
ACHA KUMKOSOA MUUMBA WAKO.
(Ujumbe kwa mabinti/wanawake)
Huu ni Ujumbe unaokuhusu wewe dada/mama ambaye unamkosoa Muumba wako aliyekuumba kwa uzuri.
Biblia inasema..
“Tazama, hili tu nimeliona; Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu, lakini wamebuni mavumbuzi mengi”. (Mahubiri 7:29).
Mungu alikuumba ukiwa umekamilika tena akaona ya kuwa kazi aliyoifanya ni chema, Lakini leo unamkosoa, unabadilisha maumbile yako, unabadilisha muonekano wako kuanzia juu mpaka chini.
Ngozi ambayo Mungu amekuumbia umeona haifai, nywele ambazo Mungu amekuumbia na akaihesabu kama anavyosema katika Luka 12:7 “Hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote…” Umezikataa, umebuni nywele zako, umebuni ngozi yako, mpaka mdomo umebadilisha, masikio, pua, macho ambayo Mungu aliumba kwa lengo lake, wewe umegeuza kuwa viungo vya mapambo. Je utaepukaje hukumu ya jehanum?
Biblia Neno la Mungu lililo hai linasema..
Isaya 29:16 “Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; KITU KILICHOFINYANGWA KIMNENE YEYE ALIYEKIFINYANGA, HAKUNIFINYANGA HUYU; AU KITU KILICHOUMBWA KIMNENE YEYE ALIYEKIUMBA, YEYE HANA UFAHAMU?
Isaya 45:9 “OLE WAKE ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?
Warumi 9:19 “Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?
[20]La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? JE! KITU KILICHOUMBWA KIMWAMBIE YEYE ALIYEKIUMBA, KWANI KUNIUMBA HIVI?
[21]Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?
Tafakari sana hayo maneno ewe dada unayemkosoa muumba wako.
Acha kumkosoa Muumba wako, acha kujichubua hiyo ngozi, acha kutoboa toboa na kujichora chora huo mwili, acha kujipaka paka rangi bandia, fahamu huo mwili sio mali yako mwenyewe? Ni mali ya Mungu na amekusudia akae ndani yake.
1 Wakorintho 6:19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;”
Sasa, yamkini hukufanya hivyo kwa kukusudia, lakini huwenda umedanganywa na yule joka aitwaye ibilisi na shetani, yule audanganyaye ulimwengu wote. Au umejikuta unafuata mkumbo wa kizazi hiki kilichopotoka, na ukadhani kuwa ukifanya hivyo utapendeza na utaonekana mwenye akili na anayekwenda na wakati, na pengine ulimsikiliza mchungaji wako anayehubiri kuwa Mungu anaangalia moyo na hana shida na mwili.
Lakini leo nakuonya wala sio mimi bali ni Bwana, hakika usipotubu na kuacha kumkosoa Mungu, hautakuwa na sehemu katika mbingu, bali sehemu yako itakuwa ni lile ziwa liwakalo moto na kibiriti kama maandiko yanavyosema kuwa wachukizao wote sehemu yao ni huko (Ufunuo 21:8).
Hivyo ni heri tu leo uamue kutii Neno la Mungu kwa kuondoa mapambo katika mwili wako, ondoa hizo nywele bandia na marasta kichwani, ondoa hizo kucha bandia na hiyo rangi mbandia uliyopaka kwenye kucha, ondoa hizo hereni, vipini, bangili, lipusticks, mekaups, wanja, na kila aina ya uchafu kwenye mwili wako.
Kama unataka kujipamba, subiri uende kule mbinguni ukajipambe utakavyo kama kutakuwepo na huo utaratibu, lakini kwasasa tunaishi kama Mungu atakavyo na sio kama sisi tutakavyo. Biblia imeshasema..
“Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, KUSUKA NYWELE; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;
[4]bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.
[5]Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao.” (1Petro3:3-5)
Umeona mapambo ya wanawake watakatifu, sio kuvaa hereni, au kusuka nywele, sio kutia rangi mdomoni au kwenye kucha, hapana watakatifu wa zamani na wa sasa hawajipambi hivyo, bali wanajipamba kwa mapambo ya ndani yaani roho ya upole na utulivu. (Uzuri wa ndani).
Hivyo Dada, amua leo kumpa Yesu maisha yako kwa kujikana nafsi yako kabisa, naye atakubadilisha kama anavyowabadilisha wengine.
Usiogope kuonekana mshamba na watu wa dunia hii, we amua kumfuata Yesu na kuishi sawa sawa na Neno lake. Kwasababu itakufaidia nini kusifiwa na walimwengu kwamba unaenda na wakati na huku hatima yako unaishia kwenda kutupwa jehanumu ya moto.
Mbona unapendeza tu ukibaki katika uasili wako Mungu aliyokuumbia nayo. Usimpe ibilisi nafasi maana yeye amekwisha hukumiwa hawezi tena kutubu hivyo anatafuta kila namna ya kuwadanganya wanadamu wamkosee Mungu na mwisho wakajikutanishe katika lile ziwa la moto.
Waefeso 4:27 “wala msimpe Ibilisi nafasi”.
Bwana akujalie kuelewa haya na uchukue hatua.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.