
Nikatambua na tazama Siye Mungu aliyemtuma.
Nehemia 6:11 “Nami nikasema, Je! Mtu kama mimi nikimbie? Naye ni nani, akiwa kama nilivyo mimi, atakayeingia hekaluni ili kuponya maisha yake? Sitaingia.
[12]NIKATAMBUA, NA TAZAMA, SIYE MUNGU ALIYEMTUMA; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri.
[13]Kwa sababu hii aliajiriwa, ili mimi niogope, nikafanye hivyo na kutenda dhambi, kisha wao wawe nazo habari mbaya, ili wanishutumie”.
Ikiwa wewe ni mwamini uliyesimama imara katika imani na unamatumaini ya kuingia Yerusalemu mpya, basi yakupasa uwe makini sana katika nyakati hizi tunazoishi.
Tunaishi katika kipindi cha hatari ambacho hakijawahi hata kutokea katika vizazi vyote vya nyuma, ambacho kina mchanganyiko mkubwa wa MANABII WA UONGO NA MANABII WA KWELI.
Hivyo ni lazima uwe na jicho la TAI ili uweze kutambua njia ya kweli na njia ya upotovu.
Ukisoma kitabu cha Ufunuo, utaona wapo wale wenye uhai 4, wanaosimama mbele ya kiti enzi cha Mungu, mmoja akiwa na uso kama wa Simba, mwingine wa Ndama, mwingine kama wa mwanadamu na Mwingine kama wa Tai (Ufu 4:7).
Sasa hizo nyuso zao na mionekanayo yao sio urembo tu, hapana bali zilikuwa zinafunua nguvu za Roho Mtakatifu katika nyakati tofauti tofauti za kanisa..Sasa mwenye uhai wa kwanza hadi yule wa Tatu, walifanya kazi kwa vipindi vya makanisa 6 ya mwanzo, kwa urefu wa Habari hiyo fungua hapa >> UFUNUO: Mlango wa 4
Lakini yule mwenye uhai wa 4 ambaye ndiye mwenye uso wa Tai, alianza kutenda kazi katika kanisa la 7 na la mwisho lijulikanalo kama Laodikia, ambalo ndio tunaishi mimi na wewe, na kanisa hili lilianza mwaka 1906, (hilo linajulikana na wanazuoni wote na wana theolojia wote duniani, sio jambo la kutengeneza)..
Sasa kama tulivyosema, Sio kwamba huyo mwenye uhai wa 4 ndio anayetenda kazi hapana, bali Ni Roho ya Mungu yenye tabia ya Tai ndio iliyoachiwa kwa kanisa la Mungu tangu huo wakati na kuendelea (Mwaka 1906- Pentekoste ya mwisho ilipoanza)
Hivyo mimi na wewe tunaishi katika Upako huo wa Roho ya Tai.
Sasa ni kwanini iwe ni Tai na sio wale wengine, labda simba, au ndama, au mwanadamu?.
Ni kwasababu kanisa la sasa hivi linahitaji wakristo wenye jicho la TAI,..Kumbuka tai ni ndege anayeona tokea mbali kuliko kiumbe kingine chotechote duniani, Tai anaona kwa umbali ambao wewe mwenyewe huwezi kumwona angani. Anaweza kuona vitu vya mbali sana, vidogo sana,..tofauti na ndege wengine kama kuku, kuku yeye anaona hapa chini tu, lakini kile kinachotokea maili mbili mbele hawezi kukiona.
Hivyo jicho hilo la Tai ni jicho la kinabii, Kwamba wakristo wote waliopo duniani leo hii Roho hii inapaswa iwepo juu yao, ili wawezi kuushinda ulimwengu huu wa sasa, vinginevyo watakachukuliwa tu maji..Na ndio maana kusema tu Umeokoka, hilo halitoshi kwa majira haya..Ni lazima uwe na jicho la kinabii.. Na jicho la kinabii sio kuona maono usiku, wala wachawi, wala kutabiri…Bali ni utashi wa kujua wakati tuliopo, na kuona mambo yajayo, ambayo bado hayajafika yatakayoupata ulimwengu, na hivyo kuchukua tahadhari mapema.
Mungu alijua kabisa wakati huu udanganyifu utakuwa mkubwa duniani, na watu watamsahau Mungu kupindukia kama alivyosema watu watakuwa wa kupenda anasa kuliko kumpenda Mungu (2Timotheo 3:4), alijua kabisa kutatokea mapinduzi makubwa ya kiteknolojia, alijua kabisa kutakuwa na mwingiliano mkubwa wa watu na wa-kiutamaduni katikati ya mataifa, alijua kabisa dini nyingi zitaongezeka duniani, kiasi kwamba mpaka sasa duniani zipo dini Zaidi ya 4,300, ukristo ni mmojawapo na madhehebu yasiyoweza kuhesabika.
Alijua kabisa lile wimbi kubwa la makristo wa uongo, na manabii wa uongo, alilolitabiri zamani halitatokea wakati mwingine wowote, bali katika wakati wetu huu wa siku za mwisho.
Alijua kabisa ile siri ya kuasi itakuwa inatenda kazi kwa nguvu, katikati ya ukristo, kiasi kwamba watu wengi watazombwa na nguvu hiyo..
Na ndio maana katika kizazi hichi chetu aliiachilia Roho ya Tai, Ili kukabiliana na udanganyifu uliopo sasa hivi. Na ni lazima kila mtu awe nayo, kwasababu ni kwaajili yetu.
Hili ndilo lile jicho ambalo Mtumishi wa Mungu Nehemia alikuwa nalo, mpaka akaweza kutambua hila za maadui zake waliokuwa wanamjia kwa kivuli cha manabii wa uongo.
Na sisi kama wateule wa mbinguni hatuna budi kuwa na jicho la TAI, ili tuweze kutambua hila za ibilisi.
Tunapaswa tuchukue tahadhari kubwa zaidi kuliko hata za watakatifu waliokuwa wanaishi nyakati za kale kabla yetu, kwasababu biblia pia inasema shetani angali akijua kuwa muda wake ni mchache anafanya juu chini awaangushe wengi kwa njia yoyote ile. Mkristo ni kuwa makini huu sio wakati wa kuamini kila “roho” inayodai kuwa ni ya Mungu, biblia imetuonya na kutuambia,
1Yohana 4:1 “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani”
Na pia Bwana Yesu alisema..
Mathayo 7.15-23 “ Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.
16 Mtawatambua kwa MATUNDA YAO. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?
17 Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya.
18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.
Sasa tutawatambuaje kama hatuna hili jicho la kuona mbali.
Na jicho hili hatupati kwa kuombewa, hapana, tunapata kwa kuzama kwenye wokovu wa kweli na kuwa msomaji wa NENO na muombaji wa kina.
Jiulize Wewe unayejiita mkristo tangu ulipoamini, maisha yako ya kiroho yamesonga mbele kiasi gani. utakuwaje mkristo halafu biblia husomi!?? sasa utawatambuaje manabii wa uongo au manabii wa ukweli kwa namna hiyo watakapokujia na mafundisho yao??. Utakuwa unapelekwa na kila upepo unaokuja wa elimu yoyote. Maana njia pekee ya kumpima nabii wa uongo au Nabii wa ukweli ni kwa NENO TU!. Na sio kitu kingine.
Jijengee kila siku tabia ya kusoma NENO na kuomba. Hizi ni nyakati za hatari tunaishi zile zilizotabiriwa kuwa watatokea manabii na makristo wengi wa uongo nao watawadanganya wengi yamkini hata walio wateule. Kumbuka ni wateule ndio wanaozungumziwa hapo kuwa wanaweza wakadanganywa sasa jiulize wewe ambaye sio mteule utaonekania wapi? wewe ndio hautaelewa chochote kinachoendelea utaishia kuwashangilia na kuwasifia kama Bwana Yesu alivyotabiri juu ya manabii wa uongo.
Tunaishi katika kizazi kile alichokisema Bwana cha kuzuka kwa makristo na manabii wengi wa uongo, wanaohubiria watu injili nyingine, na Yesu mwingine, ambaye hakuhubiriwa na mitume. Mitume walihubiri watu watubu, wakabatizwe kwa jina la Yesu kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zao na wapokee Roho Mtakatifu. lakini wao hilo halina maana sana kwao, unaweza ukawa na Yesu tu(umeokoka) hata ukiwa unavaa nguo za nusu uchi,unapaka wanja,lipstick, unaabudu sanamu, n.k. Mungu haangalii mavazi anaangalia moyo.
Biblia pia inasema Yesu ndiye njia kweli na uzima, wao wanasema zipo njia nyingi za kumfikia Mungu kipimo ni upendo tu, unaweza ukawa dini nyingine na ukaenda mbinguni bila hata kumwamini Bwana Yesu, Injili zao siku zote ni za kumfariji mtu katika hali ya dhambi aliyopo. Hazilengi kumwelekeza mtu mbinguni, bali zinalenga kumwelekeza mtu kufanikiwa tu katika mambo ya mwilini, hazihubiri hukumu inayokuja kwa watu ambao wapo kwenye dhambi zinafundisha mtu ambaye hajafanikiwa ndio kipimo halisi cha kulaaniwa na Mungu..n.k.
Hizi zote ni roho za kunguru zinazotangulia kudanganya watu wa kweli wa Mungu.
Lakini tunazitambuaje? Ni kuwa na jicho la TAI (Roho Mtakatifu katika ujazo wote), ambayo tunaipata kwa kuamua kuzama ndani ya Yesu kweli kweli.
Hivyo ndugu hizi ni siku za mwisho, JE! UMEOKOLEWA!,. biblia inasema Roho Mtakatifu ndio Muhuri wa Mungu , na wote wasio na Roho wa Mungu hao sio wake(warumi 8:9).
TUBU sasa mgeukie Yesu Bwana aliye mkuu wa uzima wako akuokoe na akupe jicho la kutambua hila za shetani.
Ubarikiwe sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.