SIKU YA BWANA KULIPISA KISASI KWA ADUI ZAKE INAKUJA.

Siku za Mwisho No Comments

SIKU YA BWANA KULIPISA KISASI KWA ADUI ZAKE INAKUJA.

Nahumu 1:2 “BWANA ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; BWANA hujilipiza kisasi, naye ni mwingi wa hasira; BWANA hujilipiza kisasi juu ya adui zake, huwawekea adui zake akiba ya hasira”.

Adui za Bwana ni mashetani na wafuasi wake wote. Yaani marafiki wote wa dunia hii, kwa kuwa biblia inasema…

Yakobo 4:4 “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu”.

Kitendo tu cha kuipenda dunia, na mambo yake, tayari umefanyika kuwa adui wa Mungu. Mtu akipenda anasa, akipenda uzinzi, akipenda fashion, akipenda starehe za ulimwengu huu, kama miziki, ushabiki wa mipira, ulevi, ukahaba, wizi, utapeli, tamaa za fedha, tamaa mbaya ya vitu vya kiulimwengu vinavyopita kama magari, nyumba, kiasi kwamba unaweza kufanya chochote ili uvipate n.k Mtu huyo tayari kashafanyika kuwa Adui wa Mungu.

1Yohana 2:15 “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

Kumbuka ndugu/Dada siku ya kisasi ya Bwana ipo karibu, siku hiyo Bwana atalipa kisasi kwa adui zake wote wakimo wale wanaosema wanampenda Mungu na huku mioyo yao imeshikama na dunia, wanaosema hawazini lakini ndani ya mioyo yao kumejaa tamaa na uchafu wa kila namna.

Siku hizo za kutisha Bwana Yesu aliziita siku za mapatilizo, alipokuwa pale katika milima ya Mizeituni akiwaleza wanafunzi wake mambo yatakayotokea katika siku za mwisho.

Luka 21:22 “Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.”.

Unaona? Yote yaliyoandikwa ni lazima yatimie, kisasi Bwana alichosema atalipa ni lazima kije tu, maovu yanayoendelea sasa hivi duniani, mauaji, ubakaji, uabuduji sanamu, uchawi, uzinzi, n.k. yote Bwana ni lazima ayapatilize kabla ule mwisho haujafika.

Ezekieli 7: 5 “Bwana MUNGU asema hivi; Ni jambo baya, JAMBO BAYA LA NAMNA YA PEKE YAKE; ANGALIA, LINAKUJA.

6 Mwisho umekuja, mwisho huu umekuja; unaamka ukupate; angalia, unakuja

7 Ajali yako imekujia, wewe ukaaye katika nchi hii; majira yamewadia, siku ile inakaribia; siku ya fujo, wala si ya shangwe milimani.

8 BASI HIVI KARIBU NITAMWAGA GHADHABU YANGU JUU YAKO, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; NAMI NITAKUPATILIZA MACHUKIZO YAKO YOTE.

9 Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, napiga”.

Siku hizo Bwana anasema hakutakuwa na huruma, watu watalia na kujutia na kutubu lakini hakuna atakayesikia, mpaka ghadhabu ya Mungu ya mwisho itakapomalizwa kumwagwa duniani. Na Bwana anasema ni HIVI KARIBUNI. Wapo watu wanadhani mwisho bado siku nyingi. Ni jambo la kutisha sana kujikuta umebaki siku ile, kwasababu ni lazima Mungu apatilize uovu wote, kwa watu wote wanaokufuru leo, na kuutukana msalaba.

Waebrania 10:28 “Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.

29 Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?

30 Maana twamjua yeye aliyesema, KUPATILIZA KISASI NI JUU YANGU, MIMI NITALIPA. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake.

31 NI JAMBO LA KUTISHA KUANGUKA KATIKA MIKONO YA MUNGU ALIYE HAI.”

Swali: Je! Wewe ni Rafiki wa Mungu?.. au Adui wa Mungu?… Kama bado unaupenda ulevi, uasherati, fashion, anasa, wizi, matusi, ni mshabiki wa mipira na mambo mengine yote ya uliwemwengu huu, ni Adui wa Mungu bila hata kutamka kwa kinywa chako. Kama hujampokea Kristo leo hii ni siku yako, hapo ulipo tubu! Kwa kumaanisha kuacha dhambi zako, na pia tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa Jina la Yesu, kulingana na Matendo 2:38, na Roho Mtakatifu atakufanya rafiki wake wa kweli na wa kudumu, na utakuwa umeepuka kisasi cha Mungu.

Bwana akubariki.

Maranatha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *