Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa.

Mwanamke No Comments

Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa.

Zaburi 68:11 “Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa;”

Biblia inamwita mwanamke mwenye kutangaza habari njema kuwa ni “jeshi kubwa “ Nini biblia imeona kwa mwanamke hata kumfananisha na jeshi kubwa? Unajua unapozungumzia kuhusu jeshi kubwa una maana ya watu waliokuwa na mafunzo ya kujilinda na kushambulia, Watu wenye uwezo wa kutumia silaha zote,watu wenye kujua mbinu za kupambana na adui,watu wenye uvumilivu mkubwa,watu wenye ngome N.K ( Sifa zipo nyingi za jeshi)

Ukweli ni kwamba, mwanamke ana nafasi kubwa ya kuwavuta watu kwa Kristo kuliko hata mwanaume, na vilevile mwanamke anayo nafasi kubwa ya kuwapeleka watu kwa shetani kuliko mwanaume.

Siyo ajabu leo hii, wanawake wengi ndio wanatumiwa na ibilisi kuchafua dunia kwa uzinzi na uasherati.

Mwanamke mmoja tu anaweza kuharibu jamii yote akitembea nusu uchi, hivyo hiyo ni siri ambayo adui ameifahamu kuwa wanawake ni jeshi kubwa, kwasababu ni rahisi kutangaza habari na kupokelewa na watu wengi kirahisi..kuliko wanaume. Sasa hivi ukipita kwenye kila bar utakuta ni wanawake ndio wanahudumu, ukipita mjini utakuta midoli ya wanawake zipo uchi, ukipita mitandaoni utakuta wanawake wamejianika uchi, we ujiulizi ni kwanini iwe ni wanawake?

Jibu ni lile lile, ”wanawake ni jeshi kubwa” mionekano yao tu inatosha kutangaza habari, iwe ni habari njema au mbaya tutajua tu kwa mwonekano wa nje, ndio maana kuna umuhimu sana mwanamke wa kikirsto kujistiri ipasavyo.

Kwahiyo mwanamke wa kikirsto aliyeokoka kweli kweli, anayo nafasi kubwa ya kuwavuta watu wengi kwa Kristo kuliko hata mwanaume.

Leo hii binti wa Yesu ukipita tu njiani, watu wakikuona jinsi ulivyojistiri kutoka juu kichwani mpaka chini miguuni, watavutiwa na wewe bila hata kuzungumza, si zaidi ukienda pale stend au pale kijiweni na kutangaza habari njema za Kristo, ni vijana wangapi watatega masikio kukusikiliza? Bila shaka kila kijana atakusikiliza na katika kukusikiliza Roho wa Kristo atamvuta aokoke, hiyo ni nafasi ambayo itakuwa rahisi kwako kutekelezeka kuliko wengine ambao ni ngumu kusikilizwa.

Kumbuka, hapa hatuzungumzii nafasi ya mwanamke kuhubiri kanisani au kufundisha..biblia haiwezi kujichanganya iseme mwanamke hana ruhusa ya kufundisha bali anyamaze (1Wakorintho 14:34) na huku iseme wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa. Hapa biblia inalenga kuhubiri Injili nje ya kanisa, kuwatangazia watu wa nje habari za Yesu waokoke, habari njema inahubiriwa kwa watu wa ulimwengu na sio watu wa kanisani waliookoka.

Hivyo, mwanamke/Binti uliyempokea Yesu kweli kweli na kujazwa Roho Mtakatifu, usimzimishe Roho, amka nenda kawatangazie ulimwengu habari njema za ufalme wa Mungu. Kumbuka we ni jeshi! Usiwe unaenda tu kanisani na kurudi nyumbani, fanya jambo la ziada kujizoezesha kutangaza habari njema, Usionee injili haya kwamaana injili ni uweza wa Mungu.

Warumi 1:16 “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia”.

Na pia Kristo alisema..

Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”. (Marko 8:38)

Hivyo usimuonee Kristo haya, usione aibu kwenda kuwaambia watu waache matendo ya giza kama uasherati, ulevi, ulawiti, ufisadi, uvaaji mbaya, utazamaji wa pornography, usengenyaji, na mambo yote mabaya, usione aibu kuwaambia watu watendao matendo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu kwamaana biblia imesema hivyo katika Wagalatia 5:19.

Hivyo mwanamke tumia hii nafasi yako vizuri kuwavuta watu wengi kwa Kristo kwa maana dhawabu yako ni kubwa, fahamu kuwa kuna maelfu ya wanawake wanashuka kuzimu kila siku kwasababu ya kuvaa vimini, masuruali, kupaka wanja, mekaups, kuvaa mawigi, kusuka marasta, kuvaa mahereni n.k, nenda kawatangazie kuwa mambo hayo ni machukizo kwa Mungu, ni rahisi wakusikilize wewe kuliko mwanaume.

Kazi ya kutangaza habari njema/kuhubiri Injili sio ya wainjilisti tu pekee yao, na wala sio ya wanaume tu, ni ya wakristo wote..pasipo kujalisha jinsia, umri, cheo. Ni agizo kwa wakristo wote. Tena wanawake wana nafasi kubwa katika kizazi hiki cha zinaa.

Lakini, kama hujaokoka.. huwezi kufanya kazi hii, kwasababu Roho Mtakatifu hayupo ndani yako na hivyo huwezi kuwavuta watu waokoke.. haijalishi utapasa sauti kiasi gani. Kumbuka ni Roho Mtakatifu ndiye anayeshawishi mioyo ya watu na sio ushawishi wa maneno yetu mazuri.

Kwahiyo, unapaswa kwanza kuokoka kweli kweli, yaani kutubu dhambi na kumaanisha kuacha ulimwengu kabisa kisha unaenda kubatizwa kwa maji mengi na Kwa jina la Bwana Yesu Kristo na hivyo utapokea Roho Mtakatifu..hapo utakuwa na nafasi ya kufanya kazi ya Mungu.

Je! Umempokea Yesu ipasavyo? Je unatumia nafasi yako wewe kama mwanamke kutangaza habari njema? Kama ni hapana, hebu leo tafakari na uchukue hatua.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *