Ngazi saba ambazo mkristo lazima azipande ni zipi?

Maswali ya Biblia No Comments

Shalom, karibu tujifunze Maneno ya Uzima

Swala la kuokoka peke yake halitoshi mbele za Mungu, kuna ngazi 7 ambazo ni lazima mtu wa Mungu azipande ili Mungu auone ukamilifu wako unapokuwa hapa duniani. Inatakiwa tuende mbele zaidi ya kuokoka na kubatizwa hatutakiwi tubaki hapo kwa sababu hatutakuwa na ushuhuda wowote na pengine tukafa kiroho.

Mtume Petro anatuandikia hayo mambo saba ambayo mtu anatakiwa kuyafanya kwa bidii baada ya kuokoka.

2Petro 1:5 “Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, …..,


1.WEMA


Hili ni jambo la kwanza ambalo mkristo anatakiwa kulifanyia kazi, Yatupasa kusimama katika imani huku tukitenda mema kwa watu wanaotuzunguka. Hili ni tendo linaoashiria kujali, kuwathamini na kuwaheshimu wengine pamoja na kuwa waaminifu.


Kama watu wasiomjua Mungu hawana heshima kwa wengine au hawawathamini wengine basi sisi haitupasi kufanya kama wao, hapo hakuna wema. Ikiwa una mamlaka kazini kwako na unaona wengine hawawatendei vyema wafanyakazi walio chini yao hawalipi mshahara mzuri au hata kuwaongezea basi hiyo si sababu ya wewe kuwaiga, watendee wema wape misharaha yao kwa wakati na hata ikibidi kuwaongeza,

Tuangalie mfano wa Bwana Yesu kwa wale watu waliopelekwa shambani saa 11 na wengine walikuwa wameshaenda tangu asubuhi, ulipofika wakati wa kupokea mshahara wale walioenda asubuhi walitaka walipwe zaidi ya wengine waliochelewa,

Bwana anasema..

Mathayo 20:14 “Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.

15 Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa MWEMA”

Huu ndio wema tunaopaswa kuuchukua na kuuiga…

Tunasoma habari za mtu mmoja aitwae Barnaba, huyu alikuwa na ushuhuda mzuri wa kuwajali watu wengine hasa wale waliokataliwa na alifikia hatua ya kuitwa mwana wa faraja. Na sisi pia yatupasa kuwaonyesha watu wema wetu, maana hili ni moja ya tunda la roho mtakatifu kama tunavyosoma, Wagalatia5:22 (utu wema)..

Warumi 12:21 “Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema”.

2.MARIFA

Biblia inaendelea kusema..

“ 1:5..na katika wema wenu maarifa,”


Maarifa anayozungumia Petro sio ya duniani ni maarifa ya kumjua Mungu. Wakristo wengi tumekosa maarifa ya kiMungu na tunaangamia kwa sababu hatujui jinsi Mungu anavyotenda kazi kwa wakati na majira gani na wala hatujui yatupasayo kufanya….

Mfano kutokujua kuna nguvu inayowapoteza watu ambayo imeachiliwa na Mungu mwenyewe ili iwapotoshe wasiotaka kuitafuta kweli na nguvu hiyo ipo kwa manabii wa uongo ambao wafanya miujiza aliyoifanya Mungu. Lakini pia watu hawana maarifa juu ya neema ya ya wokovu, watu hawajui kwamba hii neema haitadumu milele kwa sisi watu wa mataifa kuna wakati itaondolewa na kupelekwa Israel na sisi mataifa mengine tutakuwa kama mafarisayo na masadukayo. Na ndio sababu watu wanachukulia swala la ukristo kwa mzaha wanafikiri bado wanayo nafasi siku zote…


Hivyo yatupasa tujifunze maneno ya Mungu kila siku, tunaye Roho Mtakatifu atatusaidia kuyachunguza maandiko na kuyaelewa na tutajua siri na mipango ya Mungu katika wakati tunaoishi. Hii ni hatua ya pili hivyo hakikisha unapata maarifa ya Mungu ya kutosha.

3.KIASI

“1:6 na katika maarifa yenu kiasi”,

Baada ya kupata maarifa yatupasa kuwa na kiasi. Wapo watu wana maarifa na utu wema lakini bado hawana kiasi hawawezi kujizuia katika mambo fulani na baadae hujikuta wameanguka dhambini kutokana na hayo mambo..

Utakuta mtu wa Mungu muda wote anawaza kuhusu kazi zake anakosa hata muda na kuongea na Mungu. Muda aliopaswa kuwa faragha na Mungu anasema amechoka anaahirisha na kusema nitaomba kesho, nitafanya siku nyingne. Na wengine hupoteza muda wao kwa mambo yasiyo na faida kwao kama kuangalia Tv, kuchati, kuperuzi katika kitandao ya kijamii na kuangalia mambo ya kidunia lakini mtu huyo anatumia mda mchache sana katika mambo ya kiroho. Neno linasema, sisi tulio wa mchana tuwe na kiasi ili tupate muda wa kuwa karibu na Mungu. (1 Wathesalonike 5:8)

4.SABURI

“1:6…Na katika kiasi chenu saburi


Tukishajifunza kuwa na kiasi yatupasa tuwe na saburi pia, Saburi maana yake ni uvumilivu au uwezo wa kustahimili jambo katika imani. Tusipokuwa na uvumilivu hasa nyakati za majaribu imani yetu haiwezi kwenda mbele. Mara nyingi watu huikana imani kwa sababu ya njaa, kukosa ajira, mateso anayopata kutoka kwa watu…

Kuna wakati mitume walifungwa gerezani na kupigwa lakini bado hawakuacha kuieneza injili kwa watu. Tusikubali kukosa saburi kwa ajili ya masumbufu ya duniani ambayo ni ya muda kitambo tu ili tuweze kufika katika viwango ambavyo Mungu anatarajia tuvifikie, kwa kukosa uvumilivu wakristo wengi wamekwama na kushindwa kusonga mbele hasa pale vile walivyotarajia hawakuviona kwa wakati walioupanga na mwisho wa siku wanakata tamaa. Saburi ni mpango wa Mungu, hivyo tunapaswa kuwa na saburi..

Warumi 5:3 “Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;

4 na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;


5.UTAUWA

“1:6…na katika saburi yenu utauwa


Utauwa ni tabia ya uungu. Mungu wetu ni mtakatifu na sisi kama watu wake yatupasa tuwe watakatifu, ni lazima kuikataa dhambi na mambo yote mabaya na kuishi maisha matakatifu yenye kumpendeza Mungu.

1Petro 1:16 “kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu


Ili tuweze kuishi maisha matakatifu inatubidi tuwe waombaji na tuwatangazie wengine habari za wokovu, hivyo ndivyo alivyokuwa Bwana Yesu. Ikiwa hatuombi basi hatuwezi kuishi katika utauwa ambao Bwana Yesu anautaka.

6.UPENDANO WA NDUGU

Hii ni hatua inayofuata baada ya utauwa, huwezi kufikia hatua hii pasipo kupitia zile nyingne. Upendo tunaozungumzia ni upendo wa ndugu katika Kristo, sisi kama wakristo tunatakiwa tupendane sisi kwa sisi. Aina hii ya upendo imekuwa vigumu kuonekana kati ya wakristo, wengi husengenyana, huumizana wao kwa wao kama vile hawapo chini ya Bwana mmoja. Yatupasa kujitafakari na kuacha vitendo hivyo maana jambo hili halihitaji maombi bali bidii ya kila mmoja wetu..

1Petro 1:22 “Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo”.

7.UPENDO


1:7…na katika upendano wa ndugu, upendo”.

Upendo unaozungumzia hapa sio ule upendo wa ndugu, huu ni upendo wa ki-Mungu. Mtu akiwa na upendo huu anakuwa karibu sana na Mungu pia anamjua Mungu zaidi. Huu ni upendo usio na sababu haungalii kama fulani kanitendea vizuri basi na mimi nimtendee vizuri, hapana. Wakati Mungu anamtoa mwanae wa pekee kwa ajili yetu hatukuwa tumefanya jambo lolote zuri ni upendo wake tu kwetu. Upendo huu asili yake ni mbinguni haujaanzishwa na mwanadamu wala mnyama. Ni upendo tunaouona katika….

4 Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;

5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; gauges Abu mabaya;

6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;

7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.

8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.

Hapa ndipo mwisho wa kila kitu. Mtume Petro anasema tukiyafikia hayo yote hatutakuwa watu wavivu wasio na matunda lakini pia hatutajikwaa ovyo katika mambo ya imani bali tutakuwa na uwezo wa kujua mambo yajayo…

2Petro 1:8 “Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.

9 Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani.

10 Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.

11 Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo”


Basi kwakuwa tumeyafahamu hayo tufanye tathimini tujue hatua tuliyopo na kisha tufanye bidii kutendea kazi hatua ambazo bado tumekuwa walegevu, tusiishie kusoma makala peke yake tuchukue hatua.


Bwana wetu Yesu Kristo akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *