
SULIBISHA MWILI WAKO KWA BWANA.
Wagalatia 5:24 “Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
[25]Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho”.
Siku zote fahamu kuwa adui wa kwanza wa mtu ni MWILI wake na wala sio shetani.
Shetani anautumia mwili wako kukushawishi utende dhambi.
Hivyo ukiruhusu mwili wako ukutawale, mwisho wako utaangukia tu kwenye dhambi na dhambi mwisho wake ni mauti.
Kwahiyo huo mwili wako fahamu kuwa ndiye adui wako wa karibu, ukiendekeza katika tamaa zake mwisho wake utakusababishia mauti kwasababu nia yake ni hiyo.
Warumi 8:5 Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho.
[6]Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani.
[7]Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii.
[8]Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.
Hivyo ukitaka kwenda kumuona Mungu katika mwaka huu kwa viwango vingine ni sharti uamue kuusulubisha mwili wako.
>Ukitaka kushinda dhambi yoyote ile na kuishi maisha ya utakatifu, huna budi kuusulibisha mwili wako.
>Vile vile ukitaka kukua kiroho na kuzaa matunda ni lazima uusulibishe mwili wako.
Sasa nini maana ya kuusulibisha mwili na tunausulibishaje?
Kusulibisha mwili maana yake ni kuutesa, kuunyima raha yake, raha ya mwili ni ipi?
Raha ya mwili ni usingizi, vyakula, fashions, anasa n.k
Sasa haimaanishi tusilale usingizi, au tusile vyakula kabisa. La hasha, lakini kusulibisha mwili maana yake unapangia hayo mahitaji ya muhimu na sio mwili unakupangia.
Unalala kwa kiasi, una kula kwa kiasi, maana yake ni lazima uwe na vipindi vya kuunyima mwili usingizi (mikesha), unakuwa na vipindi vya kuunyima mwili chakula (mifungo)
Mtume Paulo ambaye alikubali kuusulibisha mwili wake ili afanikiwe kiroho anasema..
1Wakorintho 9:27 “BALI NAUTESA MWILI WANGU na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa”.
Kumbuka kuutesa mwili kunakozungumziwa hapa si kujiumiza kwa viboko na mapigo… bali ni kuuzuia mwili kupata vitu viupendavyo, ili makusudi kutimiza mapenzi ya MUNGU.
Na mwisho kumbuka, kujizua kufanya dhambi kama uzinzi, ulevi, sio kuutesa mwili, bali ndio kuupa mwili pumziko..kwasababu dhambi ni sumu ya mwili pia, dhambi inauharibu mwili… Mtu anapojiuzuia kutenda dhambi katika mwili, mwili wake hauteseki badala yake ndio unajengeka zaidi, kwahiyo usichanganye kutotenda dhambi na kuutesa mwili.
Ukiona dhambi kama Ulevi au Uzinzi au nyingine yoyote inakufanya mateka, kiasi kwamba usipoifanya mwili wako unateseka basi ni dalili ya kuwa bado utakaso kamili haujaingia maishani mwako, hivyo ni wakati wa kumgeukia Bwana kwa moyo wote kwa kutubu, kubatizwa kwa ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Bwana YESU na kisha kupokea Roho Mtakatifu.
Na ile sheria ya Roho wa uzima itakuweka huru mbali na dhambi, BUREEEEE kabisa..
Warumi 8:2 “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti”.
Bwana atusaidie tuitese miili yetu kwa kufunga na kuzuia usingizi, ili tupate muda wa kukesha na kuomba kwa faida ya roho zetu.
Warumi 13:14 Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.