Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tujifunze maneno ya uzima ya Mwokozi wetu.
Katika kila Habari tunayoisoma katika Biblia nyuma yake kuna fundisho kubwa sana na la muhimu sana kulifahamu kwa kila Mkristo. Kila Habari imebeba ujumbe mkubwa sana nyuma yake, na bahati mbaya tunaishia kuona stori tu peke yake na hatuoni kile Mungu anataka tujifunze na kukielewa.
Na bahati mbaya tuko katika kizazi ambacho ni kivivu cha kusoma na kutafakari. Mungu kakusudia katika kila Habari nyuma yake tupate fundisho lakini kwa sababu tunakuwa ni wavivu wa kutafakari na kujifunza na Shetani anafurahia katika hilo. na anataka tuendelee kuona hizo hizo stori tu. Lakini tusifahamu fundisho lilio nyuma ya habari hiyo.
Sasa kwa neema za Bwana tutakwenda kuitazama sura hii kwa undani kabisa ili tupate fundisho lililoko nyuma yake litusaidie katika safari yetu ya wokovu.
Ni vizuri ukipata Muda upitie sura yote naamini utapata zaidi ya haya tutakayojifunza.
Katika sura hii inaanza tunamuona nabii ambae hakujulikana kwa jina lakini alikuwa ni nabii wa Mungu kweli na Mungu alimtuma kwenda kutoa unabii katika nchi ya Israeli akitokea katika nchi ya Yuda.
Ambae mfalme wake alikuwa ni Yeroboamu(Israeli)mwana wa Nebati. Mungu alimtuma akatoe unabii juu ya Mfalme Yeroboam juu ya maovu aliyoyafanya na akatoa unabii wa kuzaliwa kwa mfalme atakaekuja kutoa masamu yote. na alifanya hivyo na Mungu akathibitisha kile alichokisema kwa ishara iliyoonekana pale pale.(madhabahu ilipasuka na majivu kumwagika).
Sasa nabii huyu licha ya kutoa unabii na ishara zote zile lakini alipewa agizo na Mungu kwamba atakapomaliza kutoa unabii asiingie nyumbani mwa mtu yoyote, wala asile wala kunywa kitu chochote kwa mtu yoyote hata kwa mfalme Yeroboamu na pia asirudie katika njia ile aliyoiijia. Na mfalme Yeroboamu alimkaribisha apate chochote lakini hakukubali kufanya hivyo. Kuingia ndani mwake.
1 Wafalme 13
7 Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu.8 Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa;
9 maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la Bwana, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
Unaona kuanzia hapo kwenye mstari wa 8? Ni maagizo ambayo alikuwa amepewa na Mungu na alipaswa kuyatafa na katika eneo hili alifanikiwa wala hakuingia nyumbani mwa Mfalme kabisa.
Sasa alipotoka pale alikutana na Mtu mwingine ambae alimdamganya na akubali kuingia kwake na mwisho wa siku akaangamia kwa kuraruliwa na Simba.
NI NINI TUNAJIFUNZA KATIKA HABARI HII.
Jambo la kutafakari Sasa ni fundisho gani tunalipata katika kahabari hii na nini Mungu anachotaka tukifahamu?
TUSIPUUZE AGIZO LA KWANZA.
Wakristo wengi katika nyakati za Mwisho hizi wamekuwa ni watu wa kuupuza mambo yale Roho Mtakatifu aliyosema nao.
Kwa sababu tu mchungaji, nabii,Mwalimu, mtume amesema jambo fulani basi wanaamimi Katika hilo zaidi kuliko hata kile ambacho Roho Mtakatifu amesema nao.
Leo hii Roho Mtakatifu anakushuhudia ndani yako usivae vimini,usinyoe viduku,usiwe mtu wa anasa anasa,hubiria watu wengine injili waokoke, na ujiepushe na mahali palipo na mazungumzo mabaya, ufunge ,uingie katika maombi nk,
Lakini unasikia Mchungaji wako au mtumishi fulani wa Mungu anasema
“kwani kuvaa vimini,suruali nk ndio vinafanya usiende mbinguni? Mungu haangalii mwili mimi mwenyewe nilikuwaga najua hivyo lakini baada ya kujifunza na roho wa bwana kunifunulia nikajua sio, unaweza ukavaa vimini, ukanywa pombe nk na ukaenda mbinguni yaani Mungu akuzuie kuingia mbinguni kisa eti unavaa suruali na kupaka make-ups? Kazi ya Mungu ni kamilifu nk”
Na wewe unajikuta unaanza kusema
“ila kweli yaani Mungu alieacha enzi na mamlaka kunikomboa Mimi eti nisiingie mbinguni kisa tu Navaa wingi,suruali nk mbona haiwezekani?”
Ndugu yangu nataka nikwambie inawezekana kabisa na utaangamia. nabii huyo tulisoma alikufa kwa sababu ya kula chakula tu na kunywa maji na kuingia ndani ya nyumba tena ya nabii mwezie.
Tusome kulithibitisha hilo…
1 Wafalme 13
15 Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula.
16 Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa;
17 kwani nimeambiwa kwa neno la Bwana, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
Unaona hapo aliendelea kushikilia kile Mungu alichokuwa amemwambia kile kile alichomjibu Yeroboamu mfalme wa Isaya na ndicho anachomjibu huyu nabii mzee.
Lakini sasa ni nini kiliendelea baada ya kujibu?…….
1 Wafalme 13
18 Akamwambia, MIMI NAMI NI NABII KAMA WEWE, na malaika akaniambia kwa neno la Bwana, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. LAKINI ALISEMA UONGO.
19 Basi mtu yule akarudi pamoja naye, AKALA CHAKULA , AKANYWA MAJI NYUMBANI MWAKE.
20 Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia nabii yule aliyemrudisha;
21 akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, Bwana asema hivi, Kwa sababu UMEIASI KAULI YA BWANA , wala hukuishika amri ile aliyokuamuru Bwana, Mungu wako,
22 BALI UMERUDI, UKALA CHAKULA,UKANYWA MAJI, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako.
23 Basi ikawa, alipokwisha kula chakula na kunywa maji, yule nabii aliyemrudisha akamtandikia punda.
24 Na alipokuwa amekwenda zake, simba alimkuta njiani, akamwua. Maiti yake ikatupwa njiani, na yule punda akasimama karibu naye; na yule simba naye akasimama karibu na maiti.
Unaona hapo… nataka uone hakufa kwa sababu chakula kile kilikuwa na sumu la!. alikubali kudanganyika na akaona kwa sababu huyu ni mtu wa Mungu wacha nimfuate lakini kumbe alisema Uongo Shetani alikuwa nyuma ya uongo huo na ikapelekea mauti kwa nabii yule.
Tuwe makini katika nyakati za Hatari hizi na mbaya za kutisha ambapo watumishi wengi wa uongo wapo na wanafanya kazi kama maandiko yanavyosema.
2 Timotheo 3:1
“Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.”
Unaona kabisa Roho Mtakatifu anakushuhudia juu ya jambo fulani acha haijalishi watumishi wa Mungu wa ngapi wanasema halina shida yoyote acha mara moja. hata kama wanalisapoti sikiliza agizo kuu ulilopewa usilipuuze hata kidogo.
Unaona waimbaji wa nyimbo za injili wamevaa vibaya na kupaka make-ups, nguo zina mipasuo mikubwa kabisa,wamenyoa style za kidunia na wanaimba uwepo wa Bwana unashuka, usiwaige ndugu yangu hizi ni nyakati za Mwisho okoa roho yako.
Baki katika kumtii Roho Mtakatifu kwa kile alichokuagiza haijalishi watu watakaokupinga ni wangapi usiwatazame muangalie yeye aliekufia pale msalabani anasema nini juu ya hicho, usilazimishie utaangamia.
Ubarikiwe sana.
Maranatha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.