Mawaa ni kasoro au dosari yoyote inayofanya kitu fulani kipoteze sifa yake iliyo nzuri.
Kwa mfano mtu mwenye uso mzuri akipata jipu kwenye shavu tutasema ana mawaa kwa sababu lile jipu limeharibu uso wake…
Au mtu aliyenunua bati kwa ajili ya kuezekea nyumba yake lakini bati lile likawa limetoboka hapo tunasema lina mawaa. Lakini pia shati jeupe likipata doa la rangi nyingine tayari linakuwa na mawaa.
Katika maisha ya kiroho hatutakiwi kuwa na mawaa, katika vifungu vifuatavyo tunaona jinsi ambavyo Mungu wetu hataki kuona kasoro yoyote ndani ya kanisa..
Wakolosai 1:21 “Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa;22 katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama”
Basi ukiwa mkristo uliyeokoka tambua kuwa ni wajibu wako kuishi maisha matakatifu yasiyo na dosari. Wapo watu wanasema tumeokolewa kwa neema na hivyo wanaamua kuishi vile wanavyopenda wao, mfano mtu anaifanya kazi ya Mungu lakini anaishi na mume au mke wa mtu, mtu wa namna hii ana mawaa hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu
Mwingine ni mtoaji mzuri wa zaka, mwanakwaya, tena kiongozi wa vijana lakini bado anaangalia picha mbaya mtandaoni, unafunga na kuomba kila wakati upo kanisani lakini bado unapokea rushwa kazini, haya yote ni mawaa.
Kwa hiyo inatupasa tuwe kanisa ambalo Kristo analitaka lisilo na mawaa wala lawama, hapo ndipo tutapata nafasi ya kuingia katika ufalme wa Mungu, vifungu vifuatavyo vinaelezea juu ya hili.
1Timotheo 6:13 “Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato,
14 kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo”.
Yohana 1:27 “Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa”
Tazama na,
Waebrania 9:14
2 Petro 2:13
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
- Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.