SIMAMA KWA MIGUU YAKO.

Uncategorized No Comments

SIMAMA KWA MIGUU YAKO.

Ezekieli 2:1 “Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe.

[2]Naye aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami.”

Upo umuhimu mkubwa wa wewe kusimama kwa miguu yako mwenyewe hasa katika zama hizi za uovu. Ninaposema kusimama mwenyewe kwa miguu yako..ninamaanisha kuwa na mahusiano yako binafsi na Mungu.

Wapo watu ambao wanasimama kwa miguu ya watu wengine, wanasimama kwa miguu ya nabii, anasimama kwa miguu ya mchungaji, Mtume n.k, ni hatari sana kusimama kwa miguu ya mtu mwingine ilihali una miguu yako mwenyewe. Na leo Mungu anakuambia simama kwa miguu yako.

Dada/Kaka simama mwenyewe leo kwa miguu yako ili Mungu aseme na wewe, acha kusubiria tu mpaka jumapili ndio ukasikie Neno, acha kusubiria tu ratiba ya maombi itangazwe na mchungaji, kuanzia leo anza kumtafuta Mungu mwenyewe bila kusukumwa sukumwa, anza kujiwekea ratiba ya maombi na mifungo binafsi, anza kujisomea biblia wewe mwenyewe pasipo kusubiria kukumbushwa na mtu.

Unataka kupokea nguvu za Mungu ili uendelee mbele katika wokovu, simama kwa miguu yako. Unataka kujazwa Roho Mtakatifu ili ufurahie wokovu na utakatifu usiwe mzigo kwako..kanuni ni hiyo kusimama kwa miguu yako. Bwana alisema Baba atawapa Roho Mtakatifu wale wamuombao na sio wale waombewao.

Luka 11:13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?

Kwahiyo amka hapo ulipolala..na simama kwa miguu yako mwenyewe..anza kuwa muombaji tena wa masafa marefu, anza kuwa na desturi ya kusoma biblia kila siku, anza kufunga na kukesha kila week..na hakika utaona nguvu za Mungu zikianza kushuka juu yako, utaanza kupanda viwango. Ukifikia hapo, nakuambia shetani na mapepo yake watakuwa wanakukwepa kila wakikutana na wewe. Hofu zote zitakimbia kabisa mbali na wewe, hata ikija dhoruba ya namna gani haitakushutua hata kidogo, Na halikadhalika kuishi maisha ya utakatifu itakuwa ni kawaida kwako. Hiyo ndio faifa ya kusimama kwa miguu yako mwenyewe katika imani.

Leo hii unasema umeokoka, lakini bado unasumbuliwa na hofu za wachawi na majini, unashindwa na tamaa za mwili, unahangaika huku na huku kutafuta msaada, sio vibaya kufanya hivyo, lakini kuna vitu ambavyo Mungu hawezi kuachilia kwako mpaka usimame mwenyewe kwa miguu yako, na pale unapodhubutu kusimama kwa miguu yako..ndipo Bwana naye atakusaidia kusimama imara kama Ezekieli..yeye alikuwa na hofu ya kwenda kusema maneno ya Mungu..lakini aliposimama kwa miguu yake..akapokea nguvu ya ziada..na baada ya hapo hakuogopa tena mtu yoyote..hata wakati alipofiwa na mke wake yeye hakutikisika aliendelea mbele kwasababu alishapokea nguvu ya ziada. Na wewe leo ukisimama mwenyewe kwa miguu yako..nataka nikuambie kuna nguvu ya ziada utapokea kutoka kwa Bwana, hiyo hofu ya kushuhudia habari njema za wokovu kwa wengine itaondoka kabisa..we simama tu kwa miguu yako, usitazame mtu mwingine.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *