NA MIAKA ELFU NI KAMA SIKU MOJA

Biblia kwa kina No Comments

NA MIAKA ELFU NI KAMA SIKU MOJA

2 Petro 3:8 “Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja”.

Kuna msemo ambao unajulikana na watu wengi kwamba ”Mungu hachelewi wala hawahi” maana yake wakati sisi tunaona amechelewa/amekawia kumbe yeye anaona amewahi sana, na halikadhalika wakati tunaona amewahi sana.. kumbe yeye anaona amechelewa. Maana yake yupo kinyume na sisi.

Ni kwanini iwe hivyo. Ni kwasababu yeye ni Mungu na sio mwanadamu, mawazo yake yako mbali na mawazo yetu..

Isaya 55:8 Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA.

[9]Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.

Hivyo kwake yeye siku moja ni sawa na miaka Elfu na miaka Elfu ni sawa na siku moja. Bwana hakawii wala hawahi, anaweza akaja kabla ya wakati usiotarajia au akaja baada ya wakati usiotarajia.

Wakati wanadamu wanaona muda wako wa kuzaa umepita, au muda wa kubeba mimba bado, Mungu yeye anaona huo wakati ambao kwa mwanadamu haiwezekani..ndio wa kuzaa. Jifunze kwa Mariamu na Elisabeth.

Wakati tafiti za kisayansi zinasema mwanamke akishafikisha umri wa miaka 40 anakoma katika desturi ya kuchukua mimba hivyo hawezi kuzaa tena, lakini kwa Mungu hakuna kuchelewa wala kuwahi, wakina Sara, Elisabet na wengineo walizaa wakiwa na zaidi ya miaka hizo za wanasayansi, Sara alimzaa Isaka akiwa na miaka 90, Elisabeti naye alikuwa mzee amekoma katika desturi ya wanawake lakini alimzaa Yohana Mbatizaji. Kasome Mwanzo 18 & Luka 1.7)

Na sio kwamba hachelewi au hakawii tu, lakini pia Mungu anatenda hata jambo kabla ya wakati ambao tumejiwekea.. Mariamu alichukua mimba ya Mwokozi wetu Yesu kabla hata hajakutana na mwanaume.

Na sio katika hilo tu la kuzaa, hata na mambo mengine yote ni hivyo hivyo, ukiona umeomba Bwana hitaji fulani, na unaona imepita sasa zaidi ya miaka 10 au zaidi, usikate tamaa ukatoka kwenye imani, wala usiruhusu akili yako na mawazo ya wanadamu ikudanganye kuwa hilo jambo haliwezekaniki tena, we simama imara na usonge mbele kumtumainia Bwana, ukijua kuwa Bwana hakawii wala hawahi, siku moja kwake ni sawa na miaka elfu na miaka elfu ni sawa na siku moja. Na fahamu pia kuwa kila jambo lina kusudi lake, huwezi jua kwanini hilo jambo uliloliomba limekawia.. japokuwa kwa Mungu halijakawia, zipo sababu nyingi.

Lakini pia yapo mambo mengi ambayo Bwana anakufanyia/atakufanyia kabla hata ya wakati usioutarajia, tunapoona siku moja ni fupi sana kwetu Mungu kufanya jambo, tujue kuwa kwa Mungu ni kama miaka elfu, maana yake ahadi zake alizotuahidi anaweza kuzitimiza ndani ya siku moja… Kwahiyo hatupaswi kumkosea Mungu Imani, hata kama tumeona siku inakaribia kuisha na hatujapata kile tunachokitafuta, tufahamu kuwa Mungu anaweza kufanya jambo kubwa ndani ya siku hiyo hiyo moja kabla haijaisha yote, kwasababu kwake yeye ni kama miaka elfu.

Lakini, kama hujaokoka sawa sawa, kama bado unatanga-tanga huku na huku na kuufurahia ulimwengu, fahamu kuwa Bwana anaposema saa ya wokovu ni sasa na wakati uliokubalika ni sasa (2Wakorintho6:2), usidhani kwamba hayo maandiko yameandikwa tu ili tusome basi.

Fahamu kuwa saa ya wokovu ni sasa, ni wakati huu unaposoma ujumbe huu, ndio Bwana amekukutanisha na ujumbe huu ili uokoke leo na sio kesho, leo ondoa hayo mawazo yanayokuambia kesho utaokoka au siku fulani utaokoka tu, hayo ni mawazo ya ibilisi..hivyo usimpe ibilisi nafasi, fahamu kuwa siku moja ya Bwana ni sawa na miaka elfu, na miaka elfu ni sawa na siku moja.

Maana yake usione kuwa siku ulizopewa utii injili na uokoke ni nyingi sana…na kwamba bado una muda mbeleni, nataka nikuambie unajidanganya…na utakuja kujutia sana muda ambao umepewa ukachezea, ukaona hii dunia itakaa hivi hivi daima na wewe utadumu milele.

Fahamu kuwa masaa mawili mbele ni mengi sana kwa Bwana, lolote linaweza kutokea..si zaidi siku moja ambayo ni sawa na miaka elfu moja.

Zaburi 90:4 “Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita, Na kama kesha la usiku”.

  1. Hivyo, ni heri leo ukakubali kutii wito wa Mungu ambao unakuita utoke katika dunia ambayo hivi karibuni inaenda kuanguka.

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *