Nakusalimu katika Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
Kuna funzo kubwa sana Mungu anatamani tulifahamu katika habari ile ya mwanamke msamaria na Bwana Yesu pale kisimani. Wengi wetu huwa tunaisoma na kuona ni Habari ya kawaida tu lakini sivyo.
Swali hili tujiulize/nikuulize “Je inahitaji kipindi fulani kipite katika wokovu ndio tumtumikie Mungu?”
“Au je unahitaji kipindi fulani katika wokovu ili umtumikie Mungu?”
Jambo hili limekuwa ni udhuru/kisingizio kikubwa cha Wakristo wengi katika kuifanya kazi ya Mungu.
Leo hii Mkristo amekaa katika imani kwa kipindi Karibu mwaka mzima lakini bado anajiona yeye ni mtoto mchanga hawezi kumtumikia Mungu anataka kuendelea kulishwa tu. Anasubili mpaka apate maarifa mengi ya kutosha ili aweze kumtumikia Mungu(kuwahubiria injili wengine).au anasema mimi sio karama yangu hiyo..
Lakini kibiblia hili jambo likoje? Je! Yesu amekusudia iwe hivyo? Jibu ni la!
Tukisoma kwenye kitabu cha injili ya Yohana Mtakatifu katika ile Habari ya mwanamke msamaria aliekuwa akichota maji kisimani na Yesu alipomwendea na kumuomba ampe maji.
Katika mazungumzo yale waliokuwa wakizungumza wengi huwa tunayaona yalikuwa ni mazungumzo ya kawaida tu wanabadilishana mawazo lakini pale Yesu Kristo alikuwa anamhubiria INJILI mwanamke yule.Na yule mwanamke aliamini na akaokoka.
Tuisome kidogo Habari hiyo kwa ufupi na tuone mwanamke yule baada ya kuamini ni nini alichokifanya baada ya kumwamini Yesu kuwa yeye ndio Mtiwa mafuta(Masia) wa Mungu.
ili kuelewa Habari hii Soma YOHANA 4:7-27 lakini tutasoma mistari michache tu hapa usiwe mvivu wa kusoma fungua biblia yako..
Yohana 4
14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.
15 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.
Ukianza mstari wa saba utapata mtiririko wa Habari hiyo vizuri.
Baada ya hapo tunamuona Bwana Yesu anaanza kumfunulia siri zake zote na yule mwanamke akadhani ya kuwa Yesu ni nabii tu lakini alifuliza kumhubiria pale walipokuwepo..
Sasa baada ya hapo tunaona mwisho Yesu anamwambia kuwa yeye ndio Masihi mwenyewe yaani mtiwa mafuta wa Mungu..
Yohana 4
25 Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote.
26 Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye.
27 Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye?
Hivyo baada ya wanafunzi kuja tayari mwanamke yule alikuwa ameshaamini injili ya Yesu Kristo yaani ALIOKOKA saa ile ile.
NINI KILITOKEA BAADA YA MWANAMKE MSAMARIA KUAMINI(KUOKOKA)?
Sasa tuangalie vizuri kwa makini ni kipi kilitokea baada ya mwanamke yule kupokea injili?
Yohana 4.
28 Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu,
29 Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?
30 Basi wakatoka mjini, wakamwendea.
Soma kwa makini mstari huo wa 30 unaona baada ya kutoka pale kisimani tu alienda mjini kuwaambia watu.. wengi wetu tunaposoma mstari huu tunadhani yule mwanamke alikuwa anataka na wale wengine waambiwe mambo yao lakini haikuwa hivyo.
Mwanamke huyu alimtambua Yesu ndio Masihi mwenyewe hivyo alitaka watu wamjue wote kuwa yeye ndio Mwokozi wa ulimwengu huu ndio kusudi kubwa la mwanamke yule..
Unaona baada ya kupokea injili anakwenda muda huo huo kuwahubiria watu waje kwa Kristo na watu wakamfata Yesu. (Kuna mambo unaona kama hayawezekani lakini yanawezekana kabisa)
Sura hii yote ukisoma kwa makini mpaka mstari ule wa 40 inazungumzia haswa utendaji kazi wa Mkristo pale anapookoka.
Mwanamke huyu hakusubili apate ujuzi na maarifa mengi sana. Wala hakusubili aambiwe yeye mwenyewe alitoka kwenda kushuhudia Habari njema.
Na watu wale waliokoka wote..
Yohana 4
41 Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake
42 Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.
Unaona hapo??? watu hao wanasema “…twajua ya kuwa hakika huyu ndie MWOKOZI WA ULIMWENGU “
kumbuka kazi ya kuwafanya watu waamini si yako ni ya Mungu kazi yako wewe ni kama huyu mwanamke alivyofanya kuwahubiria injili tu.
Yohana 4:39
“Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda.”
Unaona hapo yeye aliwashudia tu juu ya kile Yesu alichokifanya na maneno ya uzima aliyoyasikia kwake na akasikia roho yake kuhuishwa ndani yake..
Kumbuka agizo kuu tulilopewa watu tuliomwamini Yesu Kristo ni kuwahubiria wengine habari njema za Kristo. Je unalitimiza agizo hilo? Siku ile utaulizwa na Bwana kama uliingia shambani mwake kuvuna au hukwenda na kwa nini??
Usiseme mimi siwezi au ni kazi ya mchungaji na watumishi wa kanisani ndugu umempokea Yesu ni kazi yako pia kufanya hivyo..
Yesu anasema mavuno tayari yamekwisha kuiva kazi yetu ni kuchukua mundu na kuyavuna je unataka pia na mundu ushikiwe na uvuniwe??
Yohana 4.
35 Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno.
36Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja.
Soma vizuri huo mstari wa 36 anasema “….Avunae hupokea Mshahara..” kumbe hakuna kupokea Mshahara pasipo kuvuna au kufanya kazi. Jiulize thawabu yako utakuwa ni nini katika siku ile.?
Hujawahi kumhubiria mtu na kumvuta kwa Kristo utalipwa nini siku zile? Umekaa kwenye wokovu kwa muda gani? Na kipi unasubiria kuifanya kazi ya Mungu? Je bado unajiona huwezi na wakati umepewa Roho Mtakatifu vipi kama usingelipewa?
Agizo kuu ni hili….
Mathayo 28:19
“Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;”
Litimilize agizo lako kuu ulilopewa kama mwamini Mwanamke yule aliokoka siku ile ile akafanya kazi ya Mungu je ? Toka lini umeokoka na hutaki kuifanya kazi ya Mungu uko bize na kazi za ulimwengu huu ambazo hazidumu milele??
Kumbuka kazi ya Mungu inadumu milele na matunda utakayoyapata katika wokovu wako ni wa milele si kazi uliyonayo ambayo unaona umebanana huwezi hata kuwahubiria wafanyakazi wenzako .
Usiwe mvivu fanya kazi ya Mungu watu waokolewe kupitia wewe katika eneo hilo ulilopo kuna watu wanakufa na kwenda kuzimu kwa sababu ulitakiwa uwahubilie waokoke lakini umekaa kimya. Usikae kimya tena MTANGAZE YESU KRISTO.
Ubarikiwe sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.