USISUBIRI MPAKA UVUMILIVU WA MUNGU UKOME JUU YAKO.

Siku za Mwisho No Comments

USISUBIRI MPAKA UVUMILIVU WA MUNGU UKOME JUU YAKO.

Jina la Bwana wetu Yesu libarikiwe. Nakukaribisha tulitafakari Neno la Mungu, ambalo ndio pekee lenye uwezo wa kuokoa roho za watu.

Na leo nataka tuitafakari tena juu ya hukumu ya Mungu inayokuja ulimwenguni.

Ndugu yangu usidhani ukiachwa sasa kwenye UNYAKUO utakuwa na nafasi ya pili mbele za Mungu, kwamba utatubu na Mungu atakuhurumia, Fahamu nafasi ni moja tu nayo ni kwa Njia ya YESU KRISTO peke yake na sio kwa njia yako, ingekuwepo ipo nafasi nyingine, Yesu asingesema mtu haji kwa Baba isipokuwa kwa njia yangu mimi, badala yake angesema mtu haji kwa Baba isipokuwa kwa njia yangu au yako..Hautafika mbinguni ndugu kama chujio la UNYAKUO litakupita.. Na wote watakaobaki hakuta kuwa na lingine lililosalia kwao isipokuwa kukutana na ghadhabu ya hasira ya Mungu, na hiyo haina lengo lingine zaidi ya kuwaharibu watu wote waovu ambao, walikataa neema, walikataa kuishi maisha ambayo Mungu alikusudia kila mwanadamu ayaishi, ni mapigo ambayo hata mtu aombolezeje hawezi kusikiwa.

Sasa hivi watu wanahuburiwa waache njia zao mbaya, waache matendo ya giza wamrudie Mungu lakini hawataki kuacha, wanadhani wataendelea kufurahia hayo maisha ya dhambi siku zote, hawajui uvumilivu wa Mungu unaenda kukoma hivi karibuni.

Wakati wana wa Israeli walipoonywa kwa mamia ya miaka waache maovu na wamgeukie Mungu, lakini hawakutaka, Bwana aliwaonya waache maovu wasije wakapelekwa utumwani hawakusikia, wakatenda maovu mpaka ikafikia hatua ya Mungu kutokusamehe tena..kikombe cha ghadhabu ya Mungu kilikuwa kimejaa juu yao, ulinzi wa kiMungu ukaondoka juu yao, Nebukadneza akaja akawachinja watu mbele ya macho kama kuku, na waliosalia akawapeleka utumwani Babeli.. Tunasoma hayo katika.

2 Nyakati 36: 11 “Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja, alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi na mmoja;

12 akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, Mungu wake; wala hakujinyenyekesha mbele ya Yeremia nabii aliponena kwa kinywa cha Bwana.

13 Tena akamwasi mfalme Nebukadreza, aliyemwapisha kwa Mungu; lakini AKAJIFANYA SHINGO NGUMU, AKAJITIA MOYO NGUVU ASIMGEUKIE BWANA, Mungu wa Israeli.

14 Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana aliyoitakasa katika Yerusalemu.

15 Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;

16 lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, HATA KUSIWE NA KUPONYA.

17 Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mkongwe; akawatia wote mkononi mwake”.

Soma tena mstari wa 15 na wa 16…inasema.. “Bwana aliwatumia wajumbe wake, kwasababu aliwahurumia lakini wakawacheka na kuwadhihaki, hata ilipozidi ghadhabu HATA KUSIWE NA KUPONYA”..Unaona kuna hatua inafika kutakawa HAKUNA KUPONYWA TENA!! Yaliyotokea yametokea, hayawezi kubadilika tena wala kubadilishwa.

Unajua siku zote mtu ambaye ni mwepesi kuudhiwa, au mwepesi kulia, au mwepesi kukasirishwa basi mtu huyo mara nyingi anakuwa pia ni mwepesi kusahau makosa, au mwepesi kufurahi au mwepesi kucheka..Lakini mtu ambaye ni mzito kuudhika pale anapoudhiwa, au kukasirika au kulia au kuwaka hasira, basi mtu huyo vile vile mpaka afikie hatua ya kukasirishwa na baadhi ya mambo basi ujue kuwa itachukua muda sana kuituliza ghadhabu yake au hasira yake.

Tuchukulie tu mfano mtoto mdogo, kama ukimtazama kwa siku anaweza kulia hata mara tano au sita, utakuta kinachomliza ni vitu vidogo vidogo tu visivyo na maana, lakini mtu huyo huyo dakika chake mbeleni utakuta ameshasahau anacheza na wewe kana kwamba hujawahi kumuudhi kabisa..Lakini tuje kwa mtu mzima, anaweza asidondoshe chozi kwa hata kwa mamiaka, lakini siku ukimkuta analia basi ujue kuna jambo zito, tena zito sana tena sio jepesi hata kidogo, pengine utakuta ni msiba au kaumizwa sana,au kajeruhiwa sana, na hivyo mpaka hali hiyo imtokea ndani yake, basi haiwezi kuwa ni kitendo cha dakika chache kuondoka, pengine itamgharimu miezi au miaka ndipo iishe kabisa.

Hali kadhalika biblia imetuweka wazi kabisa, kuhusu hali ya Mungu wetu wa mbinguni tunaye mwabudu siku zote, yeye ni Mungu mvumilivu sana, ni mwingi wa rehema, ni mnyenyekevu, ni mwenye neema, ni mwingi wa huruma, haoni hasira haraka,..Na ni kweli ndivyo alivyo hata sisi wenyewe tunalishuhudia leo hilo pale tunapoona watu tunaona wanatembea barabarani uchi, watu wanamtukana Mungu hadharani lakini hasemi chochote, watu wanawachinja wenzao kama wanyama bila huruma na Mungu hafanyi lolote, watu wanawakata viungo watoto wadogo wasio na hatia wakiwa hai, na kuchukua viungo vya maalbino, wengine wanawachuna ngozi ili kwenda kuuza kwa waganga, mpaka tunajiuliza hivi Mungu hayaoni haya yote? Mbona hachukui hatua yoyote kali..Ingekuwa ni wewe au mimi ni Mungu ni wazi kuwa hakuna hata mmoja angesalia tungeshawateketeza wote.Lakini kwa Mungu haipo hivyo yeye alisema “..

Bwana si mwepesi wa hasira, (Nahumu 3:1)…Ni mpole wa Hasira, mwingi wa rehema (Hesabu 14:8)

Pia Kutoka 34: 6 “…., Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; 7 mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi;..”

Na pia Daudi anashuhudia hilo na kusema “Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, Zaburi 145:8” Na ukisoma pia Yona 4:2 na Nehemia 9:17..utathibitisha jambo hilo hilo.

Unaona hiyo ndio sifa yake kuu.. Lakini yeye kuonyesha rehema zake hata kwa waovu sio kwamba anapenda kuendelea kuwaona wanafanya mambo yao maovu, bali kinyume chake anataka wote wafikie toba, na ndio maana kila siku anawahubiria watubu, Lakini wasipotaka kutubu, kama tulivyoona kuwa mtu Yule ambaye si mwepesi kuudhika,ikifika siku ameudhika basi jua kuwa ghadhabu yake haiishi leo wala kesho, ndivyo ilivyo kwa Mungu ukali wa hasira yake hakuna atakayeweza kuuzima, si kwa toba wala kwa kulia siku ile itakapofika..

Watu wa kipindi cha Nuhu walipuuzia sana uvumilivu wa Mungu kwao, walihuburiwa injili kwa miaka mingi, lakini waliona mbona hakuna dalili yoyote ya kuadhibiwa, kama vile Mungu hayupo, Mungu hawezi kuangamiza dunia yote na watoto ndani yake,ndivyo walivyokuwa wanajifariji, Nuhu alionekana kama kichaa anacheza lakini siku ile walipoingia kwenye safina, ndipo waovu walipojua kweli hasira ya Mungu ni kali…watu 8 tu kati ya mabilioni ya watu waliokuwa wanaishi duniani ndio waliopona.

1Petro 3:20 ”watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji”.

Vivyo hivyo ilikuwa katika siku za Lutu, na ndivyo itakavyokuwa katika SIKU ILE YA HASIRA YA BWANA kama Bwana alivyoifananisha siku ile na hizo, ambayo hiyo ipo karibuni sana kutokea. Kutakuwa na kulia lakini Mungu hatasikia, kutakuwa na maombolezo lakini Mungu hataokoa,

Ukiona kwanini dunia mpaka dakika hii haijateketezwa, ujue kuwa sio kwamba Mungu anafurahia ulawiti wako, au uzinzi wako, au ulevi wako, au uvaaji vimini vyako, ni kwasababu uvumilivu wake unakungoja utubu, ili usiingie katika adhabu kuu ya siku ile, Unazini lakini Mungu hakusemeshi chochote, unatazama pornography kwa siri, lakini Mungu hakuadhibu kwa lolote, unafanya mambo machafu lakini Mungu kama vile hakuoni..sio kwamba anapendezwa na wewe au kwamba wewe ni mtu pekee sana kwake, na ndio maana hayakukuti mabaya sasa..

Lakini fahamu si mwepesi wa hasira ni Mwingi wa hasira..uvumilivu wake ndio unaokuvuta utubu..

2Petro 3:8 “Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.

9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, BALI HUVUMILIA KWENU, MAANA HAPENDI MTU YE YOTE APOTEE, BALI WOTE WAFIKILIE TOBA.

10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.

11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa,”

Soma tena Warumi 2:4 Bwana anasema..

Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?

[5]Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu,”

Kama bado unasua sua, au upo vuguvugu ni wakati sasa wa kuanza kuyatengeneza mambo yako sawa na Mungu wako..Usijivunie dini au dhehebu,..wakati tuliopo ni wakati wa kuutafuta uhusiano wako binafsi na Mungu wako. Jiulize je! Ikiwa unyakuo utapita leo nitakuwa na uhakika wa kwenda na Bwana..Je! nikifa leo nitakuwa na uhakika wa kwenda mbinguni, au kwenye lile shimo la kuzimu.

Usipotubu leo upo wakati mbaya unakusubiria mbeleni usiokuwa na msamaha. Leo hii ukiwa tayari kuyakabidhi maisha yako kwa Bwana kwa kumaanisha kabisa, na sio nusu nusu, mguu mmoja huku na mwingine kule atakusamehe kabisa na kuyafuta makosa yako yote, kwasababu hicho ndicho anachokitafuta kwako.

Hivyo uamuzi ni wako, lakini maombi yangu ni leo utubu ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.Kisha baada ya hapo utakuwa umezaliwa mara ya pili, kwa Roho Mtakatifu atakayeingia ndani yako”

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *