NA WANADAMU WAKAUNGUZWA MAUNGUZO MAKUBWA

Siku za Mwisho No Comments

NA WANADAMU WAKAUNGUZWA MAUNGUZO MAKUBWA

Ufunuo wa Yohana 16:8 “Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto.

[9]Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu”. 

Umewahi kuitafakari mwisho wa hii dunia itakuaje?

Biblia imeweka wazi kuwa hii dunia imewekwa akiba kuangamizwa kwa moto. Tunasoma

2 Petro 3:1 Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha,

[2]mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu.

[3]Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,

[4]na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.

[5]Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;

[6]kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.

[7] LAKINI MBINGU ZA SASA NA NCHI ZIMEWEKWA AKIBA KWA MOTO, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.

[8]Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.

[9]Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.

[10]Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.

Kama huamini biblia kuwa hayo yote ni kweli yatatimia, basi huwenda ukawa miongoni mwa viumbe vitakavyoteketea siku hiyo.

Biblia ilitabiri miaka 2000 iliyopita kuwa siku za mwisho watakuja watu wenye kudhihaki habari hizi za kurudi kwa MASIHI mara ya pili na mwisho wa mambo yote, watu hao biblia inasema WANAFUMBA MACHO YAO, kwasababu gani?

Kwasababu hawataki kusikia wala kutafakari mambo yaliyotokea zamani na mambo yanayokuja kuikumba hii dunia.

Hivyo wewe ambaye Bwana amekupa neema ya kufika mahali hapa na kukutana na ujumbe huu, Mungu anataka maisha yako leo yabadilike pale ambapo utaenda kutafakari kwa kina huu ujumbe na kuchukua hatua.

Sasa kabla hatujaendelea mbele na ujumbe wetu, hebu kwanza tuweke msingi kwa kutazama baadhi ya mambo yaliyotabiriwa na biblia na yakatimia kwa wakati wake, biblia ambayo ni Neno la Mungu liliowekwa katika maandishi..ilishatabiri kutokea kwa mambo kadha wa kadha kabla ya mwisho wa dunia, ambayo tukiziona hizo basi tujue ule mwisho umekaribia. Na mengi ya mambo hayo yamekwisha tokea na sisi tukashuhudia. Hebu tutazame baadhi ya mambo hayo yaliyotabiriwa kutokea kabla ya kurudi kwa Bwana Yesu.

Luka 21:8-11 Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao.

[9]Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi.

[10]Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme;

[11]kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.

Tuendelee kusoma..

Mathayo 24:23 Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki.

[24]Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.

Ni wazi kuwa tunaishi ukingoni kabisa mwa siku za mwisho, sisi wenyewe ni mashahidi kuwa hayo mambo yamekwisha timia siku nyingi, manabii wa uongo wametapaka kila kona, vita na tetesi za vita tunashuhudia ulimwenguni, matetemeko ya ardhi, tauni mbali mbali kama korona, Ebola, n.k tumeshuhudia kuanzia karne ya 20, maasi yameongezeka duniani mpaka watu wanabadili jinsia zao, na mambo mengine tu mabaya na ya kutisha yanafanyika hadharani, hii ni kutuonyesha kuwa mambo yote yaliyotabiriwa na biblia ni lazima tu yatimie kwa wakati kwasababu biblia ni Neno la Mungu..na Mungu sio mwanadamu hata aseme uongo.

Sasa tukishayajua hayo, biblia pia ilitabiri mambo mabaya na ya kutisha ambayo yataikumba hii dunia katika siku za mwisho baada ya UNYAKUO.

Unyakuo ni kitendo cha watakatifu wa Mungu kunyakuliwa juu mbinguni wakati wa parapanda ya mwisho, hili ni tukio ambalo lipo karibu sana kutokea.

Sasa baada ya tukio hilo la ajabu kupita, kulingana na kalenda ya biblia .. dunia hii itakuwa imebakiza muda wa miaka kama saba tu! Na kati ya miaka hizo, nusu yake yaani miaka mitatu na nusu itakuwa ni utawala wa shetani rasmi duniani..watu wote waliobaki hapa duniani watalazimika kumuabudu shetani kwa kupenda au kutopenda, na wale ambao watakataa watapitia dhiki kuu na baadaye watauawa. Na shetani hatakuja na kujitangaza kuwa mimi ni shetani ni lazima mniabudu.. hapana, atamtumia mtu wake ambaye atakuja kama mtu wa amani, na ataleta amani ya bandia.. hivyo watu wengi watampenda na watakubaliana na mfumo wake (chapa yake) pasipo kujua kuwa wameungana na shetani kwenda kwenye ziwa la moto. Ni kama tu leo watu wanavyoungana na shetani kupitia mifumo ya dini, na mawakala wake pasipo kujua..huku wakidhani wanaabudu Mungu mmoja kumbe wanamwabudu shetani.. ndivyo itakavyokuwa.

Sasa, baada ya huo utawala wa giza, miaka mingine mitata na nusu ya mwisho, mambo yataanza kubadilika ghafula, hiyo amani bandia ya shetani itaanza kutoweka, adhabu ya Mungu itanza kuachiliwa duniani, mambo kadha wa kadha ya kushangaza yataanza kutokea katika baadhi ya sehemu za dunia, baadhi ya mambo hayo tunasoma katika biblia..

Ufunuo wa Yohana 8:7 Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; THELUTHI ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea.

[8]Malaika wa pili akapiga baragumu, na kitu, mfano wa mlima mkubwa uwakao moto, kikatupwa katika bahari; THELUTHI ya bahari ikawa damu.

[9]Wakafa THELUTHI ya viumbe vilivyomo baharini, vyenye uhai; theluthi ya merikebu zikaharibiwa.

[10]Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya THELUTHI ya mito, na juu ya chemchemi za maji.

[11]Na jina lake ile nyota yaitwa Pakanga; theluthi ya maji ikawa pakanga, na wanadamu wengi wakafa kwa maji hayo, kwa kuwa yalitiwa uchungu.

[12]Malaika wa nne akapiga baragumu, theluthi ya jua ikapigwa, na THELUTHI ya mwezi, na theluthi ya nyota, ili kwamba ile theluthi itiwe giza, mchana usiangaze theluthi yake, wala usiku vivyo hivyo.

Umeona hapo, ni theluthi ya dunia tu ilipigwa kwa mapigo hayo, lakini baadaye mwishoni mwa miaka hiyo mitatu na nusu, haitakuwa tena theluthi.. dunia yote itapigwa. Tukisogea mbele kidogo tunasoma kuna vitasa saba ambayo kila kitasa kilipomiminwa tunaona kilichotokea duniani. Ni mambo ya kutisha na ya kuogopesha sana kiasi cha kutetemesha, hutatamani kabisa kuwepo wakati huo.(Kumbuka haya sio mambo ya kutungwa bali ni unabii wa Mungu ambayo ni lazima tu itimie kama ilivyo kwa wakati wote)

Ufunuo wa Yohana 16:1 Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi.

[2]Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake.

[3]Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa.

[4]Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu.

[5]Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi;

[6]kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili.

[7]Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.

[8]Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto.

[9] WANADAMU WAKAUNGUZWA MAUNGUZO MAKUBWA, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu.

[17]Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa.

[18]Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo.

[20]Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena.

[21]Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno.

Unaelewa maana ya vitasa, vitasa ni mabakuli ambayo yamejaa ghadhabu ya Mungu, ndiyo itakayomiminwa siku hizo. Kumbuka hizo siku zimekaribia sana. Ukisoma hapo juu anasema..

15 (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)”

Ndugu yangu, hayo mambo yapo mbioni kuujilia ulimwengu, ni unyakuo tu ndio tunasubiria na wenyewe umekaribia sana. Hebu kaa kwa utulivu..tumia muda kutafakari hayo mapigo ya ghadhabu ya Mungu vizuri.

Hebu tafakari hiyo Neno “wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa” hayo maunguzo ni ya namna gani? Hebu tafakari hili jua tu saivi ambalo lipo mbali linakuunguza namna hiyo, sasa itakuwaje siku hiyo itakapopewa kuunguza wanadamu, ni maunguzo makubwa mno..watu watalia na kusaga meno, hebu tafakari unachomwa na jua kali huku ukiwa na majipu mwili mzima na hakuna maji!!.

Hebu tafakari hiyo mvua ya mawe kama talanta, unafahamu ukubwa wa talanta.. talanta moja ni sawa na kilo 30, hayo ni mawe, kuna mtu atapona kweli?

Ndio maana.. biblia imeonya juu ya watu wanaodhihaki na kuitamani hiyo siku kuu ya Bwana.

Amosi 5:18 Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya BWANA; kwani kuitamani siku ya BWANA? Ni giza, wala si nuru.

[19]Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma.

[20]Je! Siku ya BWANA haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga.

Sasa ufanyaje ili kuepuka hiyo ghadhabu na hasira ya Mungu inayokuja.

Hakuna njia nyingine ya kuokoka..isipokuwa tu ile iliyokwisha kuwekwa na Mungu mwenyewe, nayo ni kumuamini mwanawe mpendwa Yesu Kristo na kutubu dhambi kwa kumaanisha kuziacha kabisa.. baada ya hapo unaenda kubatizwa kwa maji mengi na kwa jina lake yaani jina la Yesu. Ndivyo biblia inavyosema.

Matendo ya Mitume 2:37 Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

[38]Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

Unaelewa maana ya kutubu, kutubu sio kuomba msamaha tu, hiyo inakuja baada ya kutubu, kutubu ni kuacha njia za ulimwengu na matendo yote ya giza kama uasherati, ulevi, wizi, uvaaji mbaya wa vimini na masuruali ikiwa we ni mwanamke, mapambo ya kidunia ikiwemo mekaups, nywele bandia, kucha bandia, na vitu vyote vya kidunia unamua kuchoma moto, ikiwa ni miziki ya kidunia unavuta zote kwenye simu yako, ikiwa ni magemu na filamu zenye maudhui ya uasherati unavuta mara moja bila kubakiza hata moja, unamgeukia Yesu unasema mimi na ulimwengu basi, mimi na disco mwisho, unaachana na makundi yote mabaya bila kutazama tazama pembeni, biashara zote haramu unaacha hata kama inakulipa Yesu atakupa nyingine, Hiyo ndio maana ya kutubu.

Je! Upo tayari kutubu dhambi na kumgeukia Yesu leo au utaendelea kuishi maisha ya dhambi mpaka siku hiyo ya kutisha ikukute! Kumbuka hata isipokukuta ukiwa hai, huwezi tu kupona..maana ukifa na dhambi moja kwa moja unaenda kuzimu ambapo huko hakuna afadhali hata kidogo. Kwahiyo suluhisho pekee ni kumpokea tu YESU na kuacha dhambi na mambo yote ya kidunia.

Ikiwa leo upo tayari kufanya uamuzi wa kumgeukia Yesu Kristo na unahitaji msaada, tutafute kwa namba uzionazo chini ya makala hii, nasi tutakuongoza sala ya toba na kukupa muongozo wa kufuata. Lakini hata sasa kama umeanza kutubu ndani ya moyo wako kwa kujutia maisha unayoyaishi.. tayari umefungua mlango wa Yesu kuingia kwako, kilichobaki tu ni wewe kudhihirisha toba yako kwa vitendo na kutafuta ubatizo.

Ubarikiwe sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *