WOTE NIWAPENDAO MIMI NAWAKEMEA NA KUWARUDI.

Biblia kwa kina No Comments

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu wetu Yesu Kristo karibu tuyatafakari maneno ya uzima ya Bwana wetu Yesu.

Ufunuo 3:19 “Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.”

Kama Mkristo uliyeokolewa/kukombolewa kwa damu ya thamani ya Yesu Kristo maana yake wewe umefanyika kuwa ni mwana wa Mungu. Yeye ni Baba kwako na wewe ni mtoto kwake hivyo pale unapokosa kuwa mwepesi wa kutubu na kuendelea mbele kwa kuacha kabisa yale matendo maovu ya uliyokuwa ukiyafanya.
Sawa sawa na maandiko yanavyosema..

Yohana 1:12 “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;”

Unaona hapo! Hasemi ‘…..Aliwapa uwezo wa kufanyika WATU WA MUNGU…” lakini anasema aliwapa uwezo wa kufanyika “WANA WA MUNGU” sasa mimi na wewe ni watoto wa Mungu.

Sasa ni lazima ufahamu kabisa kuna wakati Mungu atakuadhibu kwa kiboko chake pale unapokosea ili kukurudisha katika mstari usipotee. Watu wengi hawalijui hili jambo na kuna injili zingine zinakwambia kabisa Mungu hawezi kukuadhibu anakupenda sana.

Lakini ukweli ni kwamba

“hakuna upendo usiokuwa na maonyo ndani yake wala adhabu katika mambo yasiyokuwa mazuri.”

 

Upendo pasipo kuwa na maonyo basi huo ni unafiki wala sio upendo.

Ni sawa na wazazi wetu wa Mwilini pale tunapokosea wanalikuwa wanatuonya kwa fimbo lengo si kwamba walikuwa wanatuchukia ama hawatupendi la! Sivyo ila walikuwa wanatupenda walikuwa wanafanya vile ili kutetengeneza tusipotee.

siku zote Baba anaemuadhibu mtoto anampenda kinyume chake Baba asiyefanya hivyo hampendi mtoto wake wala hamuwazii mema yeye anaona vyovyote ni sawa tu.”

 

Mithali 13:24

“Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema. ”

Ndugu usidanganyike kwamba kutokumuadhibu ni upendo la! Sivyo hivyo hii ni injili ya shetani.

Maandiko yanaweka wazi kabisa..

Waebrania 9:12 “Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi?”

unapokosea hakuna kosa dogo kwa Mungu  ni sisi tu na fahamu zetu huwa tunasema Mungu hawezi kuniadhibu katika hili ni kawaida tu

ndugu yangu Mungu anajua sio kawaida. Kila jambo Mungu analichukulia katika uzito na lina adhabu yake anajua yeye ni kwa nini katika kila jambo.

Kusamehewa utasamehewa lakini adhabu utakutanana nayo tu ili kukutengeneza ili kukuonya na kukupeleka katika njia iliyo nzuri ili usipotee. Japokuwa utaona mateso makali, utalia utaishiwa raha, na amani, wakati mwingine kuosa tumaini na amani nk. Lakini mwisho wa siku utamshukuru sana Mungu kwa nini alifanya vile. Kama ni mtu wa kutafakari utaliona hilo jambo.

Maandiko yanaweka wazi tukisoma…

Waebrania 12:6-7 “Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?”

Unaona hapo! anasema “…Maana yeye ambaye Bwana AMPENDA HUMRUDI NAYE HUMPIGA KILA MWANA AMKUBALIE.” Mungu anatutendea kama wana yaani(anatufundisha na kutuonya/discipline).

siku zote fimbo ya Mungu inaposhuka kukuadhibu lazima uamze kujikagua na kutazama ni wapi hapako sawa wakati mwingine Mungu anaweza kukufunulia ni kwa nini inakuwa hivyo.

Sasa kama Mungu asipotuadhibu maana yake sisi sio watoto halali wake tutakuwa ni wa haramu kama maandiko yanavyosema.

Waebrania 12:8 “Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa WANA WA HARAMU NINYI, WALA SI WANA WA HALALI.”

Unaona hapo! Jitafakari ndugu je! Umewahi kurudiwa na Mungu? Ikiwa unafanya maovu na makosa unaona ni kawaida tu huoni chochote Mungu akikuonya basi kuna shida mahali Fulani tengeneza “KIBOKO CHA MUNGU NI KIZURI SANA”.

Sasa tutakwenda kuwatazama watu wacheche waliorudiwa na Mungu/adhibiwa na Mungu ili tujifunze maana maandiko yanasema ‘mambo hayo yaliwpata wao kwa jinsi ya mifano yakaandikwa ili kutuonya tuliofikiriwa na miisho ya zamani.”
.
WATU WALIOADHIBIWA/KURUDIWA NA MUNGU.

1. DAUDI
Daudi ni mtu alieupendeza sana moyo wa Mungu. Lakini aliadhibiwa zaid ya mara tatu. Njia zake zilimpendeza sana Mungu lakini alikumbana na adhabu pale alipokosa wala Mungu hakumuacha tu maana alijua akimuacha vile vile ayampoteza. Tunalidhibitisha hilo..

Matendo ya Mitume 13:22 “Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona DAUDI, MWANA WA YESE, MTU ANAYEUPENDEZA MOYO WANGU, ATAKAYEFANYA MAPENZI YANGU YOTE. ”

Unaona hapa Mungu anamshuhudia daudi kabla hata hajawa mfalme kuwa anaupendeza moyo wake lakini alipokosa Bwana hakusita kumrudia.

Tunaona Mungu anamuadhibu Daudi baada ya kuwahesabu Israeli wote wakiwemo na mashujaa. Ijapokuwa watu wake wa karibu walimzuia asitende vile lakini kwa sababu alikuwa na nguvu na ndie mfalme basi ikawa hivyo. Mungu alichukizwa na hicho kitendo kikapelekea adhabu kwake na watu wote pia hata ambao hawakuwa na hatia. Lakini Daudi alikuwa ni mwepesi wa kutubu.

Unaweza ukaona ni kawaida kufanya sensa lakini ni jambo ambalo halikumpendeza Bwana maana hakutaka Daudi afanye vile (2 SAMWELI 24:1-17).

2 Samweli 24:10-13 “Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia Bwana, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.

[11] Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la Bwana likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema,
[12] Nenda, ukanene na Daudi, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo.

[13] Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.

Pia Daudi baada ya kulala na mke wa jemedari wake Uria Mhiti na mwisho kufanya njama mpaka kumuua jemedari wake hilo jambo halikuwa jema machoni pa Mungu likapelekea adhabu kuu na mbaya sana kwake.

Mungu hasapoti wala kukumbatia uovu unapokosa lazima akuadhibu haijalishi anakupenda vipi

ni vyema ukalielewa hili ndugu yangu. Lengo lake ni kukukamisha wewe na mimi.

2. ANANIA NA SAFIRA.
Tunaona mume na mke wanakumbana na adhabu ya kifo kwa kumdanganya Roho Mtakatifu. Kosa kubwa hapa watu tunadhani ilikuwa ni kuzuia sehemu ya zile fedha la! Sivyo hivyo ijapokuwa lilikuwa ni kosa pia lakini kosa kubwa hapa lilikuwa ni KUSEMA UONGO. Yaani kumdanganya Mungu mwenyewe muumba wa Mbingu na nchi yeye ambaye kwake hakuna kitu kilichotupu vyote ni wazi mbele zake.
Kosa kama hili linapelekea watu kufa usifikiri ni kawaida tu mambo tunayoyachukulia kawaida kawaida ni tofauti na jinsi Mungu anavyoyachukulia inatupaswa kuwa maini sana na Mungu atusaidie.

3. MUSA.
Musa alikuwa ni rafiki wa Mungu kiasi anaongea na Mungu ana kwa ana lakini alipotenda kosa Bwan ahakuacha kumrudia kabisa.

Tunasoma kwenye kile kitabu cha Hesabu 20:1-13 kwa kosa moja tu la kutokufuata kile alichoambiwa anasamehewa lakini Mungu anamwambia hataingia katika ile nchi ya ahadi anaambiwa asimame mlimani aiangalie kwa mbali lakini hataingia .

Ndugu yangu hebu tutafakari kwa kina hapa na kujiuliza hapa

Musa aliekuwa rafiki w Mungu anaongea nae uso kwa uso hata kuoa mahsuari kwa Mungu hasira yake ilipowaka kuwaangamiza Israeli na Mungu anawaacha kwa sababu ya yeye kuwaombea Rehema lakini anafanya kosa anaanbiwa hata nchi ya kaani hatafika.”

Mungu alikuwa amekusudia aingie na ndio maana tunaona japokuwa Musa alikuwa ana umri mkubwa lakini nguvu zake hazikupungua NI JAMBO KUTISHA SANA NA KUOGOPESHA ndugu yangu tuwe makini san asana na Neema ya Mungu iongezeke juu yetu. Ipo mifano mingi sana lakini kwa leo tuitafakari hii.

Tuwe tayari kupokea adhabu kutoka kwa Baba yetu maana anatupenda sana na hafanyi hivi kutukomoa ama kwa sababu anatuchukia la. Bali anatupenda na anatuwazia mema. Baki na hili Neno moyoni mwako.

Yeremia 29:11 “1 Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. ”

Ubarikiwe sana na Bwana YESU.
Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *