Shalom mwana wa Mungu,
Wewe kama mwana wa Mungu lazima ufahamu kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na ushirika, na ushirika unatokana na kushiriki Katika Mambo fulani, na ili ushirika ule ulete matokeo ni lazima uambukizwe aina ya sifa au tabia ya kile unachoshiriki nacho kwa wakati…
Ikiwa kuna ushirika unaleta sifa njema, basi fahamu upo ushirika pia unaleta sifa mbaya, na huu umekuwa ukitumiwa sana na shetani, shetani anayazindua mapepo yake ili yaendeelee kufanya ushirika na wale wanaofanya Ushirikina, kwasababu ni neno moja lenye maana ya ushirika, na ushirika unafanyika pale mtu anapoyafanya mambo ya kishirikina basi anaambukizwa tabia za mapepo,
Imekuwa ni desturi ya watu wengi kila wanapopitia changamoto fulani au wanatamani kupata jambo lolote,akili ya kwanza wanakimbilia kwa waganga, hawafahamu kule wanakwenda kufanya ushirika na mapepo kwa zile dawa wanazopewa wakazitumie, na kwa uwongo wa shetani anawafumba macho waone kama wamepona mambo yao kumbe ni kwa kitambo tu mwisho wa siku pepo hilo hilo linakuja kukuletea madhara makubwa hata ya kukuua, na hiyo ni asili ya shetani tokea mwanzo, yeye ni muuaji..
Hivyo kuna hatari kubwa ya kufanya mambo ambayo yapo kinyume na neno,maana yake unapoyakubali kuyafanya unakuwa na shirika na mapepo,mnakuwa pamoja kitabia..
Ushirika upo pia kwa Mungu, Mungu na yeye anafanya ushirika na watu wake, lakini ana kanuni zake na taratibu ili uige ile sifa njema na tabia njema kutoka kwake, hivyo kama utakuwa ni mtu wa jumapili tu kanisani, hushirikiani na wapendwa wenzako, umekuwa kama mtalii au mtembeleaji fahamu kabisa utaukosa huu ushirika wa kiMungu na mwisho wa siku utakosa nguvu..
Tuangalie aina za ushirika wa YESU KRISTO
Kuwa mtu wa kuhudumu
Kushiriki meza ya Bwana
Kutawadhana miguu
Umeona ushirika wa Kristo unavyotakiwa uwe, watu wengi wanakuwa wanaukwepa huu ushirika wa kwanza wa kuhudumu labda pengine wakijua ni wa watu fulani, swala la kuhudumu ni la kila mmoja ndani ya kanisa, anao wajibu wa kuwafundisha wengine, anawajibu wa kufanya usafi, kufagia chooni, ana wajibu kufanya shughuli zote kwenye kanisa pamoja na watakatifu wenzake mana ndivyo wanavyozidisha ushirika na kuujenga mwili wa Kristo, na hii itakupa sababu za kusonga mbele kwenye wokovu..
Ushirika wa pili ni kushiriki meza ya Bwana, ushirika huu unakuunganisha na Mungu mwenyewe, unakufanya umuelewe Mungu kwa namna nyingine ya kitofauti sana, ni sawa na wale vijana wawili walikuwa kwenye maandiko waliokuwa wanakwenda kijiji cha Emau,wakiwa njiani Bwana aliungana nao lakini hawakumjua ila waliposhiriki mkate wakati huo huo wakafumbuliwa macho wakamuona Bwana, hivyo kuna faida kubwa sana za kushiriki meza ya Bwana..
1Wakorintho 10:14 “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. 15 Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo.
16 Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, JE! SI USHIRIKA wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, SI USHIRIKA wa mwili wa Kristo? 17 Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.
18 Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu? 19 Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu?
20 Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani”.
Ushirika huu wa meza ya Bwana una nguvu ya kuleta matokeo makubwa sana Katika roho, hivyo usipoula mkate na kuinywa damu ya Bwana huna Uzima ndani yako, ndivyo Bwana anavyosema (Yohana 6:53)
Na ushirika wa tatu ni kutawadhana miguu, huu ni wa sisi kwa sisi, unapoishika miguu ya mKristo mwenzako na kuiosha maana yake unatangaza, kujishusha,unyenyekevu kwake, hivyo Bwana akiliona hilo anashusha Neema ya upendano wa ndugu ndani unajikuta mnyenyekevu na mpole kwa watu..
Ukitaka upokee tunda la Roho ndani yako,kama Upendo, Amani,utu wema,upole na yale yote yatokayo kwa Mungu ni lazima uwe Katika ushirika na yeye, maana nje ya hapo haiwezekani kuwa na ushirika na Mungu,
Matendo 2:41 “Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. 42 Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali”
Dumu Katika ushirika na Bwana Yesu maana yeye ndiye chanzo cha uhai wetu,
Maranatha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.