USITIE MACHUKIZO NDANI YA NYUMBA YAKO

Biblia kwa kina No Comments

USITIE MACHUKIZO NDANI YA NYUMBA YAKO

Kumbukumbu la Torati 7:26 ”na machukizo usitie ndani ya nyumba yako, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa; kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa”.

Machukizo ni nini?

Machukizo inatokana na neno “chukizo” na chukizo ni kitu kinachosababisha chuki/hasira. Kwa Mungu kitu chochote kinachoipandisha ghadhabu yake kinaitwa “chukizo”.

Sasa Neno la Mungu kama tunavyosoma hapo juu, linasema ”usitie machukizo ndani ya nyumba yako”

Lakini, je unaelelea vyema maana ya hilo andiko katika nyakati hizi? Hebu tuone nyumba ambayo tunapaswa kuitunza zaidi hata ya haya majengo tunayolalia.

Maandiko yanasema katika…

1 Petro 2:5 Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe NYUMBA YA ROHO, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.

Ohoo, kumbe! sisi ni nyumba..yaani miili yetu, tena ni nyumba ya Roho, yaani Roho Mtakatifu. Tena sehemu nyingine anasema..

Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

[17]Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.” (1Wakorintho 3:16-17)

Ili kulithibitisha zaidi hili, kuwa miili yetu ni nyumba/hekalu la Mungu…hebu tusome tena maandiko haya katika…

Yohana 2:19-21 Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.

[20]Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?

[21]LAKINI YEYE ALINENA HABARI ZA HEKALU LA MWILI WAKE.

Bila shaka, kwa udhibitisho huo, miili yetu ni nyumba/hekalu la Mungu. Sasa tukirudi katika Kumbukumbu la torati 7, Neno la Mungu linasema..

Kumbukumbu la Torati 7:26 NA MACHUKIZO USITIE NDANI YA NYUMBA YAKO, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa; kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa.

Kulingana na tafsiri ya nyumba kama tulivyosoma katika maandiko yaliyotangulia, tunaweza tukaweka hilo andiko katika lugha nyingine, ikasomeka namna hii..

NA MACHUKIZO USITIE NDANI YA MWILI WAKO, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa, kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa.”

Bila shaka, sasa natumai tumeelewa vyema hilo andiko kwamba sio ile nyumba tu tuliyojenga kwa mikono yetu ndio tusitie machukizo, hapana, bali hata na miili yetu ni nyumba..tena ni nyumba ya Roho, hivyo hatupaswi kabisa kutia wala hata kuisogezea kitu chochote ambacho ni chukizo kwa Mungu.

Hebu, tuone baadhi ya vitu ambavyo ni machukizo kwa Mungu ili tuviepuke kabisa na tuweke mbali na nyumba zetu/miili yetu.

1. Ibada ya Sanamu.

Sanamu ya aina yoyote ile ilikuwa ni machukizo kwa Mungu na hicho ndicho kitu cha kwanza kilichokuwa kinaletea wivu kwa Mungu.

Kumbukumbu 27:15 “Na alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga, au ya kusubu, machukizo kwa Bwana, kazi ya mikono ya fundi, akaisimamisha kwa siri. Na watu wote wajibu, waseme, Amina”.

Kuabudu sanamu: Katika agano la kale ni kitendo chochote cha kwenda kuabudu au kusujudia, au kutumika kitu kingine chochote, tofauti na Mungu mkuu mmoja aliye hai (YEHOVA).

Moja ya amri 10 Mungu alizowapa wana wa Israeli, ilikuwa ni pamoja na kujiepusha na ibada za sanamu za aina yoyote..

Amri ya pili inasema hivi..

Kutoka 20:4 “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. 

5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 

6 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu”.

Hivyo mtu akikigeuza kitu chochote, kuwa mbadala wa Mungu, huko ni sawa na kuabudu sanamu, ukiweka mdoli nyumbani kwako na kwenda kumpigia magoti na kumwomba kana kwamba ni Mungu, ujue hapo unafanya ibada za sanamu..

Ukitengeneza kinyago chenye sura ya mtakatifu Fulani labda Mariamu, au Bwana Yesu akiwa pale msalabani, kisha ukakihusianisha na mambo ya ibada kwa mfano kukisujudia, au kukiabudu, au kuombea dua zako kwa kupitia hicho, tayari hiyo ni ibada za sanamu,

Ukining’iniza picha ukutani ya mtu Fulani maarufu, au mnyama , au kitu Fulani kwa lengo la kukifanya kama kipatanishi chako na Mungu, au kitu chako kinachoweza kukupa bahati Fulani, hiyo tayari ni ibada za sanamu.

Hata ukipanda mti, au Ua fulani, ukiamini kuwa linaweza kukulinda, au kueleza hatma ya maisha yako, tayari hiyo nayo ni ibada za sanamu.

Kumbukumbu 16:21 “Usipande mti uwao wote kuwa Ashera kwako kando ya madhabahu utakayofanya ya Bwana, Mungu wako.”

Na ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu, yanayomtia wivu kiasi cha Mungu kukupatilizia maovu hata ya baba zako, uone ni jinsi gani kitendo hicho kinavyomuudhi Mungu..

2 Jambo la Pili ni MAPAMBO: 

Mapambo yoyote ambayo yanaweza kuning’inizwa juu ya mwili wa mtu, ni machukizo mbele makubwa mbele za Mungu, kumbuka tumeona miili yetu ni nyumba ya Roho Mtakatifu na sio roho chafu, Wengi hawapendi kusikia haya lakini ni afadhali usikie leo hii ubadilike, ili siku ile usije ukasema “mbona sikupata mtu aliyeniambia ukweli”.

Nataka nikuambie UKWELI ndugu/Dada yoyote unayevaa wigi, au unayevaa herein au unayevaa nguo fupi (yaani vimini, pamoja na suruali kwa wadada)..au unayevaa mambo yoyote ambayo hujui maana yake, na bado umesema umempa Bwana maisha yako..kama unafanya hayo pasipo kujua, leo hii nakuambia ukweli yaache mambo hayo yanapeleka mamilioni kuzimu. Mwili wako tangu ulipompa Bwana maisha yako ulifanyika Hekalu lake..na Bwana anasema..

Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.” (1Wakorintho 3:17)

Kuanzia leo, fahamu kuwa mwili wako ni nyumba ya sala..ndio maana inaitwa HEKALU, hivyo usitie alama au kitu chochote bandia maana ni machukizo kwa Mungu.

3. Jambo la tatu ni Uasherati na ulawiti.

Walawi 18: 22 “Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo”.

Soma tena Mambo ya Walawi 20:13

Uasherati ndio jambo la kwanza kabisa linaloweza kumwangamiza mtu anayesema amempa Bwana maisha yake, Na uasherati/uzinzi ndio dhambi ya kwanza inayoliharibu Hekalu la Roho Mtakatifu..Mtu mzinifu na bado anasema ameokoka..anafanya dhambi mbaya kuliko hata mtu mwuaji ambaye hajampa Bwana maisha yake.

* 1 Wakorintho 6:17 “Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye.

18 IKIMBIENI ZINAA. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe”.

Mithali 6: 32 “Mtu aziniye na mwanamke HANA AKILI KABISA; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake”.

Kaka/Dada..usidanganyike, uashetari kabla ya ndoa, ni sawa na kujiwekea kitanzi mwenyewe shingoni na kwenda kujiua. Ni sawa na ndege anayeenda mtegoni peke yake biblia inasema hivyo katika (Mithali 7:23-27).

Biblia inasema pia “unafanya jambo litakalokuangamiza nafsi yako”. Bwana hawezi kuridhia huo uovu juu ya Hekalu lake, ambalo lingepaswa kuwa Takatifu, na sehemu ya sala. Ni heri uwe umeamua kuwa mtu wa ulimwengu kuliko kusema umeokolewa na YESU KRISTO halafu unafanya uasherati. Ni hatari sana.

4. Mavazi yasiyopasa.

Kumbukumbu 22:5 “Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako”

Mfano wa mavazi yasiyopasa, ni suruali kwa mwanamke, na nguo mfano wa magauni kwa wanaume

Mwanamke yeyote kuvaa suruali ni machukizo mbele za Mungu, Suruali sio vazi la kumsitiri mwanamke, hakuna mwanamke yeyote anayevaa suruali na kuonekana kama kajisitiri, badala yake ataonekana kama kajidhalilisha au kajifunua..hata kama amevaa kubwa kiasi gani bado itabaki kuwa chukizo kwasababu ni vazi la jinsia nyingine, Na maandiko yanasema wanawake na wavae mavazi ya kujisitiri.

1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani”

Hivyo mwanamke yeyote hapaswi kuvaa suruali, wala vimini wala nguo zozote zinazochora maungo yake.

Hayo ni baadhi tu ya vitu ambavyo ni machukizo kwa Mungu pale tunapotia ndani ya miili yetu ambayo ni nyumba zetu pia…na biblia inasema..

“na machukizo usitie ndani ya nyumba yako, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; UKICHUKIE KABISA, na kukikataa kabisa; kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa.”(Kumb.7:26)

Je! wewe kama mkristo unayesema umeokoa, je unaitunza nyumba yako? Au umeifanya kuwa pango la wanyang’anyi?

Kumbuka, biblia inasema katika…

Ufunuo wa Yohana 21:8 Bali waoga, na wasioamini, na WACHUKIZAO, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.

Kama mkristo, fahamu kuwa tangu siku ulipompa Bwana maisha yake, Roho Mtakatifu alikugeuza wewe kuwa Hekalu lake takatifu, usiliharibu ili naye asikuharibu. Kama ulikuwa unafanya hayo pasipo kujua, Mungu ni mwenye huruma, leo hii umeujua ukweli ukitubu kwa kusudia kutokufanya hayo tena yeye ni mwamini atakusamehe kulingana na Neno lake, tupa leo hizo suruali ulizokuwa unavaa, tupa leo hizo wigi, na hereni ulizokuwa unavaa, acha kupaka uwanjua na lipstick…weka nywele zako katika uhalisia wake, zitunze tu, na la muhimu kabisa Acha uasherati. Usitamkwe kabisa! Litakase Hekalu la Mungu.

Na vilevile, ondoa hizo picha ulizoning’niniza ukutani mwa nyumba yako ili kuabudu na hizo sanamu za kila namna… maana hayo yanamtia Mungu wivu.

Bwana akubariki,

Na kama hujampa Bwana maisha yako, ni vyema ukafanya hivyo leo, angali mlango wa Neema haujafungwa, mgeukie yeye kwamaana biblia inasema “mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijakaribia siku zilizo mbaya”.

Bwana akusaidie katika hilo na aikamilishe safari njema aliyoianza moyoni mwako.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *