Karibu tujifunze Neno la Mungu,
Tunapozungumzia nafsi tunamzungumzia mtu mwenyewe, kwahiyo badala ya kusema “Tambua thamani ya nafsi yako” tunaweza tukasema TAMBUA THAMANI YAKO!.
Watu wengi leo wanatoa maisha yao bure kwa mambo yasiyo na maana, wanauza nafsi zao bure kwa mambo ya ulimwengu huu, kwasababu ya tamaa za miili yao, tamaa za fedha, mali n.k, wanaamua kuuza nafsi zao hata kwa shetani ili tu wapate kujifurahisha katika vitu vya dunia hii, mtu yupo radhi kupoteza nafsi yake kwa waganga, vikundi vya kishetani(freemason), ili tu apate mafanikio anayoyataka..
Na ni kwanini wanakuwa wepesi kufanya hivyo? Ni kwasababu hawajui thamani ya nafsi zao, laiti wangejua wasingethubutu kutoa nafsi zao bure kwa shetani, wasingediriki kufurahia mambo ya ulimwengu huu huku nafsi zao zikipotea,
Leo tutaangalia ni kwanamna gani nafsi zetu zinathamani kubwa zaidi ya mambo yote yaliyopo duniani. Ni vizuri sana wewe kama mwamini ujue thamani yako ili uzidi kujitunza na mambo ya ulimwengu huu, na vilevile wewe ambaye bado upo nje ya Kristo ni vyema utambue thamani yako ili uchukue hatua ya kusalimisha nafsi yako kwa Bwana YESU Mkuu wa Uzima maana huko ulikoweka umepoteza.
Hebu tufakari haya maneno ya Bwana Yesu..
Marko 8:34 “Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.
35 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.
36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
37 AMA MTU ATOE NINI BADALA YA NAFSI YAKE?
Umeelewa hapo! Bwana Yesu anasema mtu atakayeiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza kwa ajili yangu ataipata.
Maana yake ukitaka kuiponya nafsi yako isiende kuangamia kwenye ziwa la moto ni lazima ukubali kuangamiza!. na ukikubali kuangamiza kabisa hapo ndipo umeiponya.
Kawaida za ulimwengu unasema mtu akiwa na maisha mazuri, nyumba nzuri, magari, fedha nyinyi, na mafanikio makubwa hapo ameipata nafsi yake, ila hekima ya mbinguni inasema mtu akipata hayo yote na huku hana Yesu ndani yake ameipoteza nafsi yake!.
Kwahiyo leo hii kama upo nje ya Kristo na unajiona una maisha mazuri, una nyumba nzuri, una familia bora, una miradi mikubwa, una elimu kubwa, n.k, fahamu kuwa umepotea ndugu yangu!. Yesu anakuambia ITAKUFAIDIA NINI ukipata ulimwengu wote na ukapata hasara ya nafsi yako. Hayo yote unayoyatumainia sasa itakufaidia nini ukiwanayo na huku unaenda jehanum ya moto,
Dhamiria kuangamiza nafsi yako kabisa kwa kutoka huko ulikoiweka ili upate kuokoka na moto wa Jehanumu, ikiwa ni kwenye fedha, mali, anasa, n.k, angamiza kabisa kwa kuamua kutoa huko, huko unakotumainia, angamiza kabisa kwa habari ya mambo yote yanayofurahisha nafsi ambayo ni machukizo kwa Mungu,
Angamiza kwa habari ya tamaa za mwili, tamaa za macho, jikane kabisa, jiambie kuanzia leo sitoenda huko kilabuni, kuanzia leo sitokunywa pombe na kutumia madawa ya kulevya, kuanzia leo mimi na wanaume/wanawake ninaozini nao ndio basi na futa kabisa namba zao na uwaambie umeokoka, futa picha zote chafu kwenye simu yako na useme kuanzia leo mimi na pornography ndio bayi bayi,
Kuanzia leo mimi na kujichua ndio mwisho, mimi na movies, mipira, magemu kamari ndio basi tena sitoshiriki huko tena na fanya hivyo kwa vitendo huku ukifuta hayo magemu na hiyo miziki za kidunia kwenye simu/ na kutoitazama kwenye tv..
Kama wewe ni mwanamke/Binti kusanya zile vipodozi unazotumiaga kujimekaup, kujichubua, na vile vyote kama lipustick, hereni, mikufu, wanja, na aina zote za mapambo nenda ukazitupe chooni na useme sitorudia tena kuvitumia kwa Jina la Yesu, kusanya mavazi yasiyo na staha/ heshima na adabu kama hizo suruali, vimini, , na nguo zote zinaonyesha ama kuchora mwili wako nenda ukavichome zote useme kuanzia leo mimi nimekuwa wa Yesu sitorudia tena kuvaa mavazi ya kikahaba, na pia kama umesuka biblia inakataza kusuka na kuvaa wigi hivyo huna budi kufumua nywele zako na ubaki katika uasili wako vile Mungu alivyokuumba.
Ukifanya hivyo utakuwa umeangamiza nafsi yako kabisa..huko ndiko kijikana nafsi! sio rahisi ila ukiamua utaweza kabisa, kumbuka ni lazima ufanye hivyo ili uokoke na jehanum/ziwa la moto vinginevyo utakuwa umepoteza nafsi yako.
Na haya yote yatawezekana pale ambapo umetambua thamani ya nafsi yako, maandiko yanasema…
Marko 8:36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
37 AMA MTU ATOE NINI BADALA YA NAFSI YAKE?
Umeona hapo. anasema ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake? Maana yake hakuna chochote ambacho mtu anaweza akatoa iwe fidia ya nafsi ili asiende motoni, Maana yake hata ukitoa mali zote na fedha zote zilizopo katika Benki zote za dunia ili iwe fidia kwa ajili ya kuzuia nafsi yako isiende kuangamia ni jambo lisilowezekana milele,
kwasababu gani? Kwasababu thamani ya nafsi ya mtu ni kubwa..mtu anaweza akapata ulimwengu wote na ikawa hasara kwake kwa maana hakuna chochote kinaweza kulingalishwa na thamani ya nafsi.. Utukufu kwa Bwana Yesu..
Leo hii mtu akipata shida kwenye viungo vya mwili wake ambayo inaweza ikapelekea kifo labda shida ya figo, Kuna uwezekano wa mtu huyu kuokolewa kwenye mauti kwa kuwekewa figo ya mtu mwingine, maana yake mtu anaweza akatoa kiungo cha mwili wake ili aokoe maisha ya ndugu yake au kiungo hicho kikapatikana sehemu nyingine kwa fedha, ila kwahabari ya nafsi hakuna mtu ambaye anaweza akatoa nafsi yake kumwekea mtu mwingine asife, au mahali ambayo nafsi inauzwa, hilo jambo halipo..
maana yake ukishakufa ndio basi! au nafsi yako ikipata shida hakuna hospitali au dawa ya pharmacy unaweza ukatumia kuponya nafsi yako. Ni Yesu tu pekee ndiye aliyejitoa nafsi yake akafa kwa ajili yetu, na ndiye mponyaji wa roho zetu, ukimpata huyo basi hautakufa.. namaanisha hata ukifa hapa duniani utaenda kwenye umilele wa kuishi ndio maana alisema mahali fulani mtu akiniamini, ajapokufa, atakuwa anaishi.(Yohana11:25)
Ila ukikosa huyo, basi hauna tumaini la maisha haya, utasumbuliwa na mapepo, utasumbuliwa na shida zote za rohoni na hakuna wa kukusaidia, hakuna hata dawa za kupunguza maumivu ya nafsi, pale ambapo imepata shida, zaidi ya yote huwezi kutoa chochote ili iwe fidia usiende kuangamia kule jehanum, au ukamkomboa ndugu yako asiende kuangamia kwenye ziwa la moto. Kwamaana fidia ya nafsi zao zinagharama.
Zaburi 49: 7 Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake,
8 (Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hana budi kuiacha hata milele;)
9 ili aishi siku zote asilione kaburi.
Umeona hapo!. Leo tambua thamani ya nafsi yako, na ufahamu yupo mmoja aliyetoa maisha yake kwa ajili yetu na huyo si mwingine zaidi ya Bwana Yesu Kristo Mkuu wa Uzima.
Salimisha maisha yako kwake kwa kumwamini na kudhamiria kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi zote na kubatizwa kwa jina lake sawa sawa na Matendo 3:38 ili upate uzima wa milele.
Kumbuka muda uliobaki, nao sio mwingi. hizi ni siku za mwisho.. mlango wa neema utafungwa muda wowote. na hakutakuwepo tena kuponywa baada ya hapo.
Marko 8:35 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataingamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.
36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
37 AMA MTU ATOE NINI BADALA YA NAFSI YAKE?
Shalom, Maran atha
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.