
Njia ya uzima ni nyembamba na imesonga sawa sawa na maneno ya Bwana aliyoyasema katika..
Mathayo 7:13 Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, NA NJIA NI PANA IENDAYO UPOTEVUNI, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo.
[14]Bali mlango ni mwembamba, NA NJIA IMESONGA IENDAYO UZIMANI, nao waionao ni wachache.
Hii imeitwa Njia kuu kwasababu wanaopita juu yake ni wachache, na ni WATAKATIFU tu WALIOSAFARINI ndio watakaopita juu yake, Hakuna mtu mwingine yeyote atakayeweza kupita katika hiyo njia isipokuwa amekidhi hivyo vigezo, ndio maana wengi hawataki kupita, bali wamechagua kupita ile njia pana iendayo upotevuni. (Njia ya mauti)
Na njia ya Uzima imenyooka haina migawanyiko mingi (sawasawa na Yohana 14:6), ambapo Bwana YESU alisema yeye ndio hiyo “Njia”, na mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yake yeye.
Lakini anaendelea kusema… hiyo “Njia kuu” itaitwa Njia ya utakatifu, na ya watu wasafirio..
Isaya 35:8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, NJIA YA UTAKATIFU; wasio safi hawatapita juu yake; BALI ITAKUWA KWA AJILI YA WATU HAO; WASAFIRIO….”
Maana yake wote wanaiendea hiyo njia ya Uzima (YESU) Ni lazima “utakatifu” uwe muhuri wao sawasawa na kitabu kile cha Waebrani 12:14.
Vile vile ni lazima wawe “wasafiri”.. Tabia ya msafiri huwa anadumu katika chombo cha usafiri awapo safarini, na hawezi kujishikisha na mambo akutanayo njiani au barabarani…. na chombo chetu cha usafiri ni NEEMA YA MUNGU. Tuwapo katika safari hii ya kwenda mbinguni kupitia njia ya Bwana YESU, mambo ya ulimwengu hayapaswi yashikamane na sisi.
1Petro 2:11 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho”.
Ndugu, je! unapita katika hii njia kuu? Kumbuka biblia inasema ni NJIA KUU ni NJIA YA UTAKATIFU, haijasema ni njia ya dini, au ya dhehebu, au ya upako, au ya miujiza, au ya utajiri, au ya umaskini, hapana inasema ni NJIA YA UTAKATIFU, ikiwa na maana kuwa wale wasafiri ambao ni watakatifu ndio wanaoipita hiyo,na si mwingine yeyote unaweza ukadhani upo katika njia hiyo kwasababu tu wewe unayo dini, lakini ndugu kama huna UTAKATIFU haupo katika hiyo njia, hata kama utatoa zaka kiasi gani, kama wewe haujajiweka kama mtu anayesafiri, basi jua haupo katika njia hiyo. Biblia ipo wazi kabisa inasema.
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”;
Unaona hapo?, wewe unayesema ni mkristo na unasema upo safarini, umefika katikati ya safari yako umekutana na anasa na burudani za ulimwengu huu, unasahau kuwa wewe ni mkristo unayesafiri unaanza na wewe kushikamana na hivyo vitu vya ulimwengu huu vinavyopita, unaanza na wewe kuhudhuria karama za ulafi, unaanza kujishughulisha na rushwa, unaanza kujichanganya na watu waovu wa ulimwengu huu, ulikuwa ni mwombaji mzuri hapo mwanzo lakini sasa biashara na udanganyifu wa mali vinakusonga, wewe kila wakati ni mali tu, unasahau maisha yako ya rohoni, hujui kuwa muda unazidi kwenda na kile chombo ulichokuwa unasafiria (Neema) hakiwezi kikakusubiria muda wote huo,
Ulikuwa unavaa vizuri na kujisitiri hapo mwanzo, lakini ukafika kituo ukakutana na fashion za ulimwengu huu, ukasahau kuwa upo safarini ukauacha utakatifu uliokuwa nao hapo mwanzo na wewe ukaanza kuvaa suruali na kaptura, ukaanza kuvaa nguo fupi, ukaanza kuvaa nguo zinazochora maumbile yako, ukaanza kupaka ma-lipstick, na wanja, na hereni na ma-wigi kama wanawake wa ulimwengu huu, hujui kuwa muda unazidi kwenda na kile chombo ulichokuwa unasafiria kimeshaanza kukuacha.
Mwanzoni mwa safari yako mawazo yako yalikuwa yameelekea mbinguni tu, ulikuwa unatamani ufikie kilele cha safari yako mapema, ulikuwa unafikiria kila siku habari za mbingu mpya na nchi mpya lakini umefika mahali umegota safarini, umeiacha NJIA KUU YA UTAKATIFU, umegeukia njia ya mauti, umeanza kutazama pornography, umeanza kusengenya, umeanza kutukana, umeacha upole wako na ukarimu wako, ndugu ukiendelea hivyo hivyo hautauingia ule mji Yerusalemu ya Bwana, usijidanganye na Dini yako ukadhani inatosha kukufikisha mbinguni, kwasababu biblia ilishasema..”
Mithali 14: 12 Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti”..Kumbuka kama ilivyosema..Pasipo huo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu…
Isaya 35: 8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, NJIA YA UTAKATIFU; WASIO SAFI HAWATAPITA JUU YAKE; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; WASAFIRIO, WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO.
Umeona biblia inasema watakaopita katika njia hiyo, ulimwengu utawaona ni wajinga, wataonekana kama watu wasiostahili kuwa katikati yao, wanawake waliokataa mitindo ya ulimwengu huu wataonekana washamba na wajinga, wanaume wasiokuwa walevi, wala waasherati, watu wanaoishi maisha matakatifu watadharauliwa, lakini hao ndio Mungu aliowachagua wapite katika njia ile KUU, Biblia inasema wajapokuwa ni wajinga machoni pa ulimwengu lakini hawatapotea katika njia hiyo.
Kumbuka ndugu, biblia imetuonya tufanane na wasafiri wenzetu wa Imani waliotutangulia, ambao walijikana kweli kweli, watu ambao mawazo yao yote yalikuwa ni mbinguni tu, kama tunavyowasoma katika
Waebrania 11: 36 “wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;
37 walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;
38 (WATU AMBAO ULIMWENGU HAUKUSTAHILI KUWA NAO), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.
39 Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;
40 kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi…”
Waebrania 11: 13 Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, NA KUKIRI KWAMBA WALIKUWA WAGENI, NA WASAFIRI JUU YA NCHI.14 MAANA HAO WASEMAO MANENO KAMA HAYO WAONYESHA WAZI KWAMBA WANATAFUTA NCHI YAO WENYEWE.
15 Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea.
16 Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji”.
Ndugu hawa watu walijikana nafsi zao kwasababu waliuona uzuri uliopo mbele yao, waliona furaha isiyokuwa na kifani kuingia katika ule mji, waliona ni heri maisha yao ya miaka 80 yasiwe ni kitu kulinganisha na miaka ya umilele inayokuja huko mbeleni. Ndugu kosa kila kitu lakini usikose mbingu, Biblia inasema wenye haki watang’aa kama jua, Mambo ambayo Mungu amewaandalia wampendao ni mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia, hakutakuwa na uchungu tena, wala kudharauliwa, watapewa miili ya utukufu wa ajabu, watatawala na Kristo Yesu kama wafalme na makuhani, milele na milele, tujitahidi tusikose huko.
Utajisikiaje unyakuo umepita na wewe umeachwa? Wenzako wamekwenda katika karamu ya mwanakondoo mbinguni na wewe umebaki?hapa duniani ukisubiria ziwa la moto?
Utajisikiaje??..Ifuate hiyo NJIA KUU LEO, kwa kumpa Yesu Kristo maisha yako kama hujafanya hivyo angali muda upo, ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa kwenye maji tele na kwa Jina la YESU KRISTO, upate ondoleo la dhambi zako (Matendo 2:38) na kisha utapokea kipawa cha Roho Mtakatifu kitakachokuwezesha kuwa mtakatifu ili uweze kuiendea hiyo NJIA KUU YA UTAKATIFU ili siku ile Uingie katika ile Yerusalemu mpya ya Bwana aliyowaandalia watakatifu wake.
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.