Tunatakaswa au tunajitakasa katika Yesu Kristo?

Maswali ya Biblia No Comments

Tunatakaswa au tunajitakasa katika Yesu Kristo?

Shalom nakusalimu katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo karibu tuyatafakari maneno ya uzima ya mwokozi wetu.

Katika Biblia maneno yote haya kutakaswa na kujitakasa yote yametumika sehemu tofauti tofauti na ni muhimu kuzingatia Muktadha wa kila habari maneno hayo yanapotajwa/kuandikwa. Na biblia imeweka wazi katika kila Eneo maneno haya yanapotajwa yanaonyesha uhusika wa kitu kinachofanya hivyo.

Sasa katika Ukristo kuna utakaso wa aina kuu tatu. Ni vizuri ukaelewa ili usije ukachanganywa au kupotoshwa na mafundisho ya uongo.

Na kila mmoja tutakwenda kuutazama kwa kina na kimaandiko ili tupate ufahamu kamili, unapoona kutakaswa na kujitakasa basi uwe na ufahamu mpana hata katika maombi yako au hata unapomfundisha mtu juu ya utakaso.

Kuna hatua tatu kuu za utakaso kimaandiko na hizo kila Mkristo lazima azipitie lakini zingine lazima aishi katika hizo hakuna hata hatua moja ambayo inapaswa kuachwa kuna za kuendelea nazo na ambazo zinafanyika mara moja tu.

Tutakwenda kutazama utakaso mmoja baada ya mwingine kwa kina zaidi.

Kabla ya kuzifahamu hizo hatua ni vizuri kwanza tuelewe nini maana ya utakaso?.

Utakaso, ni hali ya kuoshwa au kutengwa mbali na vitu vichafu. Kwa maana ya kiblia zaidi

Utakaso ni Kitendo cha mtu kutengwa na kutakaswa kwa ajili ya Mungu kuwa safi, kuachana na dhambi, na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Yaani kutoka dhambini.

1.Utakaso wa Awali(Kumwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wako).

Huu ni utakaso wa awali kabisa pale unaposikia injili na kuamini moyoni mwako kuwa Yesu alikufa na kufufuka kwa ajili ya dhambi zako na unapomwamini unapokea msamaha wa Dhambi yaani  Ondoleo la dhambi maana yake unatakaswa.

Huu ni utakaso wa awali na hafanyi mtu ila Mungu mweyewe kwa mapenzi yake.

Waebrania 10:10
“Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.”

Kristo amekufa kwa ajili yetu na utakaso huu una dumu milele hatutakaswi mara mbili kwa Yesu Kristo kurudi tena msalabani huu ni utakaso unaotokea mara moja tu kwa sababu ya sadaka ya Kristo msalabani.

Soma tena Waebrania 10:4.

1 Wathesalonike 5:23
“Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.”*

Unaona hapo? Mwenyewe ndio awezae kutakasa nafsi zetu,roho zetu na miili yetu..

Anaendelea kusema tena…

Waebrania 13:12
“Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango.”

Kila mmoja aliemwamini Yesu ametakaswa kwa damu yake kwa kuondolewa makosa na hatia za kila namna na sasa yupo huru katika Kristo hana shutumu lolote.

2.Utakaso kwa njia ya Neno la Mungu.(Endelevu kupitia neno).

Huu ni utakaso endelevu kwa kila Mkristo na ni utakaso wa kila siku, na hapa tunatakaswa kwa kuijua kweli ya neno la Mungu.
Kupitia Neno la Mungu tunatakaswa pale tunafahamu kweli au uhalisia wa neno basi kwa njia hiyo tunatakaswa kwa kutoka katika ujinga fulani wa kiroho na kuelekea katika nuru kamili.

Yohana 17:17
“Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.”

Katika Yohana 15:3 anasema ” wamekuwa safi kwa sababu ya lile Neno alilowaambia, kumbuka hapa ni kabla hata ya kifo chake msalabani,kupitia mafundisho/kweli aliyokuwa akisema basi wale watu walikua wanatakasika. Kwa namna gani? Mtu anapofahamu kweli habaki tena kuwa mtumwa anakua huru..

Leo kuna Wakristo wengi kweli wameokolewa kwa damu ya Kristo na wameamini kazi ya msalaba lakini bado ni wafungwa mahali fulani kwa sababu hawajaifahamu kweli na ikawaweka huru,  ndio maana wengi wako katika ukombozi wa nyota,maji ya upako nk.

Kumbuka kutakaswa ni kusafishwa,kutengwa kwa ajili ya kazi maalumu ya yule atakasae yaani Yesu Kristo.

3.Utakaso binafsi.

Ni muhimu kufahamu jambo hili! Sisi pia tuna wajibu wa kufanya hivi, Mungu anasehemu yake ya kufanya na sisi tuna sehemu yetu ya kufanya ni vizuri sana usije ukachanganya mambo haya na kudanganywa na mafundisho ya uongo tutaangalia kimaandiko.

Huu ni wajibu wa kila Mkristo kufanya hivi na wala sio baadhi Wakati mwingine Yesu anasema “ kujitwika misalaba yatu na tumfate” sehemu nyingine anasema “ kujikana nafsi” huu ni wajibu wetu _hasemi atatusaidia kujitwika misalaba yetu ama kutusaidia kujikana nafsi la bali sisi ndio tufanye hivyo.

Sasa maandiko yanasema..

2 Timotheo 2

21  Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema.

22  Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.

23 Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.

Unaona hapo? Anasema ikiwa mtu “… amejitakasa kwa kujitenga.. ” hasemi “ ametakaswa na kutengwa” maana yake ni wajibu wako. Na anasema utakua chombo cha heshima kimfaacho..

Lakini anasema tena “.. zikimbie tamaa za ujanani ukatafute haki,imani na upendo….” Unaona hapo? Mwenye wajibu wa kukimbia ni wewe.

Nb Yusufu hakukimbizwa na Mungu(Mungu hakumwambia amkimbie mke wa Potifa yeye mwenyewe alisema atamtendaje Bwana uovu mkubwa namna hii?) Akachukua uamuzi wa kukimbia.

Mungu hakushuka akamwambia “Yusufu kimbia” hata kipindi kile Samson asingekatwa nywele zake Mungu angelishuka kumwambia.

Lakini ilikuwa ni wajibu wake kujitambua ni nani yeye na hatakiwi kutoa siri ya nguvu zake.

Anasema tena.. “… uyakatae..” wewe ndio mwenye wajibu wa kusema hapana unapoona kuna mambo yasiyofaa.

Ni sawa unamuomba Mungu akusaidie kushinda ulevi halafu bado unaendelea kwenda sehemu zinazouza vilevi na kukaa hata uombe masaa 24 hutaweza kuushinda ulevi acha kwenda. Vivyo hivyo uzinzi bado una angalia picha za uzinzi tamthilia mbovu unabidi uache wewe.

Yesu anasema kiungo chako kimoja kikikukosesha hasemi “ Kikatwe ..” anasema “ KIKATE ” wewe sio mtu mwingine au Mungu.

Hivyo unavyojitenga na mambo yote yasiyofaa hapo unajitakasa mwenyewe kwa kutokuruhu kuchafuliwa na vitu ambavyo wewe mwenyewe unaweza kuvizuia maana umepewa nguvu hizo.

Maandiko yanasema ” azuiae ulimi wake ” hayasemi ” wazuiliwao ulimi wao na Mungu

Ubarikiwe sana.
Maranatha.
@Nuru ya upendo.
Mawasiliano: 0613079530.

 

 

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

  1. Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *