
JIWEKENI TAYARI!! JIWEKENI TAYARI!!
Mathayo 24:43-44 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.
[44]Kwa sababu hiyo ninyi nanyi JIWEKENI TAYARI; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.
Unaelewa maana ya kujiweka tayari?
Ili kuelewa vizuri, hebu tafakari kuhusu wanariadha, wakati wamejipanga kwenye mstari kusubiri filimbi ya mwisho… huwa mawazo yao na akili yao yote inakuwa pale kwenye hilo tukio, kwani ikitokea mtu amezubaa tu kidogo wakati wa filimbi ya mwisho kuna uwezekano akaachwa nyuma, hivyo hana budi kujiweka tayari muda wowote kwa kuwa MACHO.
Hali kadhalika na sisi wakristo tunafananishwa na wanariadha, Neno la Mungu linasema katika…
1 Wakorintho 9:24-25
[24]”Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? PIGENI MBIO NAMNA HIYO, ili mpate.
[25]Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.”
Hivyo basi, kama vile wanariadha waliojiweka tayari kusubiria filimbi ya mwisho…nasi pia tunaambiwa tujiweke tayari.. maana parapanda ya mwisho italia wakati wowote!
1 Wakorintho 15:51-52 Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,
[52]kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; MAANA PARAPANDA ITALIA, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.
“Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari;..”
Uwapo kazini, shuleni, sokoni, njiani, kuwa kama mwanariadha anayesuburi filimbi ya mwisho.. Maana filimbi/parapanda ya mwisho italia muda wowote, na ikilia huku mawazo yako na moyo wako upo kwenye vitu vya kidunia, au mbali na tukio hili linaloenda kutokea hivi karibuni, basi kuna uwezekano ukabaki..hata kama unakumbukumbu nzuri za kumpendeza Mungu.
Na itakuwa ni uchungu mwingi sana zaidi ya kupoteza mtoto, mzazi, mume/mke au ndugu wa karibu…siku hiyo utajuta sana, sio tu kwasababu ya dhiki utakazokumbanazo, ila pia utalia na kujuta sana kwasababu umeachwa na hukupaswa kuachwa.
Ukitazama ni siku chache tu nyuma ndio ulianza kupoa, utajisikiaje? Ukitafakari sasa wenzako wanafutwa machozi mbinguni na wewe umebaki ukingojea dhiki kuu na chapa ya mnyama na ziwa la moto milele?, ukitafakari ni tamaa na kutokuwa na kiasi ndio iliyokuponza, mke au mume unayeishi naye ndio aliyekuponza, binti/kijana unayetembea naye ndiye aliyekuponza, utafutaji mali uliopindukia ndio iliyokuponza, miziki ya kidunia, tamthilia, ushabiki, na anasa za kidunia ndivyo vilivyokuponza kuikosa mbingu, utakuwa katika huzuni kubwa kiasi gani.
Siku hiyo utakapoona mwanao hayupo, dada yako aliyekuwa ameokoka hayupo, mchungaji wako hayupo, na wewe umeachwa! Itakuwa ni uchungu kiasi gani?. Ukitazama ni masaa machache tu nyuma umetoka kupokea rushwa, ukitazama ni masaa machache tu nyuma umesikia mahubiri ya kukuonya na ulimwengu ukakataa ukaendelea kuvaa vimini na masuruali na kujitia mapambo ya kidunia, Ukitazama ni wiki chache tu nyuma uliota ndoto inayokuonya kwamba hizi ni siku za mwisho ukapuuzia. Masaa machache tu ulisikia mahali panazungumziwa habari za unyakuo ukaendelea kuwa bise na mambo yako..hukutaka kujiweka tayari.
Ndugu katika Bwana jiweke tayari!! jiweke tayari!! Parapanda ya mwisho italia muda wowote..kwani ishara zote zinaonyesha kuwa Bwana yupo karibu.
Lakini kama hujaokoka…yaani hujampokea Bwana Yesu kweli kweli, ni wazi kuwa huwezi kujiweka tayari maana haupo miongoni mwa wateule/wanariadha. Lakini fahamu kuwa yapo madhara makubwa mno ambayo yatakukumba baada ya unyakuo wa watakatifu. Ni heri leo ukafanya maamuzi sahihi ya kumpokea Yesu ili uwe miongoni mwa wateule watakaosikia sauti ya parapanda.
Fahamu kuwa pasipo kumpokea huyu Yesu.. hautakuwa na tumaini kabisa katika safari ya uhai wako, kwani baada ya haya maisha… mwisho utaenda kuangamia kwenye ziwa la moto… hivyo tumaini pekee ni Yesu Kristo, pasipo yeye.. maisha mengine hayana maana.
Je! upo tayari kumpa Yesu maisha yako leo, kama ni ndiyo na unahitaji msaada basi wasiliana nasi kwa namba zilizoko chini ya makala hii.. nasi tutakusaidia.
Ubarikiwe sana.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa Mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.